Home Makala Kimataifa MAANDAMANO MAKUBWA DHIDI YA UFISADI YAIKUMBA RUSSIA

MAANDAMANO MAKUBWA DHIDI YA UFISADI YAIKUMBA RUSSIA

1263
0
SHARE
Maandamano ya wapinzani ya kupinga ufisadi mjini Moscow.

MOSCOW, RUSSIA


Kwa mara ya kwanza Vladimir Putin alishinda urais nchini Russia tarehe 26 Machi 2000. Na wiki iliyopita, miaka 17 kamili baadaye maelfu ya waamdamanaji nchini mwake walijitokeza kulaani ufisadi, suala ambalo limekuwa likijitambulisha sana ndani ya utawala wake.

Maandamano haya yanayotajwa kuwa changamoto kubwa zaidi katika utawala wake tangu mwaka 2012 yalianzia katika maeneo ya pwani ya Bahari ya Pacific mashariki mwa nchi hiyo ambako maelfu waliandama katika barabara za mji-bandari wa Vladivostok.

Na baadaye siku hiyo hiyo maandamano na mikutano, ambayo mingi yao haikuwa imeruhusiwa na mamlaka husika, iliripotiwa kutoka miji mbali mbali nchini humo – kama vile Novosibirsk na Yekaterinburg,pia miji ya viwanda ya Chelyabinsk na Nizhny Tagil.

Hali kadhalika maandamano yalifanyika hata katika mji wa Makhachkala, mji mkuu wa jimbo la Dagestan, kaskazini mwa maeneo ya Caucasian ambako Putin huwa anapata zaidi ya asilimia 90 ya kura.

Hata hivyo makundi makubwa ya watu yalionekana katika Mji mkuu wa nchi hiyo – Moscow na St Petersburg (zamani Leningrad) ambako walikusanyika katika Palace-Square – ikikumbushia mapinduzi ya Kibolshevik ya mwaka 1917, hali ambayo ni vigumu kupuuzwa na watawala wa kremlin.

Maandamano yote hayo yalikuja baada ya wito wa kiongozi wa upinzani Aleksei Navalny, ambaye amejitokeza kuwa mpambanaji mkuu wa ufisadi nchini humo.

Hivi karibuni Navalny alitoa video iliyodai kwamba Waziri Mkuu wa nchi hiyo Dmitry Medvedev, alianzisha taasisi za misaada na makampuni hewa ili kujipatia fedha za kununulia majumba ya kifahari, meli za amasa na vitu vingine vya thamani.

Video hiyo imeangaliwa mara 12 milioni nchini humo kupitia mitandao ya jamii na hivyo Navalny akawataka wafuasi wake waingie mitaani kudai majibu kutoka serikalini ya masuala hayo ya ufisadi. Waandamanji walikuwa wakiimba “Russia bila Putin” na “Russia itakuwa huru.”

Hata hivyo walipambana na vikosi vya kutuliza ghasia na magari ya maji ya washa washa. Mashirika ya haki za binadamu walidai zaidi ya watu 700 walikamatwa mjini Moscow peke yake akiwemo Navalny mwenyewe. Siku ya pili yake mahakama moja ya Moscow ilimhukumu kiongozi huyo mwa upinzani kwenda jela kwa siku 15 kwa hatia ya kuhamasisha maandamano yasiyoruhusiwa.

Wachunguzi wa mambo wanasema kwa kiongozi huyo wa upinzani kumchagua Medvedev (Waziri Mkuu) kama lengo la mashambulizi yake ilikuwa ni mpango wa kimkakati. Hii inatokana na ukweli kwamba Putin ni kiongozi ambaye bado anapendwa na wengi nchini humo na hivyo hata Warussia ambao hawamuafiki wangesita kushiriki katika maandamano dhidi yake.

Katika miaka mitatu iliyopita, wakati bei ya mafuta yasiyosafishwa ikianguka katika soko la dunia, vikwazo kutoka nchi za magharibi dhidi ya Russia vilisababisha kuzorota kwa uchumi hali ambayo imekuwa inawaumiza sana walaji wa kawaida.Kwa upande wake, waziri Mkuu Medvedev ni kiongozi anayechukiwa na wengi na kuna baadhi wanamuona kuwa ndiye anahusika kwa kuzorota kwa uchumi wa nchi hiyo.

Hata hivyo maandamano hayakuwa dhidi ya Medvedev tu, kwa ujumla yalikuwa yanabeba kauli nzito ya kutoridhishwa na mfumo mzima wa utawala.

Kwani ukubwa wa maandamano na maeneo mengi yalikotokea iliwashangaza wachunguzi wengi wa mambo, ingawa wanadai hali ya kutokea upinzani mkubwa dhidi ya utawala wa Putin hawezekani.

Hii ni kwa sababu utafiti uliofanywa na taasisi huru ya Levada (Levada Centre) unaonesha asilimia 83 ya Warussia hawatashirii katika maandamano ya kisiasa ingawa asilimia 50 tu ya wanaamini nchi inaelekea njia sahihi.