Home Latest News Mabadiliko makubwa ya soka Tanzania yaja

Mabadiliko makubwa ya soka Tanzania yaja

956
0
SHARE

NA ASHA MUHAJI,

HUENDA ikawa ni sehemu ya kufanya mabadiliko makubwa ya soka la Tanzania. Bila shaka mwanzo mzuri ulioanzishwa na klabu ya Simba kutaka kubadili mfumo wake wa uendeshaji ukawafungua macho timu na klabu zingine.

Simba kwa kauli moja walipitisha mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji kutoka ule wa wanachama kulipia kadi zao na kwenda katika mfumo wa kumiliki hisa ambapo sasa utafungua milango kwa wawekezaji kuwekeza fedha ndani ya klabu hiyo.

Mohammed Dewji, mfanyabiashara tajiri na kijana aliyechochea mabadiliko hayo tayari ameweka mezani dau la shilingi Bilioni 20 kununua hisa 51 za klabu hiyo.

Kwa mujibu wa mwekezaji huyo, kiasi hicho cha fedha kitatumika kununua hisa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), ambapo kulingana na thamani ya fedha hizo, watapewa asilimia chache zisizopungua shilingi bilioni tano ambazo ndizo zitakazoweza kuendesha klabu huku mtaji ukiwa bado umelindwa BOT.

Kwa mujibu wa MO, matumizi ya klabu hiyo kwa sasa ni shilingi Bilioni 1.2 hivyo wakifanikiwa kuwa na shilingi bilioni 4-5 kwa mwaka wataweza kuendesha klabu hivyo katika dhana ya ushindani si tu hapa nchini bali barani Afrika kwa ujumla.

Katika uwekezaji huo, MO amelenga ndani ya miaka mitatu tu kutoka sasa timu hiyo ifike fainali ya Klabu Bingwa Afrika kama siyo kutwaa taji hilo kubwa kuliko yote barani humo.

Kwa malengo ya mwekezaji huyo ni wazi Simba itakuwa timu yakwanza kuongoza kwa mafao mazuri kwa wafanyakazi wake, hali ambayo itatoa mwanya wa kutoa ushindani wa kweli barani Afrika kwa kushindana na TP Mazembe ya DRC, Al Ahly ya Misri au Etoile du Sahel ya Tunisia na nyinginezo.

Siku chache baada ya wanachama kubariki mabadiliko ndani ya klabu hiyo, Mo ameshachangia kiasi cha shilingi milioni 100 kusaidia usajili unaotarajiwa kufungwa mwishoni mwa wiki hii ikiwa ni nje ya ile ahadi yake iwapo atafanikiwa kununua hisa.

Mwamko wa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kutaka kwenda katika mfumo wa mabadiliko. Tayari uongozi umeunda kamati ya watu sita ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zito Kabwe kutoa mapendekezo juu ya mfumo gani hasa wa hisa unaoweza kuendana na mazingira ya sasa ya klabu yao.

Hata hivyo tayari wanachama wa Simba wamneshaanza kutoa maoni yao kuhusiana na mfumo huo mpya utakaoingia klabu hiyo. Zito akiwa nje ya kamati hiyo ameshatoa maoni yake na kushauri MO apewe asilimi 40, wanachama nao asilimia 40 na asilimia 20 zinazobaki wapewe wawekezaji wengine watakaojitokeza.

Lengo lake kupunguza asilimia kutoka 51 alizoomba mwekezaji huyo ili kufanya asiwe na maamuzi ya peke yake inapotokea kufanya hivyo na badala yake lazima awashirikishe wanachama.

Kufanikiwa kwa klabu hito kutafungua ukurasa mpya katika soka la Tanzania hasa kutoka klabu hizo kongwe kuinua matumaini mapya ya mchezo huo nchini.

Takribani miaka 80 sasa klabu hiyo ikiwemo pacha wake zimeshindwa kufikia maendelo yanayolingana na umri huo ikiwa chini ya mfumo huo. Ni wazi mabadiliko ya kimfumo ndiyo yatakayoikombo klabu hiyo.

