Home Habari Mabadiliko baraza la mawaziri kujumuisha upinzani yanukia Kenya 

Mabadiliko baraza la mawaziri kujumuisha upinzani yanukia Kenya 

933
0
SHARE

NA ISIJI DOMINIC 

MAAMUZI ya hivi karibuni yaliyofanywa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ndani ya chama chake cha Jubilee yametafsiriwa kama ishara ya kunukia mabadiliko yanayotajwa makubwa katika baraza la mawaziri. 

Rais Uhuru amekuwa akijiweka kando na siasa akisisitiza wanasiasa, mawaziri na maofisa wa serikali kujikita zaidi kutekeleza mahitaji ya wananchi hadi hapo muda wa kampeni utakapofika ikiwa ni kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2022. 

Mara kadhaa, Rais Uhuru ameonekana kuwa mkali na wakati mwingine kutumia lugha ya nyumbani ‘Kikikuyu’ hususan kwa wanasiasa wanaotoka eneo lake la Mlima Kenya ambao wamekuwa wakijihusisha kupiga siasa na kumshambulia kwa kupeleka maendeleo katika maeneo mengine nchini Kenya. 

Muda huu ambao Kenya ipo kwenye mapambano kudhibiti kuenea maambukizi ya virusi vya Corona, Rais Uhuru amekunjua makucha yake ndani ya chama tawala kwa kuitisha kikao cha wabunge wa Seneti wa chama cha Jubilee kilichofanyika Ikulu jijini Nairobi. 

Kikao hicho kiliazimia kufanya mabadiliko ya viongozi wa juu wa chama hicho kwenye Bunge la Seneti na hivyo kumuondoa Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen, katika nafasi yake ya Kiongozi wa Waliowengi ambayo sasa ipo chini ya Seneta wa Pokot Magharibi, Samuel Poghisio.

Kama hiyo haitoshi, kikao hicho kiliazimia kumuondoa Seneta wa Nakuru, Susan Kihika, kama Kiranja wa Waliowengi katika Bunge la Seneti na nafasi yake kuchukuliwa na Seneta wa Muranga, Irungu Kang’ata. 

Eneo lingine ambalo Rais anakusudia kufanya mabadiliko ni Bunge la Taifa na macho yote sasa yanaelekezwa kwa Mbunge wa Garissa ambaye pia ni Kiongozi wa Waliowengi katika bunge hilo, Aden Duale. 

Lakini kwasasa, Wakenya wapo kwenye mkao wa kusubiria mabadiliko yanayonukia katika baraza la mawaziri. Kabla ya janga la Covid-19 kuitikisa Kenya na dunia kwa ujumla, taarifa zilizokuwa zinazagaa mitandaoni ni nia ya Rais Uhuru kufanya mabadiliko yanayotajwa kama makubwa katika baraza la mawaziri.

Rais Uhuru anakusudia kufanya mabadiliko hayo katika serikali yake ili kuifanya iwe na mshikamano zaidi kufuatia kuongezeka kwa uhusiano baridi na Naibu Rais William Ruto pamoja na washirika wake.

Tetesi zinadai viongozi wa upinzani Raila Odinga (ODM), Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Gideon Moi (Kanu) wametafutwa katika nyakati tofauti kupendekeza majina yatakayojumuishwa katika mabadiliko ya baraza la mawaziri.

Msukumo wa ulazima wa kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri inatajwa imetokana na ushirikiano wa Rais na viongozi wa upinzani katika kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona na pia tofauti iliyopo kati ya Uhuru na Ruto.

Aidha duru za siasa zinadai mazungumzo na viongozi hao wanne wa vyama tofauti inalenga kuthibiti ongezeko la upinzani serikalini inayofanywa na kundi linalomuunga mkono Naibu Rais Ruto.

Tayari kuna uvumi Raila, Kalonzo, Mudavadi na Moi wameshapendekeza majina ya watakaoteuliwa mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wa mashirika ya umma lakini kutokana na idadi ndogo ya nafasi za mawaziri, ni dhahiri kuna watu watafutwa hususan wale wanaooenaka waasi ili kutengeneza nafasi kwa watu wengine kuteuliwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kanu, Nick Salat, alisema wapo wanachama wake wanaoshika nyadhifa za kamati muhimu ndani ya Bunge la Taifa, Bunge la Seneti na mashirika ya umma na anamatumaini hivi karibuni chama chake kitapata nafasi kwenye baraza la mawaziri.

Naye Mbunge wa Tiaty, William Kamket, alinukuliwa akisema mabadiliko hayo hayaepukiki na yatakuja kwa ‘kwa njia yoyote na muda wowote’ huku akisisitiza Ruto ameshindwa jukumu lake la kumsaidia Rais.

