Home Latest News MAAGIZO KUTOKA JUU ‘UGONJWA’ UNAOWATAFUNA WATUMISHI WASIOJIAMINI

MAAGIZO KUTOKA JUU ‘UGONJWA’ UNAOWATAFUNA WATUMISHI WASIOJIAMINI

2920
0
SHARE
Rais John Magufuli

NA HILAL K. SUED

Agizo la Rais John Magufuli wiki iliyopita kwamba wakuu katika utumishi wa umma na watendaji wengine katika utawala wawajibike katika maamuzi yao pamoja na hatua mbalimbali wanazochukua na waache kumshirikishe yeye kama ndiye aliyewaagiaza, ni agizo la kupongezwa sana.

Katika risala yake kwa Watanzania kuwashukuru kwa ushirikiano waliouonyesha katika mwaka uliopita na kuukaribisha mwaka mpya 2019, Rais Magufuli aliwaonya watendaji wake wakiwemo watumishi wa umma wasiojiamini, na ambao wamekuwa wakipendelea kutekeleza majukumu yao kwa kusingizia kwamba wanatekeleza hayo kwa maelekezo kutoka juu.

Rais alisema “upo ugonjwa ambao umeanza kuwapata watumishi wa umma ambao wamekuwa wakipendelea kusingizia kwa kila wanalolifanya kusema ni maagizo kutoka juu hata kama ni kwa mujibu wa sheria.”

Kwa tafsiri nyingine ni kwamba watumishi wa umma wasiwe wanajificha katika kivuli cha rais kama kinga na kwamba endapo wanayavurunda mambo, basi wao wenyewe ndiyo wa kubeba msalaba.

Hii ni ishara kwamba kama agizo litazingatiwa kwa vitendo sasa hivi utawala wa sheria utaanza kudumishwa kwa vitendo, na si kwa maneno ya majukwaani kama ilivyokuwa imezoeleka. Na hili ni ishara njema ya kudumisha amani na utulivu iliyopo.

Siku za hivi karibuni vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kuibuka, katika baadhi ya mikoa, migongano ya kiutendaji na kimaamuzi baina ya wateule wa rais – hususan baina ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Kwa mfano, maamuzi ya Mkuu wa Mkoa mmoja yamekuwa yakipuuzwa/yakipingwa na baadhi ya wakuu wake wa wilaya – suala ambalo kwa bahati mbaya limetinga katika ufahamu wa umma.

Inawezekana sababu kubwa la hili kutokea ni kwamba watendaji wa ngazi zote mbili ni wateule wa rais. Kutokana na hali hii, kwa mkuu wa wilaya kwa mfano, huenda anajiona naye anawajibika kwa rais pia, na hiuvyo Mkuu wa Mkoa hawezi akamwambia kitu.

Lakini hilo ni moja na linatakiwa kutatuliwa kwa haraka kabla mambo hayajaharibika zaidi. Lakini kufuatana na agizo la Rais ni kwamba uamuzi wowote wa wakuu hawa katika utendaji wao utokane na wao wenyewe, na uzingatie sheria na kanuni zilizopo kama kinga iwapo mambo yataharibika, na si kusema ni maagizo kutoka juu hivyo kufikiria kinga itatoka juu pia iwapo mambo yataharibika.

Na hili si kwa wakuu wa wilaya au wa mikoa tu bali hata kwa watendaji wengine katika vyombo muhimu vya dola kama vile vya ulinzi na usalama – hususan Jeshi la Polisi. Jeshi la polisi ni chombo ambacho kina mahusiano (interaction) makubwa sana na raia katika utendaji wao wa kila siku na ndilo linapaswa kuzingatia haki katika maamuzi – kwani raia hujenga imani kwamba wao hufuata sheria na kanuni zilizopo na si kutokana na matakwa au mihemuko tu ya wakuu wao, hususana wale wa siasa – jambo ambalo linaweza kuibua kuoneana na hivyo haki za raia kuathirika.

Sasa hili suala la utawala unaoizingatia sheria maana yake ni hiyo hiyo, kuzingatia sheria na si vinginevyo. Kwa mfano baada ya agizo la rais Magufuli wananchi wengi wanatarajia kwamba Mkuu wa wilaya anapoamrisha polisi kumuweka mtu ndani basi awe anataja kwamba agizo lake hilo analitoa chini ya kipengele na sheria ipi ya nchi. Bila ya hivyo basi agizo lake hilo litaonekana ni amri tu isiyokuwa na kinga ya sheria yoyote ya nchi.

