Home Makala MAAZIMIO YAKITEKELEZWA KATIBA MPYA ITAPATIKANA

MAAZIMIO YAKITEKELEZWA KATIBA MPYA ITAPATIKANA

748
0
SHARE
Deus Kibamba akionesha kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba

Na MAULI MUYENJWA


Machi 2 na 3 mwaka huu, Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) liliratibu Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Katiba ambao ulishirikisha wajumbe 150 wakiwakilisha vyama vya siasa, wabunge, taasisi za elimu ya juu, mashirika ya kimataifa, wahadhiri, asasi za kiraia na kidini na makundi mengine.

Katika mkutano huo, kulikuwa na vuta nikuvute juu ya hoja mbalimbali zilizowasilishwa na watoa mada. Mmoja wapo akiwa Othman Masoud Othman aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Othman alitoa mada iliyohusu matakwa na masilahi ya Zanzibar katika mchakato na maudhui ya Katiba mpya.

Hata hivyo, baada ya wadau mbalimbali kuwakilisha hoja zao kuhusiana na mkwamo wa mchakato wa Katiba, kikao hicho kilitoa maazimio ya pamoja na kama yakifanyika, basi kuna uwezekano mchakato wa Katiba Mpya ukarudi upya.

Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba, alieleza kuwa mkutano huo uliona kuwa Rais Dk. John Magufuli pekee kwa nafasi aliyonayo, ndio mwenye uwezo wa kuamua hatima ya kuokoa au kuangamiza mchakato huo.

“Kama rais akiamua na kutokana na ahadi alizoahidi wakati wa kuomba kura na alirudia wakati alipozindua Bunge jipya na sasa akiwa Mwenyekiti wa CCM, atatekeleza ilani ya chama chake kama ambavyo imeahidi kupatikana kwa katiba mpya,” anasema.

Azimio jingine rais alitangazie Taifa juu ya tarehe rasmi ambapo mchakato wa Katiba Mpya utarejeshwa rasmi ikiwemo kuagiza kuchapishwa kwa tangazo lake katika gazeti maalumu la Serikali.

Kibamba anasema Mkutano Mkuu uliofanyika Machi 23 mwaka huu, uwe ni wa kwanza tu katika mfululizo wa mikutano kama huo itakayoendelea kufanyika hadi pale hatima ya mchakato huo itakapojulikana.

“Wajumbe walikubaliana kama mkutano huo ni mwanzo tu, sasa kutakuwa na mikutano kama hiyo ambayo italeta mwamko wa kujua ni namna gani ya kudai Katiba Mpya na itakuwa ni mwendelezo isiyokuwa na kikomo mpaka kieleweke kama wasemavyo kwa lugha ya mtaani,” anasema.

Lakini pia mkutano huo uliamua kuishauri Serikali kutenga bajeti ya mwaka 2017/2018 katika fungu la Wizara ya Katiba na Sheria, ili kuwezesha shughuli za awali katika kurejesha mchakato wa Katiba Mpya kuweza kuanza.

“Serikali itenge fedha hizo hata kama ni kidogo lakini angalau iwezeshe hata urekebishwaji wa sheria mbili na zipelekwe katika Bunge na kuweza kusaidia hatua za awali zianze mapema,” alisema.

Katika mkutano huo, Kibamba anasema Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, aandae na kupeleka miswada ya marekebisho katika sheria mbili zinazoongoza mchakato wa Katiba mpya.

“Yaani Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na.8 ya mwaka 2011(pamoja na marekebisho yake) na sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 (kama ilivyorekebishwa), hili lifanyike mapema  kwenye mkutano wa saba wa Bunge unaoanza April 4, mwaka huu kama sehemu ya mchango wake (Waziri) katika kunasua mchakato wa Katiba mpya nchini.

Kibamba anaeleza kuwa ili kuweza kufika katika safari hiyo, wadau wanapendekeza kuwepo jopo maalumu linaloshirikisha wataalamu na wawakilishi wa makundi mbalimbali yanayofanyia kazi masuala ya Katiba na demokrasia likutane na rais ili kushauriana juu ya hatima ya mchakato huo na hatua bora ya kuanza awamu ya pili na Jukata iratibu maandalizi ya mkutano huo na rais.

“Vyombo vya habari viwezeshwe kuendelea kutoa elimu juu ya historia, mchakato na maudhui ya Katiba mpya kama sehemu ya kurejesha hamasa iliyojengeka awamu ya kwanza ya mchakato huo na umuhimu wake katika awamu ya pili,” alisema Kibamba.

Kibamba anaeleza kuwa kwenye mkutano huo, ziliwasilishwa mada mbalimbali kuhusu historia ya Katiba na uandishi wake Tanzania, matakwa na masilahi ya Zanzibar katika mchakato na maudhui ya Katiba mpya, mikwamo katika mchakato wa Katiba hiyo na namna bora ya kuutatua, mchango wa vyombo vya habari na mada nyingine zinazohusiana na mchakato huo.

Ni kweli kama ilivyo kiu ya Watanzania na utata uliopo, ni kweli kama Jukata itafanikiwa kutekeleza hayo, kuna uwezekano wa kupata Katiba mpya, lakini zaidi ni kwa nafasi aliyonayo rais ndio pekee wa kuokoa mchakato huo na Serikali kuwa tayari.