Home Makala MAALIM SEIF, PROF. LIPUMBA WANA NAFASI YA KUJIJENGA CUF

MAALIM SEIF, PROF. LIPUMBA WANA NAFASI YA KUJIJENGA CUF

1190
0
SHARE

NA NASHON KENNEDY


KWANZA nichukue fursa hii kuwashukuru sana wasomaji wengi waliosoma na kunitumia ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yangu, wakilishukuru gazeti la RAI kwa kuchapisha makala wiki iliyopita ikiwa na kichwa cha habari, “Mgogoro wa CUF, Mutungi asitolewe kafara”.

Niliandika makala ile lengo likiwa ni kutanguliza kwanza uzalendo wetu, maana siku machafuko ya kisiasa yakitokea hakuna watakaopona.

Wawe viongozi wa vyama vya siasa, wanasheria, wabunge, viongozi wote wa serikali, wanaharakati, waandishi wa habari na wananchi wa kawaida wote wataingia kwenye tanuru hilo la machafuko!

Mgogoro wa CUF utamalizwa na uongozi wa CUF na wanachama wake wenyewe. Wakiridhiana kwa kutumia uvumilivu wa kisiasa, mshikamano na upendo hakika mgogoro huo utakwisha.

Nawaomba wana CUF na viongozi wao kila mmoja avae uhusika wa kutatua na kutanzua mtanziko wa kiuongozi na kimadaraka ndani ya CUF.

Kwa desturi, wapo baadhi ya watu katika nchi hii, kwa  hulka zao si rahisi kuwatoa kwenye mambo ambayo wamekuwa wakiyaamini kwa muda mrefu.

Lakini kwa hili la mgogoro wa CUF watu waondokane na unazi wa kubomoa na wajikite katika ujenzi wa kudumu. Naomba wana CUF wakaribishe suluhu kwa kukaa kwenye mazungumzo na kuziondosha tofauti zao kwa njia ya mwafaka.

Na katika hili, pande mbili ziketi zikiwa na rejea ya kilichotokea katika mwafaka wa Zanzibar wa mwaka 2001, ili kisijirejee tena.

Itakumbukwa katika kipindi hicho, Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamada walijifungia ndani kutafuta mwafaka japokuwa ulileta manung’uniko kwa baadhi ya wanachama wa CUF na CCM, lakini angalau uliweza kuifanya Zanzibar na wananchi wake kuishi katika amani na kuaminiana, kuuza na kununuliana, kuoza na kuoleana na kufanya mwingiliano uwe murua kwa ustawi wa watu wa Zanzibar.

 

MAALIM SEIF vs PROF. LIPUMBA

Ukiangalia historia za maisha yao ni watu waliovuna heshima, sifa kedekede mbele ya jamii. Ni wabobezi wa shughuli za kisiasa na ni watu ambao wana weledi wa kitaaluma usiotiliwa shaka na wameshiriki kwenye mambo mengi ya msingi ndani na nje ya nchi.

 

PROF LIPUMBA

Huyu ni msomi mbobezi katika uchumi. Alizaliwa Juni 6, 1952 katika Kijiji cha Ilolanguru, Wilaya ya Tabora, mkoani Tabora. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya MSingi ya Swedish Free Mission, Sikonge kati ya mwaka 1962- 1966.

Alijiunga na masomo ya sekondari mwaka 1967 -1970 katika Shule ya Sekondari ya Tabora (Wavulana) 1967-1970 na baadaye alijiunga kidato cha V na VI katika Shule ya Sekondari Pugu 1971 hadi 1972.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia 1973- 1977 akihitimu Shahada ya kwanza katika  uchumi mwaka 1976 na shahda ya umahiri mwaka 1978.

Alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi vinara waliofaulu vyema katika ngazi zote hizo na kuajiriwa kama mhadhiri msaidizi katika idara ya uchumi.

Ana shahada ya uzamivu (Ph.D) kutoka katika Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani ambacho ni miongoni mwa vyuo vikuu bora 10 duniani.

Ana familia ya mke mmoja na watoto wawili, kikazi ni mwanataaluma aliyebobea katika uchumi, akijikita katika biashara ya kimataifa na fedha, maendeleo ya uchumi na uchumi wa kilimo.

 

SHUGHULI ZA KIMATAIFA

Kama walivyo wasomi wengine duniani, Prof Lipumba licha ya kuwa Mhadhiri wa vyuo vikuu ndani na nje ya nchi kwa nyakati tofauti na kupata heshima/tuzo (awards) za kitaaluma, amewahi kushiriki katika kufanya tafiti mbalimbali za kitaaluma ndani na nje ya nchi.