Au kwa mfano Mkuu wa polisi wa Wilaya anapoingilia mkutano wa ndani wa chama cha siasa na kuusambaratisha na hata kuwatia mbaroni viongozi wake, basi awe anataja kwamba anachukua hatua hiyo kufuatana na kipengele na sheria fulani ya nchi.

Nimeacha kimakusudi tu kutaja mikutano ya hadhara na maandamano kwa sababu mikusanyiko hii inahitaji usimamizi na ulinzi madhubuti wa polisi, ambao ndiyo hutoa ruhusa ya kufanyika na sababu ambazo huwa wanazitoa za kukataa kwamba hawawezi kutoa ulinzi wa kutosha ni vigumu kuzipinga hata kama inawezekana zikawa siyo za kweli.

Agizo la Rais Magufuli la kukataa kuwa kinga kwa maamuzi ya watendaji wake pia una maana kwamba watendaji hawa wanapoboronga na pengine kuingilia haki ya mtu mwingine, huyo mtu awe na haki ya kumshitaki mtendaji huyo mahakamani katika utaratibu wa kesi za kawaida za madai. 

Na iwe hivyo hivyo kwa upande wa Polisi – raia awe na haki ya kufungua mashitaka iwapo ataona ameonewa kwa kiasi kikubwa bila sababu yoyote – mbali na wao kuwajibishwa na dola. Turudi nyuma katika historia yetu kwani hayo yaliwezekana na yalikuwa yakitokea.

Katika ya 70 polisi walikuwa wanawajibishwa vilivyo kwa matendo yao, hasa wanaposababisha vifo vya raia wakiwa mikononi mwao bila sababu za msingi. Baadhi ya maafisa wa polisi wa vyeo vya juu na wale wa Idara ya Usalama walikamatwa na kushitakiwa mahakamani kwa makosa ya utesaji wa raia na hata kwasababishia vifo katika mikoa ya kanda ya Ziwa (Shinyanga na Mwanza).

Leo hii ni vigumu kitu kama hicho kufanyika na mara ya mwisho ilikuwa mwanzoni tu mwa utawala wa Awamu ya Nne pale baadhi ya maafisa wa polisi waliposhitakiwa kwa kuwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa Mahenge na dereva mmoja wa texi. Kuna mmoja alipatikana na hatia na kuhukumiwa kunyongwa – hukumu ambayo ilithibitishwa na Mahakama ya Rufaa Septemba mwaka 2016.

Na katika enzi hizo hizo za miaka ya 70 wakuu wa polisi walikuwa wanajibishwa kwa matendo yao wenyewe binafsi. Aliyekuwa  Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Hamza Azizi, akiwa anaendesha gari lake usiku alimgonga mtu mmoja ambaye alikufa hapo hapo. Hakujali kitu na hata hakuripoti polisi usiku ule hadi siku ya pili yake, bila shaka baada ya kushauriwa na maafisa wenzake ndipo alipokwenda kutoa ripoti kituo cha polisi.

Hayo yalikuwa enzi hizo. Sasa hivi inashangaza kuona serikali inatafuta njia ya mkato ya ‘kusimika’ amani na utulivu bila kwanza kutafakari kwa kina kwa nini amani hiyo inaweza kupotea nchini. Suala la ‘amani na utulivu’ ni suala la pande mbili – yaani raia na serikali yenyewe. Pande zote hizi mbili zinawajibika katika kuijenga na kuirutubisha amani hiyo.

Lakini cha ajabu ni kwamba siku zote watawala wetu hupenda ionekane kwamba suala la amani ni wajibu wa raia peke yao – yaani wao pekee ndiyo huwa watuhumiwa wakubwa wa kutoweka kwa amani na si serikali pamoja na vyombo vyake vya dola.

Tukubaliane kitu kimoja – kwamba katika nchi yoyote duniani amani hailetwi kwa kusisitizwa au kuimbwa majukwaani, au hata kwa mahubiri katika majumba ya ibada.

Aidha, si kitu cha kutamka mithili ya maagizo katika Taurati kuhusu kuumbwa kwa dunia “..na iwepo amani” na kweli ikawepo! Amani hujengwa kutokana na misingi madhubuti ya haki na usawa na kuisimamia kwa dhati misingi hiyo, na pia kuzisimamia vyema taasisi zinazosimamia misingi hiyo. Kama misingi ya haki haisimamiwi vizuri na kuanza kuporomoka amani inakuwa mashakani.