Home Habari MAALIM SEIF: CAG ametimiza wajibu wake

MAALIM SEIF: CAG ametimiza wajibu wake

1888
0
SHARE

MWANDISHI WETU

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amemtaka Spika wa Bunge Job Ndugai kutambua kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad alitimiza wajibu wake katika kutoa maoni hivyo hapaswi kufika mbele ya kamati ya maadili ya Bunge kama alivyoagizwa.

Akizungumza na RAI akiwa Visiwani Pemba, Seif alisema, ”CAG kueleza kuwa ripoti yake haijafanyiwa kazi ni kutokana na Bunge kuwa dhaifu, halaumiki kwani mtu akifanya kazi nzito halafu akagundua wahusika wanaburuza miguu katika kutekeleza yale yaliopendekezwa kunamfanya mtu yeyote ahisi kazi yake haikuthaminiwa,” alisema.

Aidha, alisema uamuazi wa CAG kutoa KAULI ILE hakukosea kwa kuwa Bunge limekuwa na wabunge wengi wa chama tawala ambao hawathamini michango ya wabunge wa upinzani hata kama mawazo hayo ni mazuri.

“Nafasi ya CAG ni muhimu sana kiasi kwamba CAG hawezi kuondolewa ovyo ovyo na Rais. Spika anaposema anaweza kumkamata na kutiwa pingu ni kumdhalilisha CAG, lakini pia na ofisi yenyewe ya CAG.

“Spika atakiwe kumuomba radhi CAG hadharani kama alivyomdhalilisha hadharani!

“Unafikiri ripoti za aina hii (za ukaguzi za CAG) hufanyika siku moja au mbili? Hapana. Hutumia zaidi akili na muda, ndiyo maana inaumiza sana mwisho wa siku huoni hatima ya ripoti, unadhani Profesa Mussa atasemaje kama sio udhaifu wa Bunge,” alisema Maalim Seif.

Sakata lilvyoibuka

Januari 7 mwaka huu Spika Ndugai alisema Profesa Assad anatakiwa kufika mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge kwa hiari yake Januari 21, mwaka huu kutokana na kauli yake inayodaiwa kuwa amelidhalilisha Bunge.

Licha ya CAG pia Spika Ndugai, alisema Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee naye anatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Januari 22, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Spika Ndugai, alisema kuwa Profesa Assad amelidhalilisha Bunge.

Alisema CAG Assad, akiwa nje ya Tanzania wakati anahojiwa na Idhaa ya Kiswahili Redio ya Umoja wa Mataifa (UN), alisema Bunge la Tanzania ni dhaifu.

“Kama ni upotoshaji basi CAG na ofisi yake ndiyo wapotoshaji, huwezi kusema nchi yako vibaya unapokuwa nje ya nchi, na kwa hili hatuwezi kufanya kazi kwa kuaminiana,” alisema Ndugai.

Ndugai alisema kitendo hicho kimemkasirisha kwani hakutegemea msomi kama huyo angeweza kutoa maneno ya kudhalilisha Bunge lililojaa wasomi zaidi ya mabunge yote tangu uhuru.

Itakumbukwa kuwa Desemba mwaka jana Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda, alimuuliza CAG kuwa ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.

Katika majibu yake CAG alisema. “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge, kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

“…Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika, ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa,” alisema CAG Assad

Katika majibu yake kwa swali hilo aliendelea kusema kuwa “Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua.”

Hata hivyo mwaka jana lilipoibuka suala la upotevu wa Sh1.5 trilioni kwenye hesabu za Serikali mwaka wa fedha 2016-2017, Assad aliulizwa kuhusu nini kifanyike, akataka Bunge liulizwe kwani ndilo lenye kutakiwa kuibana Serikali kuhusu kutoonekana kwa fedha hizo.

Kutokana na mahojiano hayo Spika Ndugai, alisema kuwa kama CAG anasema Bunge ni dhaifu basi mpotoshaji mkubwa atakuwa CAG na wafanyakazi wake.

“Kwa hiyo sasa na kwa mujibu wa kinga madaraka na haki za Bunge kwa sheria za Tanzania. Na Kwa mujibu wa mamlaka niliyonayo kama Spika, Kifungu cha 4, kifungu kidogo cha kwanza (a) cha nyongeza ya nane ya kanuni za kudumu za Bunge, Toleo la Januari mwaka 2016.

“Suala hili nalipeleka kwenye kamati ya haki, maadili na madaraka ya Bunge, ili waweze kulifanyia kazi. Kwa hiyo CAG Profesa Assad anapaswa kufika kwenye kamati Januria 21 mwezi huu nakazia wito huu atokee tarehe 21 na ajitokeze kwenye kamati na kuthibitisha maneno yake ya huko Marekani.

“Na mnafahamu pamoja na hatuna polisi, lakini tuna uwezo wa kumleta mtu kwa pingu kwa hiyo natumaini wito huu, atauzingatia kwa sababu nataka kumhakikishia sisi si dhaifu,” alisema Spika Ndugai.