Home Habari MADENI: WAFANYABIASHARA WALIA NA TBA

MADENI: WAFANYABIASHARA WALIA NA TBA

2335
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU


Wasambazaji wa vifaa vya ujenzi wameibua malalamiko ya madeni dhidi ya Wakala wa Majengo nchini – Tanzania Building Agency (TBA) kiasi cha zaidi ya Sh milioni 200. RAI linaripoti.

Taarifa hiyo imeibuliwa na wasambazaji hao baada ya TBA kushindwa kuwalipa madeni yao kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Wakizungumza na RAI kwa nyakati tofauti  wasambazaji wapatao wanne walisema kitendo cha TBA kutowalipa madeni hayo kimesababisha baadhi ya viwanda vya vifaa vya ujenzi kufungwa na vingine kuendeshwa kwa kusuasua.

Mmoja wa wasambazaji hao kutoka Kampuni ya Jenga Kwanza ambayo inazalisha matofali mkoani Kagera, Godwin Mlokozi alisema hadi sasa anaidai TBA zaidi ya Sh milioni 153.

Alisema kutokana na kutolipwa fedha hizo kwa wakati amelazimika kufunga kiwanda kimoja cha matofali kati ya viwili alivyo navyo Mkoani wa Kagera.

“Tulisupply matofali kwenye ujenzi wa Shule ya Sekondari Ihungo ambayo mwaka juzi ilikumbwa na tetemeko la ardhi. Tangu mwaka jana Septemba mpaka sasa hatujalipwa na kila tunapofuatilia tunaambiwa subiri wiki hii… mwezi huu … mpaka sasa ni mwaka,” alisema.

Aidha, alisema wapo wengi wanaolalamikia kutolipwa madeni yao na TBA licha ya ujenzi wa shule hiyo kudaiwa kukamilisha na sasa zaidi wanafunzi zaidi ya 600 wamesharejea darasani.

“Inatuathiri kwa sababu tuna viwanda vya matofali ambavyo uzalishaji wake unatumia mashine za kawaida na nguvu kazi ya binadamu ni kubwa zaidi kuliko ya mashine.

“Kuna gharama za kuwalipa wafanyakazi, kusarifisha matofali kwa sababu kutoka tunapozalisha matofali hadi kwenye eneo la mradi ni kama kilomita 75 hivi, kwenda na kurudi ni kilomita 150. Pia kuna ambao wanachimba mchanga na wanafyatua matofali,” alisema.

Alisema wakati anaanza uzalishaji mwaka 2016 alikuwa na viwanda viwili, Bukoba Mjini na nje ya mji lakini sasa amebakiwa na kiwanda kimoja ambacho nacho kinasuasua baada ya kushindwa kukiendesha ikiwamo kuwalipa wafanyakazi wake.

“Licha ya kufunga lakini bado wapo wanaonidai kwani tunaajiri vijana wenye nguvu. Nakumbuka TBA wamenunua mzigo wa kutosha kwani nilisupply zaidi ya asilimia 90 ya kazi iliyofanyika. Hata hii asilimia nyingine ni baada ya kuishiwa kabisa.

“Imeniathiri sana kwa sababu nimekopa Efta magari mapya ya kubeba mzigo. Mwanzo TBA walikuwa wanalipa vizuri hatukukwama hata nikiishiwa mafuta walikuwa wanaleta tunaenda vizuri, zaidi ya milioni 300 walikuwa wanalipa kwa wakati. Ila sasa hali imekuwa tofauti,” alisema.

Malalamiko hayo pia yalidhibitishwa na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Adronicus Karumuna ambaye alilieleza RAI kuwa amekuwa akipokea malalamiko ya madai ya TBA kutoka kwa wasambazaji na baadhi ya wafanyakazi waliocheleweshewa malipo yao kwa zaidi ya mwaka sasa.

Meya huyo alisema licha ya kuwasilisha malalamiko hayo kwa Mkuu wa wilaya, mkuu wa Mkoa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, bado hayajafanyiwa kazi.

“Pia nimewasilisha kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage ambaye anatokea huku kwa sababu wadai  wengi ni wamiliki wa viwanda vya matofali ambao wamesuply mzigo mkubwa kwenye hiyo shule na hawajalipwa fedha zao.

“Kipo kiwanda kinaitwa Jenga Kwanza ambacho kimesupply matofali zaidi ya milioni zaidi ya 150m/- fedha hawalipwa, nilipombana Waziri Ndalichako akasema ameshamlipa TBA zaidi ya asilimia 90 lakini TBA wameamua kukaidi kuwalipa hao wadau.