Baadhi ya tafiti hizo ni Utafiti kuhusu kushiriki kwa nchi za Kusini katika mfumo wa biashara wa kimataifa, yaani “ Uruguay Roundtable Multilateral Trade negotiations kuanzia mwaka 1986 hadi 1990.

Utafiti mwingine ni kuhusu Sera za Kilimo za zinazoendelea na alibahatika kuwasilisha maelezo kuhusu matatizo ya madeni ya Afrika kwenye Kamati ya Bunge la Marekani yaani “House Sub committee on International Development, Finance, Trade and Monetary Policy mwezi Februari 1994, kwa kifupi amefanya tafiti nyingi na kuandika maandiko mengi ya kitaaluma ndani na nje ya nchi.

Aliwahi kuwa Mshauri wa Uchumi wa Serikali ya Uganda na amewahi kuteuliwa kuwa Mjumbe wa kamati ya Umoja wa Mataifa ya sera ya maendeleo na amewahi kutayarisha vigezo vya kuanisha nchi maskini sana duniani yaani “ The list of least developed countries ( 1997 na 2000).

Kati ya mwaka 1991 na 1993 alikuwa mshauri wa Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi katika mambo ya uchumi na alipata kuwa  mshauri mwelekezi katika mashirika na taasisi kadhaa zikiwemo Benki ya Dunia, SIDA, UNDP, Global Coalition for Africa, COMESA, NORAD, DANIDA, Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland na Benki Kuu ya Tanzania.

Aliwahi pia kutayarisha na kuratibu utafiti na kupendekeza sera za viwango vya kubadilishana sarafu (exchange rate policy) na sera za kulegeza masharti ya mfumo wa fedha nchini Uganda mwaka 1997.

Kisiasa, amewahi kuwa kada wa TANU na baadaye CCM tangu akisoma na kufanya kazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na amekuwa mgombea nafasi ya urais kupitia CUF mara tano akiwa Mwenyekiti wa CUF.

 

MAALIM SEIF

Alizaliwa Oktoba 22, 1943 huko Nyali, Mtambwe katika Wilaya ya Wete Pemba. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Uondwe iliyoko Pemba na kisha alijiunga na Shule ya Wavulana ya Wete kati ya mwaka 1950 na 1957.

Alijiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Mfalme George 1958- 1961 iliyoko katika Kisiwa cha Unguja na kuendelea kidato V na VI katika shule hiyo ( 1962-1963).

Licha ya kufaulu masomo ya kidato cha sita hakujiunga moja kwa moja na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, aliajiriwa serikalini akifundisha katika shule ya sekondari ya Fiedel Castro iliyoko Pemba na Chuo cha Ualimu Lumumba kilichoko Lumumba kwa kipindi cha miaka tisa.

Mwaka 1972 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kusomea shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa, Usimamizi wa Umma na Uhusiano wa Kimataifa na kuhitimu mwaka 1975.

Mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu wa Zanzibar na kuitumikia nafasi hiyo hadi mwaka 1980
Maalim Seif alianza kujifunza na hata kuingia katika masuala ya uongozi mkubwa wa serikali mwaka 1975, alipoteuliwa kuwa Msaidizi Binafsi wa Rais wa Zanzibar wakati huo (Aboud Jumbe) ambapo aliifanya kazi hiyo hadi mwaka 1977.

Mwaka 1977 akateuliwa kuwa Waziri wa Elimu wa Zanzibar na akatumika katika nafasi hiyo hadi mwaka 1980. Kwa kifupi amepitia nyadhifa nyingi za kisiasa na serikali ikiwemo Waziri wa Kiongozi wa Zanzibar na baadaye  Makamu wa Rais wa Zanzibar baada ya kuundwa kwa  Serikali ya Umoja wa kitaifa akitokea CUF kama Katibu Mkuu wa CUF.

Aliwahi kuwania urais wa Zanzibar kupitia CUF karibu mara tano ambako hata hivyo hakufanikiwa kuipata nafasi hiyo ya juu uongozi wa Zanzibar, ingawa mara kadhaa amekuwa akilalamika mbele ya Jumuiya ya Kimataifa kutotendewa haki kwenye chaguzi hizo.

 

KWANINI HAWATAKI SULUHU?

Maalim Seif anadai hawezi kukaa pamoja na Prof Lipumba kwa sababu eti Prof Lipumba alishafukuzwa uongozi na kufutwa uanachama wa CUF na hivyo yeye ( Maalim) anadai hawezi kukaa kuzungumzia masuala ya chama na mtu asiyekuwa mwanachama wa CUF.

