Home Habari Maalim Seif nguli wa siasa Tanzania

Maalim Seif nguli wa siasa Tanzania

1216
0
SHARE

Na Balinagwe Mwambungu

Seif Sharif Hamad ni jina ambalo limekuwa midomo ya wanasiasa na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwa muda mrefu—nadhani zaidi ya miongo minne sasa. Tukisema ni mwanasiasa nguli, hili halina ubishi, lakini binafsi nawashangaa wanaompakazia mambo ambayo sio yake, ili aonekane kwamba hafai kuwa kiongozi wa juu katika nchi—hususan kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar.

Tulipokuwa kwenye mfumo wa chama kimoja, yaani tangu 1977 ambapo Chama cha Mapinduzi (CCM) kilizaliwa, Seif alikuwa miongoni mwa vijana waliokuwa wanaaminiwa na Mwalimu Julius Nyerere, Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho. Alishika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Uchumi na Mipango (1982-87). Alikuwa Memba wa Baraza la Mapinduzi (Elimu) na kati ya wanzilishi wa Baraza la Wawakilishi 1980, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (1977-87).  Baada ya Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe na na Waziri Kiongozi, Ramadhan Haji Faki, kuvuliwa uongozi (1984) kwa kile kilichoitwa ‘uchafuzi wa hali ya hewa’ Zanzibar, Seif Sharif Hamad akawa Waziri Kiongozi chini ya Rais wa Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi. Mwaka 1988 alivuliwa uwanachama wa CCM.

Seif Sharif Hamad, kwa itikadi aliyonayo, ni muumini wa umoja wa taifa na mpenda amani. Hakukubaliana na Mzee Jumbe kuhusu mpango wake wa siri ya 1+1= 3 aliokuwa anautayarisha, Wakati huo Tanzania ilikuwa kwenye mfumo wa chama kimoja. Jumbe alitaka serikali tatu. Jambo hili lilimwudhi sana Mwalimu Nyerere na akaamwadhibu Mzee Jumbe kwa kutomruhusu kukanyaga Zanzibar na kumvua madaraka yote ya Makamu wa Mwenyekiti wa CCM, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar.

Bila Seif na wenzake kumpelekea Mwalimu Nyerere taarifa ya 1+1 ni 3, leo tungekuwa tunazungumza mengine—maana ilichukuliwa kwamba kitendo hicho kilikuwa sawa na uhaini. Kwa maana nyingine ni kwamba Seif na wenzake, walioukoa Muungano.

Seif Sharif Hamad, sasa almarufu kama Maalim Seif, anasingiziwa kwamba akichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, atauvunja Muungano! Tanzania ilipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi, Seif na wenzake ambao tayari walikuwa kwenye vuguvugu la mabadiliko, wakaungana na wenzao upande wa Tanganyika, wakaunganisha nguvu na kuunda the Civic United Front (CUF), kama kinavyojulikana sasa. Zanzibar wakati huo ikiwa chini ya mbabe Rais Salmin Amour. Maalim Self akaunganisha nguvu na wenzake kwenye UKAWA (Umoja wa Katiba ya Wananchi) mwaka 2015, lakini wapinzania waje wanasema ni mbinafsi!

Maalim Seif akaingia katika kinyang’anyiro cha kiti cha Rais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza mwaka 1995. Tangu hapo amekuwa akiteuliwa na CUF kugombea kiti cha Rais wa Zanzibar. Mara ya mwisho ni Uchaguzi Mkuu wa 2015, ambao ulifutwa kibabe na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uhaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Kwa nini wahafidhina wa CCM Zanzibar wanamwogopa Maalim Seif? Wanasingizia kwamba ana asili ya Kiarabu. Eti akishika usukani wa nchi, atawaleta wajomba zake wa Kiarabu waliotimimuliwa mwaaka 1964! Lakini viongozi hao hao wakishashika madaraka hutembelea Falme za Kiarabu, na kuwabebembeleza waje kuwekeza Tanzania, hususan Zanzibar.