Wachambuzi wa soka nchini wanaona kuna kila dalili ya  mabadiliko hayo kuungwa mkono na klabu zingine kufuatia baadhi ya wanachama wa klabu kongwe ya Yanga nao kuanza kuhoji masuala kadhaa yakiwemo ya udhamini pamoja na hatima yake katika siku zijazo.

Wachambuzi hao wanautazama itisho la mkutano mkuu wa dharula uliotangazwa na viongozi wa klabu hiyo hivi karibuni kuwa ni sehemu ya kujitathimini kabla ya kutafuta njia sahihi ya kuendesha klabu hiyo yenye mashabiki na wanachama wengi zaidi hapa nchini.

Licha ya kuwa agenda hazijawekwa wazi lakini inadaiwa mustakabali wa klabu hiyo utajadiliwa katika mkutano mkuu. Mpaka sasa klabu hiyo haina mdhamini rasmi aliyetangazwa hadharani zaidi ya kuendeshwa kwa msaada mkubwa kutoka kwa viongozi wake.

Mfumo wa kutegemea wadhamini pekee umepitwa na wakati hivyo kutakiwa kwanza kuingia katika mfimo wa kmapuni au hisa ambao sasa utatoa nafasi ya udhamini.

Si kazi rahisi kwa klabu hiyo kuingia katika mfumo mpya kwani wanachama wengi wa klabu hizo kongwe wana  mtazamo tofauti kuhusiana na mifumo mipya ya kisasa ya uendeshaji inayokuja hivi sasa kwani wao wanapenda zaidi ukale kuliko usasa.

Yanga iko katika mfumo wa wanachama kama ule wa Simba licha ya kuwa kiuendeshaji inaelekea kuwa katika mfumo wa kikampuni kwani hata ukiangalia uwiano wake wa mapato yatokanayo na shughuli zake kuu na matumizi yake vinatofautiana sana.

Ni fursa kwa wana Yanga nao kufanya kile kilichofanywa na Simba ili kuleta mabadiliko makubwa katika soka la Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa klabu hizo ndizo kongwe.

Hapa unaashiria mabadiliko makubwa katika historia ya soka la Tanzania ambalo kwa muda mrefu sasa limekuwa katika kiwango kisichoridhisha licha ya uwekezaji mkubwa wa fedha unaofanywa na wadau mbalimbali.

Kufanikiwa kwa Yanga kubadili mfumo wake utasafanya sasa soka la Tanzania kwa ujumla kutoka hapa lilipo na kupiga hatua kadhaa mbele kukimbilia mafanikio yaliyopo katika klabu za nchi zinazotoka magharibi au kaskazini mwa bara hili la Afrika.

Simba inaelekea sasa kuungana na Azam inayoendeshwa katika mfumo wa kampuni huku Yanga nayo ikisubiriwa kwa hamu kuingia huko.

Muungano wa wafanyabiashara watatu wakubwa tena  matajiri hapa nchini utaamsha hamasa na ushindani mkubwa ndani ya Ligi Kuu, michuano inayotoa taswira ya timu ya taifa pamoja na soka la nchi kwa ujumla.

Mpaka sasa klabu ya Stand United licha ya kukumbwa na mgogoro wa kiuongozi bado ina nafasi ya kufanya marekebisho ya kubadili mfumo kutoka wanachama kwenda kampuni. Klabu hiyo ukiongeza na zile zinazomilikiwa na taasisi kama vile Mbeya City, Mwadui, Toto African, Mbao, Majimaji, Ndanda nazo kusoma alama za nyakati ili kwenda na mfumo wa kibiashara ili kuzipatia faida pamoja na kuleta ushindani wa kweli.

Shirikisho la Soka inapaswa sasa kusimamia kikamilifu mabadiliko hayo pindi klabu zitakapotaka kubadili katiba zao na siyo kuzikwamisha kama ilivyokuwa kwa Stand United iliyoshindwa kwenda katika mfumo wa kampuni.