Kwa upande mwingine Prof Lipumba amesikika mara nyingi akimtaka Maalim kwenda makao makuu ya CUF ili wafanye kazi za chama, lakini pia amesikika mara kadhaa akitaka mgogoro wa CUF umalizwe kwa mazungumzo na sio visingizio vinavyotokana na mtafaruku ambapo kila aliyeonekana kumuunga mkono Prof Lipumba au kupinga taratibu zinazotumiwa na Maalim Seif na wenzake dhidi ya kundi linalomuunga mkono Prof Lipumba na wenzake ndani ya CUF, kujengewa uhalali haramu wa kufukuzwa.

Katika hili, Prof Lipumba anaonekana ni mtu aliye tayari kwa mazungumzo, akitanguliza rai ya mwafaka badala ya vurugu na mitafaruku. Aidha katika kile kinachoonekana kuchoshwa na mbinu chafu za kufukuza wanachama na viongozi, walioonekana au wanaonekana kumuunga mkono Lipumba kufukuzwa na kundi la Maalim Seif.

Kundi la Prof Lipumba nalo limeonekana kujibu mapigo japokuwa siyo mara nyingi ya kuwafukuza uongozi na si uanachama, baadhi ya wale walioko upande wa Maalim Seif, katika hili lakini, kundi la Prof Lipumba limekuja na hoja za kikanuni za kukosekana uwajibikaji wa baadhi ya viongozi upande wa Maalim Seif ambao kimsingi wametuhumiwa kushindwa kufika ofisini kufanya kazi za chama.

Katika kujibu tuhuma hizi, upande wa Maalim Seif umekuwa ukidai kwamba viongozi wale walikuwa wakifanyia kazi Zanzibar na kwa msingi huo sio watoro kama inavyodaiwa na upande wa Prof Lipumba.

Upande wa Lipumba nao umekuwa ukidai kuwa Zanzibar ni Afisi Kuu ya chama na sio makao makuu ya chama, kwani makao makuu ya chama yaliyoko Buguruni jijini Dar es Salaam ndiko kimsingi kunakofanyika shughuli zote za chama kwa nchi nzima kwa mujibu wa Katiba ya CUF.

Huu ni mvutano usio na faida kwa CUF wala wanachama wa CUF, wapenda demokrasia nchini Tanzania, kizazi cha vijana kinachochipukia katika siasa wala waanzilishi wa mageuzi nchini na wala hauna afya kwa maendeleo ya kiuchumi, mtengamano na mshikamano, utulivu na amani ya taifa letu.

Lazima viongozi hawa watambue wazi na fika kwamba CUF inapewa ruzuku na serikali inayotokana na walipa kodi wa Tanzania wasiotokana na CUF yenyewe si kwa jambo jingine lolote kwa ajili ya maendeleo ya kuimarisha demokrasia ndani ya nchi yetu.

Hivyo vurugu wanazozifanya akina Maalim Seif na Prof Lipumba  zisizokuwa na mwisho, zinaghaini (hinder)  nia njema ya Watanzania wanaochangia kulipa kodi inayotolewa kama ruzuku kwa maendeleo ya vyama vya siasa na katika mlango waliouchagua wao wenyewe.

Kwa msingi huo, vurugu hizo zinadhihirisha   wizi wa fadhila za walipa kodi na nia njema waliyo nayo katika kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika kutoa mawazo yake kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Shime kwakuwa katika vita hii hakuna mshindi wa jumla, wala mshinde wakati umefika sasa kwa mapatano yasiyo na hiari kwa pande zote mbili kudhihirisha uhodari katika diplomasia na kutafuta mwafaka utakaoirejesha CUF njiani na kuipa nguvu kama ilivyokuwa au zaidi ya hapo.

Maalim Seif na Prof. Lipumba pigeni mbio kuiwania fursa hii kabla haijawaponyoka, maana haiwezekani muda wote duniani ukawa mali yenu binafsi nyie watu wawili kwa kuteka hisia za wana CUF na jamii nzima ya Watanzania katika mgogoro usio na mwisho.

Tafuteni suluhu ya mgogoro kabla ya dunia ya wapenda amani haijawachoka kwa maslahi mapana ya maendeleo ya taifa letu! Mungu ibariki Tanzania!

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa Simu Na. 0756 823 420/ 0784 822 407 au email nashon_kennedy@yahoo.com au nashonkennedy@ gmail.com