Home Makala MABALOZI WAIONYA KENYA KUTOREKEBISHA SHERIA ZA UCHAGUZI

MABALOZI WAIONYA KENYA KUTOREKEBISHA SHERIA ZA UCHAGUZI

620
0
SHARE

NAIROBI, KENYA


Mabalozi wa nchi za nje walioko nchini Kenya wameutahadharisha utawala wa chama cha Jubilee kuachana kabisa na mpango wake wa kufanya marekebisho katika sheria za uchaguzi, wakisema kimataifa, si busara na maadili mema kufanya mabadiliko ya sheria za uchaguzi karibu na siku ya kufanyika uchaguzi.

Aidha wamewaonya wanasiasa wanaochochea wananchi kwamba wanaweza kupigwa marufuku kusafiri na kuingia nchi zao (za mabalozi hao) kutokana na kunyimwa viza.

Wakiongozwa na Balozi wa Marekani nchini humo Robert Godec, mabalozi hao wameonya kwamba jumuiya ya kimataifa inafuatilia kwa karibu sana hatua na matamshi mbali mbali yanayofanywa na wanasiasa nchini humo na kwamba zitawawekea vikwazo wale wanaohatarisha amani ya nchi.

Katika taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na mabalozi 14, Godec alisema jumuiya ya kimataifa inafuatilia kila hatua ya mchakato wa uchaguzi na kutathmini kila hatua au matamko mbali mbali kutoka kwa wanasiasa.

Alisema: “Baadhi ya Wakenya wanachochea joto la kisiasa bila sababu, na tunawaomba waache kufanya hivyo. Marekani itachukua hatua pamoja na kuwanyima viza.”

Balozi huyo alitoa taarifa hiyo baada ya kukutana na makamishna Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka – Independent Electoral and Boundaries Commission (IEBC) katika Ukumbi wa Bomas mjini Nairobi kwa ajili ya matayarisho ya uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Oktoba 26.

Godec alieleza kwamba mabadiliko ya busara katika sheria ya uchaguzi iliopo huchukua muda mrefu na kunahitajika fikra za kina na makubaliano mapana kutoka wadau mbali mbali, na si kwa sababu tu ya kukomoana.

Alisema rasimu ya Muswada huo wa mabadiliko ya Sheria ya Uchaguzi (Election Laws Amendment Bill) kwa mfano inaweka shakani uwezo wa IEBC kuendesha uchaguzi mzuri katika katika kipindi cha siku 60 na pia kupandisha bila sababu joto la kisiasa

Alisema Wakenya pia wana haki ya kuujadili Muswada huo lakini muda ndio kikwazo kikubwa.

Mabalozi hao pia waliitaka IEBC kufanya kazi kwa uhuru kabisa na ijizuie kupewa maelekezo kutoka vyama vya siasa au watu wengine.

Kiongozi wa muungano wa NASA Raila Odinga alidai kwamba IEBC ambayo mwenyekiti wake ni Wafula Chebukati, na chama cha Jubilee ni “wana-njama” katika udanganyifu mkubwa wa uchaguzi wa Agosti 8 uliopelekea kufutwa matokeo yake na Mahakama ya Juu (Supreme Court) ya nchi hiyo.

Aidha mabalozi hao walisema orodha inayoongezeka kila siku ya matakwa ya kisiasa, matamshi ya hatari na vitisho vya kususuia uchaguzi vinaathiri uwezo wa IEBC kufanya uchaguzi wa marudio bila bughudha kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Kenya.

Mabalozi hao pia wamesema itakuwa vigumu kuifumua IEBC katika muda mfupi ili kuridhisha pande zote, hivyo kila mwanasiasa anapaswa kujizuia kuidhhofisha Tume hiyo.

 

mwisho