Home Uhondo wa Siasa MACHOZI NI ‘JANJA’ YA VIONGOZI KUTAFUTA UUNGWAJI MKONO?

MACHOZI NI ‘JANJA’ YA VIONGOZI KUTAFUTA UUNGWAJI MKONO?

1534
0
SHARE

NA FRANCIS DAUDI

KUNA video inayomwonesha Rais wa zamani wa Zambia, hayati Fredrick Chiluba, akilia mwaka 1993 wakati wa maziko ya kitaifa ya wachezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo. Wachezaji hao walifariki katika ajali ya ndege ambayo ilivuta hisia za wengi.

Huku akionekana mwenye majozi mbele ya halaiki iliyojitokeza katika maziko hayo alianza kwa kutoa maombi na alipozamia katika maombi hayo alishindwa kujizuia na kuangua kilio kikubwa na kupelekea wananchi waliojitokeza kuangua kilio kwa zaidi ya sekunde 15.

Chiluba ni nani?
Frederick Jacob Titus Chiluba, alizaliwa Aprili 30, 1942, alikuwa mwanasiasa wa Zambia ambaye alikuwa Rais wa pili wa Zambia kuanzia 1991 hadi 2001, alitoka madarakani baada ya jaribio lake la kujiongezea muda kukwama. Chiluba, kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi, alishinda katika uchaguzi wa rais wa vyama vingi mwaka 1991 akiwa mgombea wa Movement for Multiparty Democracy (MMD) baada ya kumwangusha rais wa muda mrefu Kenneth Kaunda.

Alizaliwa na wazazi Jacob Titus Chiluba Nkonde na Diana Kaimba na kukulia Kitwe, Zambia. Chiluba alioa mara mbili. Frederick Chiluba alisoma katika Shule ya Sekondari Kawambwa katika eneo la Kawambwa, ambapo alifukuzwa akiwa mwaka wa pili kwa kujishughulisha na mambo ya kisiasa. Alifanya kazi ya ukondakta wa basi na baadaye akawa dereva wa basi.

Ni wakati huo ndipo alipoufahamu uwezo wake wa kuwa mwanasiasa kutokana na haiba yake. Baadaye alifanya kazi kama diwani kabla ya kuwa msaidizi wa mweka hazina wa Atlas Copco, na kupanda hadi mjini Ndola ambako alijiunga na Umoja wa Kitaifa wa Ujenzi.

Mwaka 1990 alisaidia kuundwa kwa Chama cha MMD, chama ambacho Chiluba kama mgombea wake wa urais kilifanikiwa na kuleta changamoto kubwa katika utawala wa Kaunda katika uchaguzi wa 1991. Chiluba alikuwa mzungumzaji mzuri mwenye kipaji cha asili. Chiluba aliingia madarakani Novemba 2 mwaka huo. Alishinda tena katika uchaguzi huo kwa kipindi cha pili cha miaka mitano mwaka 1996 licha ya kesi ya kuhoji uzawa wake.

Chiluba siku zote alionekana nadhifu sana katika umbo lake fupi. Mwonekano wake makini na suti nzuri vikawa ndiyo nembo yake. Katika mfano dhahiri mwandishi wa gazeti la Zambia Post, Roy Clarke ambaye ni mwandishi wa safu ya mara kwa mara ambayo ilimshutumu Rais wakati alipokuwa madarakani, alimfananisha kama “kazi bure, msalaba-wenye mavazi, mvaa-visigino virefu, mgoni na kibete.”

Siku alipolia….
Ndege ya jeshi la Zambia iliyokuwa inawasafirisha wachezaji, kocha na maofisa wengine wapatao 25, Aprili 27 mwaka 1993, ilianguka katika Bahari ya Atlantiki, Pwani ya Jiji la Libreville, nchini Gabon na abiria wote kuangamia. Inaelezwa ndege hiyo ilipata hitilafu na rubani alipojaribu kurekebisha ilijikuta ikiwaka moto na kuanguka ndani ya sekunde chache.
Ikumbukwe kuwa kikosi cha Zambia cha wakati huo kilikuwa ni tishio barani Afrika na kilitarajiwa kufuzu kwa Kombe la Dunia la mwaka 1994. Kikosi hiki cha Chipolopolo kilikuwa na wachezaji wenye vipaji vya kipee na mwaka 1988 wakati wa michuano ya Olmpiki jijini Seoul, nchini Korea Kusini, iliwafunga Italia mabao 4 kwa 0.

Chiluba ambaye alikuwa safarini Afrika Mashariki alirudi na kutangaza wiki ya maombolezo. Siku ya maombolezo ya kitaifa, Uwanja wa soka (Uhuru) ilijaa waombolezaji 30,000 na watu wengine zaidi ya 100,000 walikuwa nje ya uwanja huo. Wananchi walipokea mashujaa wao na kuwasindikiza katika makaburi nje ya uwanja yanayojulikana kama ‘Heroes Acres’. Muda wa kutoa maombi Chiluba alibubujikwa na machozi tu. Haikuwa rahisi kwake kuvumilia majonzi hayo. Angalia VIDEO hii

Chiluba alifariki Juni 18, 2011. Msemaji wake Emmanuel Mwamba alitangaza kifo chake. Mwamba alisema kuwa Chiluba alikuwa na siku ya kawaida Juni 17 na hata alikuwa na muda wa kukutana na baadhi ya wanasheria wake. Baadaye alianza kulalamika kuhisi maumivu ya tumbo.

Dhana ya viongozi kulia

Kama binadamu mwingine kiongozi hufikwa na majonzi makubwa na kutoa machozi, mfano Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alilia alipouona mwili wa marehemu Moringe Sokoine (Aliyekuwa waziri mkuu na kufariki katika ajali ya gari). Miaka ya karibuni kumekuwa na mawazo tofauti kabisa juu ya viongozi kulia mbele ya umati. Mfano tu Rais wa Marekani, Barack Obama alilia mjini Newtown baada ya watoto 20 kupigwa risasi, ilielezwa ni janja ya kutaka kuungwa mkono baada ya chama chake kupoteza viti ndani ya Congress.

Waziri mkuu wa Tanzania (awamu iliyopita) Mizengo Pinda, alitokwa na machozi bungeni juu ya mauaji ya albino. Wapinzani wake walidai ilikuwa ni kukwepa hoja ya Mbunge wa Wawi, Hamad Rashidi ya kumtaka ajiuzulu baada ya kudaiwa kusema kuwa atakayekamatwa akijihusisha na kuua albino naye auawe.

Kwa sasa huko Kenya imezoeleka Makamu wa Rais, William Ruto, huangua kilio na kila anapohudhuria msiba au ibada fulani, inaelezwa naye anatafuta uungwaji mkono ili kujijenga zaidi kwa ajili ya kuchukua kiti cha urais. Angalia katika link hii

Ukiguswa na jambo jaribu kulia kidogo, majonzi yapungue. Usijikaze tu, machozi ni sumu yakibaki mwilini.