Home Makala WAUZA SIMU WAMETIKISWA

WAUZA SIMU WAMETIKISWA

1090
0
SHARE

NA HERIETH FAUSTINE


NI zaidi ya mwaka sasa tangu serikali kuweka mikakati mipya ya kudhibiti eneo la ukusanyaji ushuru wa simu.

Hii imetokana kwamba kwa sasa asilimia kubwa ya bidhaa za simu zilizokuwa zikiingizwa hapa nchini kutotozwa ushuru mkubwa, hivyo kuamua kutunga sheria ambazo zitafanya kuwepo kwa ushuru wakati wa uingizwaji.

Jambo hili limeonekana kuyaumiza zaidi makampuni ya simu, hasa yale madogo ambayo bado hayajaimarika zaidi kwenye biashara hii ya uuzaji simu.

Pia hali hiyo haijaishia kwa makampuni hayo pekee, bali pia imeenda mbali zaidi kwa kuwagusa mpaka wachuuzi wadogo wadogo wa bidhaa hizo na hivyo kujikuta wakilazimika kupandisha bei za bidhaa hiyo maradufu.

RAI limefanikiwa kuzungumza na baadhi ya makampuni hayo ambayo yanaonekana zaidi kukumbwa na rungu hilo la kodi.

Kwani wengi wao kwa sasa wanadai kuwa,  wanalazimika kupandisha bei za vifaa hivyo vya mawasiliano kutokana kwamba ushuru umepaa maradufu.

Baadhi ya kampuni hizo zimekwenda mbali zaidi kwa kuweka wazi kwamba, wanafikiria kuachana na biashara hiyo kutokana na kuwapo kwa sheria mpya zinazowakosesha uhuru wa kuendesha biashara hiyo.                                                                                                                                                                                                                                                          Raymond Kalikawe ambaye ni Ofisa Mauzo wa Kampuni ya Simu ya KZG, anasema mauzo ya simu katika kampuni hiyo yameshuka kwa kasi kufuatia  kuwapo kwa hali ngumu  pamoja na kupanda kwa bidhaa wakati  wa  kutoa nchi nyingine na kuziingiza nchini.

Anasema gharama za kuingiza mzigo  zimekuwa za juu sana tofauti na miaka yote na kama utaweza kuingiza lazima bidhaa hiyo gharama yake iwe juu zaidi.

“Kama unavyosikia kwa wananchi wanavyosema kuwa hali ni ngumu sana, hata kwa upande wetu uko hivyo hivyo. Gharama za uingizaji mzigo nchini umekuwa mkubwa sana hadi kufikia  hatua ya  kushindwa kusafirisha mzigo hadi tuangalie kiwango kama kimeshuka au laa,

“Hapo awali  gharama  zilikuwa zinategemea ukubwa wa mzigo na tulikuwa tukipewa nafasi ya jinsi ya kuangalia gharama za mzigo na  tulikuwa tunakubaliana na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), kuhusu gharama za mzigo kabla ya kuleta na ndio maana gharama ya usafiri hazikuwa juu sana.

“Sisi hatuna  tatizo ya kulipa serikalini, tatizo ni wateja kutonunua simu hizo kutokana na kupanda kwa bidhaa na ikishapanda bei, ina maana wateja hawatoweza kununua tena watakimbilia kwa zile ambazo zitakuwa na bei ndogo,”anasema Kalikawe.

Anasema kwa sasa kampuni hiyo inakabiliwa na  changamoto ya kushuka kwa wanunuaji wa bidhaa zao kufuatia kupanda maradufu kwa gharama za kusafirisha mzigo.

Anaendelea kufafanua kwa kutolea mfano kuwa kwa sasa ikiwa mzigo utauingiza sokoni kwa gharama kubwa basi lazima na wao wapandishe bei kwa wanunuaji wa jumla kwa maana ya wachuuzi.

Anasema wachuuzi hao wamekuwa wakusuasua kutokana na gharama za mzigo kupanda, huku wengine wakiendelea kushusha kiwango cha mzigo kadri siku zinavyozidi kwenda ikilinganishwa na awali.

Kwa mujibu wa Kalikawe, kama kampuni wapo katika mchakato wa kuangalia ni njia gani nzuri watumie ili kuweza kuingiza mzigo sokoni.

Lakini anaweka wazi kuwa kwa siku za hivi karibuni kumekuwapo na sekeseke ambalo limetokea katika  soko la simu Nchini China, ambalo limesababisha simu kuongezeka kwa bei ikilinganishwa kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa maeneo yanayozalisha simu kwa wingi duniani.

“Katika soko la China kuna mambo yametokea ambayo yamepelekea simu kupanda bei pamoja na vifaa vyake kama vioo, motherboard mashine kwenye kampuni kupanda na kufikia kuzinunua kwa dola mbili kwa simu ndogo tofauti na awali, jambo ambalo ukipiga hesabu ya gharama za kusafirisha bidhaa hiyo kuileta hapa nchini unatakiwa ufunge mkanda kwelikweli kwani inakuwa ni shida.

“Lakini hali hii haijaishia kwenye simu hizi ndogo tu kwani hata kwa upande wa simu kubwa
(Smartphone) nazo zimepanda bei kwa vifaa vyake na kufanya kuwe na tatizo kidogo na hivyo kujikuta  pindi zinapofika hapa nchini zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya juu, ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, jambo ambalo linafanya wateja wengi kubaki kuuliza bei tu na kuondoka,”anasema Kalikawe.

Kwa upande wa mwakilishi wa kampuni ya Itel ambayo ni miongoni mwa kampuni changa kwenye biashara hii ya uagizaji simu anasema, ilishazoeleka kuanzia miezi ya Novemba hadi Desemba kuwepo kwa soko kubwa la  simu lakini kwa mwaka  huu imekuwa tofauti na miaka ya nyuma.

“Soko la simu sana sana katika msimu wa  sikukuu, ambapo mauzo ya simu hupanda sana lakini kwa kipindi hiki mauzo yamekuwa tofauti, grafu ya mauzo imeshuka sana, ukiachana na kuwapo kwa hali ngumu ya kimaisha.

“Lakini pia kuwapo kwa ongezeko la bei za simu na kodi ambayo imefanya  mzigo kuwa mkubwa kwa wafanyabiashara wengi ambao hutoa mzigo Dubai na China imewagharimu sana na ndIo maana simu  zimepanda na wateja wamepungua,”anasema.