“Wapo vibarua ambao wamekuja ofisini kwangu kulalamika kuwa wamefanya kazi hawajalipwa pesa zao, kuna supplier wengine wa mbao na vifaa vingine, kimsingi hali sio nzuri kwa sababu serikali inasema imemlipa TBA lakini TBA haijatoa hiyo pesa kwa wanaowadai,” alisema.

Aidha, Meya huyo aliongeza kwa kusema kuwa licha ya shule hiyo kudaiwa kukamilika wapo wasambazaji wa samani na vifaa mbalimbali ambao humfuata kila mara kumuuliza kuhusu madai hyao.

“Nadhani kuna tatizo kidogo. TBA nimezungumza nao hasa meneja wa TBA aliyepo huku ambaye ni msimamizi wa haya majengo tena si mara moja. Nakumbuka RC wa awali kabla ya kustaafu alifanya ziara kwenye mradi huo na tulipofika pale Meneja wa TBA hakutaka kueleza hayo matatizo.

‘Akamwambia tunaendelea vizuri.. mimi nikasema hapana kuna moja, mbili. Pia alipokuja waziri Ndalichako meneja huyo alitoa taarifa kuwa mradi unaenda vizuri na watu wanadai kidogo kidogo, lakini nikampinga tena. Ndalichako naye alisema kuwa wizara imeshailipa TBA kiasi kadhaa kwa hiyo tatizo lipo TBA,” alisema Meya huyo.

Akizungumzia madai hayo Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Elius Mwakalinga alikana kufahamu chochote juu ya madai ya madeni hayo na kumtaka mwandishi kuwasiliana na Meneja wa TBA Kagera ambaye ni mratibu wa mradi.

Pamoja na hayo alisema suala la TBA kudaiwa na wakandarasi au wasambazaji ni jambo la kawaida kwani hata kampuni nyingine za serikali kama SUMA JKT zinadaiwa madeni makubwa kuliko ya TBA.

“Siyafahamu, ukiwasiliana na meneja mkoa wa kule atakueleza lakini kuhusu mradi wa Magomeni ulishaanza na unaendelea.

“Kama mkandarasi mwingine yeyote TBA haiwezi kuacha kudaiwa kwa sababu mara nyingi mtu anasupply alafu analeta madai, tunam-scrutinize (tunamchambua) baadaye tunalipa. Sisi pia tunatakiwa kupeleka maombi, alafu tukilipwa tunalipa, hiyo ni hali ya kawaida ambayo ipo kwenye sekta ya ujenzi. Ukienda kokote hata Suma utashangaa, wanadaiwa hata kuliko sisi huku kwetu.

“Nashangaa kwanini TBA, ni vitu ambavyo ni vya kaiwada, labda ingekuwa mradi una ubora wa hovyo au gharama ni kubwa hapo sawa ila suala la madai hayo ni jambo la kawaida,” alisema.

Hata hivyo, akizungumzia kukwama kwa baadhi ya miradi ikiwamo ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni kota Dar es Salaam, Mwakalinga alisisitiza kuwa mradi huo unaendelea vizuri.

Aidha, akizungumza na RAI, Meneja TBA – Kagera ambaye pia ni mratibu wa mradi huo, Mhandisi Salum Chanz alisema suala la mradi huo linahusu serikali hivyo si mradi wa kihuni huku akionyesha kushangazwa na hatua ya bosi wake kumrushia mpira.

“Mimi ni meneja na mratibu wa huu mradi, Kama afisa Mtendaji Mkuu amesema uwasiliane na mimi angenijulisha kwa sababu yeye ni signatory wa mkataba.

“Ila sisi hatufanyi kihuni, sisi wenyewe tunadai,” alisema meneja huyo.

Ikumbukwe kuwa Julai 24 mwaka huu TBA ilitoa gawio la Sh bilioni 1.7 kwa Serikali katika kipindi cha mwaka fedha 2017/18.

Kwa kawaida, gawio hutolewa baada ya madeni, kodi pamoja na gharama za uendeshaji zikiwa zimelipwa.

Wakati gawio hilo likitoa picha kwa umma kuwa hali ya kifedha ndani ya TBA ni nzuri kiasi cha kutengeneza ziada, uhalisia unadaiwa kuwa tofauti kutokana na wakala huyo kuandamwa na mzigo wa madeni.