Home Latest News MABADILIKO YA KATIBA YA JAPAN YALILINDA JESHI

MABADILIKO YA KATIBA YA JAPAN YALILINDA JESHI

1097
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Wiki iliyopita chama cha Liberal Democrats cha Waziri Mkuu Shinzo Abe kilishinda tena uchaguzi mkuu nchini Japan ingawa wachunguzi wa mambo wanasema ushindi huo haukutarajiwa kutokana na kupungua kwa umaarufu wa mwanasiasa huyo.

Wanasema kura za maoni zimekuwa zikionyesha Abe anaungwa mkono na theluthi moja tu ya Wajapani ingawa chama chake kilishinda kwa asilimia 51 za kura.

Kutokana na kuporomoka uungwaji mkono Abe aliamua kuitisha uchaguzi ghafla kabla ya muda wake, na uamuzi huo umejibu vizuri. Hii ni tofauti na uamuzi kama huo wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May mapema mwaka huu ambapo uchaguzi aliouitisha ulimuumiza.

Hata hivyo chama cha Abe, na kile cha mshiriki wake katika Bunge kiliendelea kuwa na theluthi mbili za Wabunge, na hivyo kuwa na uwezo wa kubadili Katiba.

Japan sasa hivi inakabiliwa na changamoto mbili kubwa: wananchi wengi wana umri mkubwa; na kuwa na jirani mchokozi – Korea ya Kaskazini, nchi ambayo kila mara huvurumisha makombora upande iliko Japan na hata kutishia kufunga vifaa vya kinyuklia katika makombora hayo.

Changamoto zote mbili ni kubwa, ingawa utatuzi wa hiyo ya kwanza (kuhusu umri) itachukua muda mrefu. Kwa muda mrefu Wajapan wamekuwa wakidhibiti kuzaliana.

Lakini hili la uchokozi kutoka Korea ya Kaskazini ndiyo kipaumbele kikubwa cha Waziri Mkuu Shinzo Abe na amedhamiria kufanya marekebisho ya Katiba kwa kuondoa vipengele vinavyoikataza Japan kuwa na jeshi lake na zana za kujilinda.

Baada ya Vita ya Pili ya Dunia mataifa washindi yalilazimisha Japan kuweka katika katiba yake Kifungu cha 9 kilichosema: “Watu wa Japan daima wanapinga kutumia nguvu za kijeshi katika kutatua migogoro baina ya mataifa… na hivyo haitakuwa na majeshi ya ardhini, ya anga na ya baharini.” Hiyo ilikuwa mwaka 1945.

Lakini kwa zaidi ya miongo saba sasa Japan imekuwa ikikiuka Katiba yake hiyo kwa kudumisha vikosi vilivyokatazwa. Bajeti yake ya kijeshi ni ya nane kwa ukubwa duniani.

Askari wake zaidi ya 300,000 hamejihami vyema kwa silaha za kisasa na serikali mbali mbali zilizopita zimekuwa zikichukulia kwamba hali hii ni halali kikatiba kutokana na kile walichoita “vikosi vya kujilinda tu.”

Hata hivyo Abe yuko sahihi katika azma ya kubadilisha katiba itakayoruhusu Japan iwe na vikosi vyake vya kijeshi, au tuseme kuhalalisha tu hali iliyokuwapo kwa miongo mingi.

Wachunguzi wa mambo wanasema utawala wa sheria ni muhimu kwani si vyema kwa serikali kukiuka Katiba yake yenyewe.

Na kwa upande mwingine miongo mingi ya ukiukwaji wa kipengele cha 9 cha Katiba kulizua mjadala kuhusu mchango wa Japan katika kudumisha ulinzi na usalama wa dunia, hasa katika ukanda wa bahari ya Pacific.

Kila mara Japan inapojikuta inataka kuwasaidia washiriki wake, au kuchangia katika operesheni ya vikosi vya kulinda amani kupitia Umoja wa Mataifa, kuna baadhi ya Wajapani walikuwa wakipinga kwamba ni kukiuka Katiba ya nchi hiyo.

Mara nyingi wamekuwa sahihi, na hata kama walipuuzwa, huwa wanachelewesha tu mambo. Hadi mwaka jana vikosi vya Japan vilikuwa vinazuiwa kuwasaidia washiriki wao waliokuwa wakishambuliwa katika maeneo mbali mbali duniani.

Hata hivyo ushiriki wa Japan katika kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa umekuwa kama dhihaka vile. Kwa mfano vikosi vyake nchini Iraq vililazimika kulindwa na vikosi vya Australia kwa sababu havikuruhusiwa kujibu mapigo kila vikijikuta vikishambuliwa na wanamgambo waliokuwa wakishambulia vituo vyao.

Wadadisi wa mambo wanasema kubadilisha Kipengele cha 9 cha Katika haitakuwa kazi rahisi, na hasa pake muswada husika utakapopelekwa kwa wananchi kuukubalia au la katika kura ya maoni.