Home kitaifa Mabilioni ya Libya kung’oka na vigogo

Mabilioni ya Libya kung’oka na vigogo

2073
0
SHARE

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SIKU chache baada ya Taasisi ya Kuzui na Kupamba na Rushwa (Takukuru) kutangaza kuwasaka watu wanne wanaodaiwa kutoweka na zaidi ya Sh bilioni 46 za mkopo kutoka Serikali ya Libya, baadhi ya vigogo waliopo serikalini ambao wanatajwa katika mtandao huo, wapo hatarini kung’oka na kufikishwa mahakamani.

Mbali na hao, pia kuna kila dalili kwa baadhi ya viongozi wastaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne nao wapo hatarini kufikishwa mahakamani.

Juni 30, 2016 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliamua kutoa ufafanuzi wa mabilioni hayo ya fedha kutoka Libya ambayo amekuwa akihusishwa nayo, ambapo alieleza kwamba fedha zote zilizotolewa kwa amri ya mahakama ni mkopo na hazikuchotwa kama ilivyokuwa kwenye kashfa za Epa au Escrow.

Fedha hizo, Dola za Marekani milioni 20 (sawa na Sh bilioni 40) zilikuwa zimehifadhiwa katika akaunti ya Libya No.004-200-0002216-01 iliyokuwa Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB).

Kwa mujibu wa waraka aliutoa kwa vyombo vya habari kuhusu fedha hizo, Membe alisema Serikali ya Libya na Tanzania zilitia sahihi mkataba wa nyongeza (Addendum to the Dept Swap Agreement) ambao ulizungumzia pamoja na mambo mengine, matumizi ya fedha hizo.

Mkataba huo wa nyongeza unatamka katika kifungu No.4.02, kwamba fedha hizo zikopeshwe kwa mwekezaji aliyeteuliwa na Libya, ambaye ni Kampuni ya Meis Industries Limited kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa kiwanda cha saruji mkoani Lindi.

Mapema juzi, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, alijitokeza mbele ya waandishi wa habari na kusema kuwa fedha hizo zilitolewa na Serikali ya Libya kama mkopo wenye riba kwa Serikali ya Tanzania.

Alisema kwa kuwa Serikali haifanyi biashara, fedha hizo zilikabidhiwa kwa Kampuni ya Meis Industries Ltd mwaka 2009 kwa ajili ya kujenga kiwanda hicho, lakini hadi sasa hakijawahi kuonekana na wahusika hawajulikani walipo.

“Mwaka 2009 Serikali hizi mbili zilitia saini mkataba ulioitaja kampuni ya Meis Industrial Limited kama kampuni itakayopewa dola milioni 20 za Marekani kwa ajili ya uwekezaji wa ujenzi wa kiwanda cha saruji eneo la Machore mkoani Lindi.

“Fedha hizo zilitolewa kwa Kampuni ya Meis kama mkopo uliopaswa kurejeshwa kwa riba nafuu na kwa mujibu wa mkataba, mkopo huo ulipaswa kurejeshwa ndani ya miaka sita, yaani 2011 hadi 2017. Hata hivyo, hadi mwaka 2019 kampuni hiyo haijarejesha mkopo huo wala kiwanda cha saruji kilichokusudiwa kujengwa bado hakijajengwa,” alisema.

Alisema uchunguzi uliofanywa na Takukuru umebaini kuwa sehemu kubwa ya fedha hizo imetumika kwa matumizi mengine kinyume na makusudio ya Serikali jambo ambalo ni kosa.

Brigedia Jenerali Mbungo alisema wahusika wa Kampuni ya Meis ambao wanatafutwa ni Islam Ally Saleh Balhabou, Merey Ally Awadh Saleh, Sabri Ameir Kuleib na Abdallah Said Abdallah bin Aliya, ambao hadi sasa hawajulikani walipo.

Alisema zipo taarifa kuwa huenda wengine walikimbilia Visiwa vya Comoro na wengine nchini Uingereza, hivyo juhudi za kuwatafuta zinaendelea.

“Tunatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa sahihi za mahali watuhumiwa hawa wanapoweza kupatikana awasiliane nasi ili wakamatwe na kuja kujibu tuhuma hizi zinazowakabili kwa kuwa kosa hili liko chini ya kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007,” alisema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mikopo hiyo, alisema Serikali ya Libya katika miaka ya 1980 iliikopesha Serikali ya Tanzania mafuta ya petrol na dizeli kiasi cha tani 200,000 za ujazo ambayo kufikia mwaka 2005 ilikuwa ikiidai Serikali ya Tanzania Dola 201,000,000.

Alisema kutokana na fedha hizo, Serikali ya Libya ilisamehe nusu ya deni ambapo Seriali hizo mbili zilikubaliana namna ya kulipa dola 101,000,000 zilizobaki.

“Katika makubaliano haya, dola milioni 61 zilitakiwa kulipwa kwa mtindo wa madeni ya kitaifa, dola milioni 20 zilipwe kwa mpango maalumu na dola 20 milioni zifanye uwekezaji nchini Tanzania na baadaye zirudishwe Libya kwa riba nafuu,” alisema.

Alieleza katika mpango huo, Kampuni ya Meis ilipewa fedha hizo kwa ajili ya kufanya uwekezaji nchini ambao ulitakiwa uwe umeshakamilika na urejeshaji wa fedha hizo nchini Libya kwa riba nafuu uwe umeshakamilika kufikia mwaka 2017.

Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani, alinukuliwa na gazeti la kila siku la MTANZANIA kwamba watuhumiwa wanaotafutwa ni raia wa Tanzania ambao ni wakazi wa Kilosa mkoani Morogoro.

“Hawa wote taarifa zinaonesha kuwa ni Watanzania, ambao makazi yao ni Kilosa mkoani Morogoro. Kwa hiyo ni watu ambao taarifa zao ni rahisi kupatikana,” alisema.

Alisema fedha hizo zilitiwa saini na Serikali ya Libya, ambapo kwa upande wa Tanzania Wizara ya Fedha iliiwakilisha Serikali na fedha hizo ziliwekwa kwenye Benki ya Rasilimali nchini (TIB).