Home Habari Maalim Seif ataka mdahalo na Dk. Shein

Maalim Seif ataka mdahalo na Dk. Shein

1925
0
SHARE

MWANDISHI WETU

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamadi ameomba kupatiwa mdahalo na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein ili kila mmoja wao aeleze ukweli kuhusu rasilimali za Zanzibar.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki katika mkoa wa Mjini Magharibi Unguja wakati akiwa katika ziara ya ujenzi wa chama baada ya kumaliza mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema kwa kuwa Rais Dk. Shein naye atakuwa kwenye ziara ya kiserikali na kichama hivi karibuni, anamtaka ajibu baadhi ya hoja ambazo wananchi wanatatatizwa nazo.

“Atuambie mafuta yetu kwanini yameuzwa. Kwa sababu alisema tumefanya jambo hili kiharaka, si kweli… siku ya kutia saini alialika televisheni lakini waliokuwepo hawakuona kilichomo ndani ya mkataba.

“Tunataka tujue kilicho ndani ya mkataba, tatuweke wazi. Tunajua rasilimali ya Zanzibar ni muhimu kuliko chochote,” alisema.

Aidha, pia alisema Dk. Shein aweke wazi kama anaweza kuzuia ujio wa serikali moja lakini pia aeleze matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kuwa kwanini yalifutwa.

“Atueleze uwezo wa kufuta umetokana na kifungu kipi cha katiba yetu.  Tuambie kifungu… Hayo ni mambo ya kuwaambia wazanzibar akianza ziara yake.

“Kama mimi ni muongo basi tufanye ‘debate’ mdahalo kwenye tevelesheni, nimchane tujue nani mwenye hoja,” alisem Maalim Seif.

Aidha, pamoja na mambo mengine alidai kuna mikakati inapangwa kuwapokonya chama hicho na kuongeza kuwa njama hizo hazitafanikiwa wala kuwavunja nguvu ya kudai haki yao mahala popote.

 “Ninafahamu zipo njama mbalimbali zenye lengo la kunyang’anywa chama na kundi linalomuunga mkono mwenyekiti wa zamani Profesa Ibrahim Lipumba.”

“Hata kama watafanikiwa hatutanyamaza tutaendelea na harakati za kudai haki kwa misingi ya kikatiba kwani ndiyo kazi ya siasa,” alisema.