 “Kati ya William Ruto na Raila Odinga, nani anamuunga mkono Rais Kenyatta? Kati ya Gideon Moi na William Ruto, nani anaunga mkono ajenda za Rais? Jibu liko wazi, hawa viongozi wawili (Uhuru na Ruto) hawajakusudiwa tu kuwa washirika wa kwaya katika hii serikali wakati watu wengine wanashambulia serikali vikali,” alisema Mbunge huyo wa Tiaty na kuongezea maoni yake kwa kile kilichowatokea Murkomen na Susan.

 “Rais amekuwa kimya wakati wanapiga kelele, wanamshambulia na sasa ni wakati wa kukunjua makucha. Amewasubiri kudhihirisho vitisho vyao na kuondoka kwenye chama lakini wamekuwa wakisuasua. Sasa ni muda wa kuwaondoa na itafanyika hivi karibuni.” 

Kauli ya Kamket iliungwa mkono na Mbunge wa Cherangany ambaye ni mshirika wa Uhuru, Joshua Kuttuny, aliyesema uongozi wa Jubilee bungeni ulihitajika kumuunga mkono Rais. 

Mbunge wa Kiharu ambaye ni mfuasi wa Naibu Rais Ruto, Ndindi Nyoro, alisema ni haki na mamlaka ya rais kuteua baraza la mawaziri lakini akamtahadharisha hatua hiyo iwe na nia ya kutoa huduma.

 “Kama itafanywa kwa mrego wa kisiasa, ni bahati mbaya haitafaulu. Wakenya wanavutiwa zaidi na hali ya mifuko yao na uchumi, sio nani anachukua nafasi gani,” alisema Nyoro.

Mapema mwaka huu, Rais Uhuru alifanya mabadiliko katika baraza la mawaziri kwa kumuondoa Mwangi Kiunjuri aliyekuwa Waziri na Kilimo na nafasi yake kuchukuliwa na Peter Munya huku Ukur Yattani akichukua nafasi ya Henry Rotich katika Wizara ya Fedha.

Japo Rais Uhuru hakusema sababu zilizompelekea kumuondoa Kiunjuri, lakini ni dhahiri siasa ndizo zilizomponza ukizingatia waziri huyo wa zamani alikuwa anaonekana wazi kumpigia debe Ruto kuelekea uchaguzi mkuu 2022, na mara kadhaa alionywa kuweka siasa pembeni.         

Kuondolewa kwa Rotich kunahusishwa na kesi ya ufisadi inayomkabili mahakamani ambapo yeye pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Kamau Thugge, wanatuhumiwa kwa matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa mawili.

Maofisa hao wawili serikalini ni miongoni mwa watuhumiwa 10 zaidi ambao Julai 23 mwaka jana walituhumiwa kwa mashitaka kibao ikiwemo matumizi mabaya ya fedha, kula njama ya kufanya uhalifu wa kiuchumi na kuidhinisha malipo kinyume na sheria.

Hata hivyo habari iliyotikisa vichwa vya habari na kuwa gumzo maeneo mbalimbali nchini Kenya ni kuondolewa kwa Kiunjuri.

Waziri huyo wa zamani ambaye pia ni mwanasiasa alisema Rais Uhuru alimtimua katika baraza lake la mawaziri kutokana na yeye (Kiunjuri) kuongea masuala yanyogusa eneo la Mlima Kenya na kuongeza kiongozi huyo wa nchi alikuwa anachagua mapambano yake vita dhidi ya ufisadi.

“Tusiache BBI (Building Bridges Initiative) itumike kama kivuli cha maendeleo ya eneo letu… kama Kiunjuri nitaendelea kusema hivyo… nitawapigania watu wangu,” alisema.

Kwa mujibu wa Kiunjuri, Rais Uhuru sasa ameamua kuwashughulikia wakosoaji wake – hususan kutoka eneo la Mlima Kenya – kwa kutumia Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mamlaka ya Ushuru Kenya (KRA) kama silaha.

“Nani alimtukana Uhuru zaidi ya (Gladys) Wanga au (Hassan) Joho au Babu Owino? walisamehewa …lakini kila mara Kiunjuri au Moses Kuria anasema ‘barabara ya Laikipia ni mbaya’, kesho yake uko DCI ama KRA ama EACC (Tume ya Maadili na Kupambana na Rushwa),” aliongeza Kiunjuri.

Kutumbuliwa kwa Kiunjuri na mabadiliko ambayo Rais Uhuru anayafanya kwa wabunge wa Jubilee wanaoshika nafasi nyeti bungeni ambao wanaonekana kupigia debe Naibu Rais Ruto kuelekea uchaguzi mkuu 2022, ni dalili za kuthibitisha yeye (Uhuru) ndiye kiongozi wa taifa na chama.