Home Habari Maalim Seif: CCM ina hofu kubwa 2020

Maalim Seif: CCM ina hofu kubwa 2020

2933
0
SHARE

Kulitoka kulia ni Maalim Seif akiwa na Rais wa Liberia, George Weah; Rais wa Gambia, Adama Barrow; Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini Mali, Soumaila Cissé na Waziri Mkuu wa zamani wa Guinea ambaye sasa ni Kiongozi wa Upinzani nchini humo, Cellou Diallo.

NA MWANDISHI WETU

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amekutana na viongozi mbalimbali wa vyama vya kiliberali kutoka nchi mbalimbali duniani na kuelezea hali ya kisiasa nchini pamoja na kubainisha athari za Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa uliofikia hatua ya kupokea maoni ya wananchi, wadau wa siasa na sheria.

Seif ambaye pia aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui kuelekea Dakar nchini Senegal, alitoa kauli hiyo wakati akishiriki mijadala mbalimbali ya kisiasa katika Mkutano Mkuu wa 62 wa Liberal International ambapo pamoja na mambo mengine alibainisha taswira halisi ya kidemokrasia nchini tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Akizungumzia muswada huo, Seif alisema muswada huo umebainisha kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa ndio atakayeamua viongozi gani waendeshe chama.

Pia umebainisha kuwa muungano wa pamoja vyama vya siasa kwa mujibu wa muswada huo ambao umekwenda bungeni ni kwamba vyama ambavyo vinataka kuungana lazima vipate idhini ya waziri ambaye ni CCM.

“Zaidi muswada huu unasema mtu akiacha chama chake hatoruhusiwa kugombea nafasi yoyote mpaka mwaka mmoja upite, labda kuna hofu CCM kuwa mwaka 2020 huenda wakawatema baadhi ya wabunge ambao sasa wanawazuia hata kwenda upinzani kwani hawataweza kugombea.,” amesema.

Maalim Seif pia alipewa heshima ya kuhutubia Mkutano huo wa siku mbili uliofanyika Novemba 30, na Disemba mosi mwaka huu pia aliongeza kuwa yanayotokea sasa nchini katika hali ya kisiasa hayajawahi kutokea.

“Suala zima la vyama vya upinzani kuzuiliwa kufanya shughuli za kisiasa ni jambo la kushangaza kwa sababu vyama vinahitaji wafuasi. Pia tunakandamizwa sana.

“Kwetu CUF tumepandikizwa Prof. Lipumba nadhani alishawishiwa na CCM atoke CUF katika kipindi kigumu sana. Walidhani akitoka Lipumba atatoka na makundi ya watu lakini akatoka peke yake.

“Sisi tuna wabunge na madiwani, ila msajili alizuia ruzuku, nilimwandikia barua akasema tuna mgogoro. Lakini cha ajabu alimpa Lipumba zaidi ya sh bilioni ndio maana tukaenda mahakamani kuzuia utolewaji wa ruzuku hiyo,” alisema

Katika mijadala hiyo, Maalim aliungana na Rais wa Liberal International, Juli Minoves na Makamu wawili wa Liberal International, Karl Heinz Paque na Abir Al-Sahlani.

Mkutano Mkuu huo ulishirikisha wajumbe takribani 300 kutoka vyama vya kiliberali vya nchi mbalimbali duniani kutoka Amerika ya Kaskazini na Kusini, Ulaya, Afrika, Asia na Australia.

Rais wa Senegal, Macky Sall; Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara; Rais wa Gambia, Adama Barrow;  Rais wa Liberia, George Weah pamoja na Waziri Mkuu wa Ubelgiji Charles Michel ni miongoni mwa waliohudhuria mkutano mkuu huo wa Liberal International.

Mbali na kushiriki Mkutano Mkuu huo uliofanyika kwa siku mbili mfululizo, Maalim Seif na Naibu wake pia walishiriki  Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama cha APR cha Rais wa Senega, Macky Sall ambao ulimthibitisha Rais huyo kuwa mgombea urais wa Senegal kwa kipindi cha pili katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika mwezi Februari, 2019.

Viongozi wengine walioshiriki ni Mmusi Maimane ambaye ni Kiongozi Mkuu wa upinzani nchini Afrika Kusini, Hans van Baalen ambaye ni Rais wa Alliance of Liberals and Democrats in Europe (ALDE) na pia Mbunge mashuhuri wa Bunge la Umoja wa Ulaya.