Hoja ya damu ya Kiarabu haina mashiko, wako watu katika serikali ya Zanzibar ambao ni damu ya Kiarabu zaidi kuliko Maalim Seif. Kwa nini Seif anaogopwa? Ni swali ambalo linapaswa kujibiwa na viongozi wa CCM wenyewe.

Lakini kimantiki, watawala hawataki mabadiliko kwa sababu wameshaona utamu wa kushika hatamu. Wanasema mapinduzi daima, kwa sababu waliondoa usultan wa Kiarabu, wameleta usultan wa Kiafrika—kupeana  madaraka wao kwa wao—Waingereza wanasema ‘self-preservation’ (kujikinga) na siajabu katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 wakaja na jina la mmoja kutoka majina ya waliokuwa viongozi wa Zanzibar—ni muendelezo ule ule.

Sasa mbinu mpya ni kumwondoa Maalim Seif kabisa kwenye ulingo wa kisiasa, maana wanajua yeyote atakaye simamishwa atashindwa. Wamefanikisha kuwafarakanisha viongozi wa CUF na Maalim kabwaaga manyanga. Kuna madai ya kwa nini Maalim Seif amekuwa akigombea urais wa Zanzibar miaka yote—1995, 2000, 2010 na 2015. Wanajua yeyote watakaye msimamisha kupambana na Maalim, atabwagwa tu—njia iliyobaki ni kumnyima nafasi hiyo—asiwe na chama.

Jibu ni rahisi tu, bila chama, Maalim Seif atakua hana nguvu kubwa kisiasa Zanzibar na ndio utakuwa mwisho wake. Maana mara zote amekuwa akiwashinda kama ilivyodhihirishwa na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2015. Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla walionesha mwaka 2015 kuwa wanataka mabadiliko.

Mtu kugombea urais mara nyingi sio dhambi na wala Maalim Seif sio wa kwanza kufanya hivyo. Abdoulaye Wade, wa Senegal, alikuja kufaulu kuukwaa urais baada ya miaka mingi, ikiwa ni pamoja na kutungiwa kesi ya uhaini na kutupwa gerezani. Dk. Kiiza Besigye wa Uganda, amekuwa mwiba kwa utawala Rais Yoweri Museveni kama Morgan Tsvangirai alivyokuwa anamchachafya Mzee Robert Mugabe wa Zimbabwe. Neil Kinock wa Uingereza, aliutafuta uwaziri mkuu kuanzia 1982 -1992 kama Kiongozi wa Labour Party.

Raila Odinga amekuwa mgombea urais Kenya kwa vyama tofauti 2007 Orange Democratic Movement (ODM), akishirikia na na Mwai Kibaki (NARC) kumwangusha Uhuru Kenyatta, baadaye alijipanga kugombea kupitia National Rainbow Coalition (CORD), katika uchaguzi uliopita alisimama kwa tiketi ya NASA-Natuinal Super Alliance na kama Maalim Seif anayo nafasi ya kuingia Ikulu ikiwa wapigakura wataendelea kumkubali na kama uwanja wa mchezo utakuwa umesawazishwa.

Lakini kimtazamo, Maalim Seif ameonesha kuwa yeye ni nguli wa siasa Tanzania Amewashangaza waliokuwa wanapanga anguko lake. Prof. Ibrahim Lipumba na wapambe wake, wakipanga mkakati wa kumwengua kutoka CUF, yeye kwa usiri mkubwa, alishapanga mkakati wa ‘kushusha tanga’ na ‘kutweka tanga’—alishasoma uelekeo wa upepo na amekataa kuzamishwa na jahazi lililotobolewa.

Ni rai yangu kwamba Maalim Seif aachwe—afanye siasa kwa uhuru. Haitakuwa vizuri kumfikisha kwenye ukuta. Polisi someni midomo ya Mkuu wa Nchi—siku za hivi karibuni amekuwa akisisitiza neno HAKI. Mwacheni Mwalimu wa Siasa, Seif Sharif Hamad afanye siasa za kiungwaana. Sio salama kumpiga paka huku umefunga mlango.