Home Habari Madhila wanayokutana nayo wanafunzi waliokosa hosteli

Madhila wanayokutana nayo wanafunzi waliokosa hosteli

1453
0
SHARE

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

KATIKA mwendelezo huu wa madhila wanayokutana nayo wanafunzi waliokosa hosteli, Rai linaendelea kukufamisha namna ambavyo wasomi hawa na wataalamu watarajiwa jinsi ambavyo wamekuwa wakihitimu taaluma zao huku wakiwa wamebeba vinyongo ambavyo kwa kiasi kikubwa vinatokana na mifumo na miundombinu haba na ulegevu wa wazazi vinazosababisha waishi maisha ya udhalili mkubwa.

Pamoja na jitihada kubwa ambazo zinaonyeshwa na wanafunzi wa wa elimu ya juu katika kuhakikisha kuwa wanafikia ndoto zao kitaaluma, lakini ushiriki wa wazazi bado ni changamoto hatua inayosababisha wengi kusoma kwa msongo ikiwamo kufanya vibarua kama kuwa walinzi usiku na wengine kugeuka kuwa mama lishe kwa lengo la kupata mahitaji ya kujikimu.

Hata hivyo, jambo la kushangaza si tu kwamba wanaosoma kwenye mazingira magumu ni wale tu waliopanga mitaani bali hata wale walioko kwenye hosteli na nyumbani kwa wazazi nao wanakabiliwa na changamoto.

Katika hilo, kutalakiana kwa wazazi nako kumekuwa ni kichocheo cha wanafunzi hao kupata elimu kwenye mazingira yanayofadhaisha zaidi kutokana na kushindwa kupata mahitaji muhimu.

Hatua hiyo na nyingine zenye sura kama hiyo zikiwamo kucharazwa fimbo na wazazi wao kwa wanafunzi wanaosoma wakitokea majumbani zimefanya baadhi yao kuahirisha mwaka kutokana na madhila wanayokutana nayo kwenye safari hiyo ya kusaka elimu.

Jambo la kushtua zaidi ni kwamba wazazi wa wanafunzi hawa wa elimu ya juu ambao wamekuwa wakiwapitisha kwenye tanuru la moto, na kuwa vinara wa kusema uongo pale wanapotakiwa na uongozi wa chuo kubainisha vikwazo vya kushindwa kutimiza wajibu wao kwa watoto wao jambo linalochangia msongo wa mawazo.

Baadhi wa wazazi wamekuwa wakishindwa kumudu kulipia ada mfano Sh. 600,000 au hata wanapofanya hivyo bado imekuwa ni mtihani kumudu fedha ya matumizi kwa mwanafunzi husika hali inayochochea baadhi kuahirisha mwaka.

Changamoto hizo na nyingine zenye kufanana na hizo ndizo zinamgeuza, Paulina Mabuga ambaye ni Mlezi wa Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kugeuka kuwa mshauri na mtatuzi wa changamoto hizi kwa wale wanaoiamini ofisi yake kuwa kimbilio, huku wale wanaoshindwa kufanya hivyo wakihitimu na kisha kuondoka na mafundo ya sonona mioyoni mwao.

Paulina alisema kuwa kuna wanafunzi wengi ambao wanasoma kwa changamoto kiasi kwamba inafikia hatua ya kufanya vibarua ili waweze kufanikiwa kujimudu kimaisha.

“Kuna changamoto kubwa kwa wanafunzi hawa wa elimu ya juu ambazo tunalazimika kupamabana nazo, kwani inafika wakati mwanafunzi anaweza akaja anakwambia kuwa Madame mimi naomba unitafutie kazi kwa yule dada wa Cafeteria (mgahawa), hivyo kuna wanafunzi wanakuwa wanasoma huku wanafanyakazi.

“Lakini ukiacha hiyo, wapo wale ambao unakuta wanasoma huku anafanyakazi ya ulinzi kwenye Kampuni binafsi za ulinzi na hizi ni kutokana kwamba wengi wamepata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walipohitimu kidato cha sita na pale changamoto zinapowabana kabisa wanakuwa hawawezi kuendelea na kazi kwa maana masomo yanawatinga.

“Wengine unakuja kugundua kwamba ameomba kazi ya kufanya ulinzi usiku ili tu aweze kumudu maisha kwa maana ya mchana awe darasani na usiku awe kazini ili kumudu maisha, yupo pia aliyeomba kazi bandarini na sehemu nyingine.

“Jambo la kushukuru ni kwamba kwa sasa tumeweza kuwasaidia na wameweza kuondokana na changamoto hii ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwepo mwaka jana, jambo lilolazimu kuingilia kati na kuwasaidia wanafunzi hawa. Hivyo sina hakika kama kuna vitendo hivi vinaendelea,” alisema Paulina na kuongeza kuwa baadhi ya wanafunzi hulazimika kufanya udobi ili kupata fedha za kujikimu.

Wakati ukistaajabu hilo, ni kwamba wapo pia wanafunzi ambao hawaishi machozi moyoni kutokana na mateso makali wanayoyapata kutoka kwa wazazi wao kila iitwapo leo hali inayowalazimu kutamani kuacha masomo.

“Shida inakuja kwamba, siyo wazazi wote wanafanya maandalizi ya watoto wao ikiwamo kugharimia elimu yao, mfano mwaka huu kuna mwanafunzi ambaye nililazimika kumuingiza kwenye mfuko wa kusaidia wanafunzi tuliouanzisha hapa chuoni miaka mitatu iliyopita, kwani kuna mwanafunzi ambaye baba yake alilipa ada, baadaye akampa Sh. 100,000 baada ya miezi mitatau mtoto akaomba tena hela kwa baba yake, lakini aliishia kumgombeza.

“Nilipomuuliza mwanafunzi akasema kwenye hiyo Shilingi 100,000 ya baba yake alichukua Shilingi 50,000 akalipa chumba kisha nusu iliyobaki akaitumia kujikimu kwa miezi mitatu wanaitapasi ndefu (kujibana) jambo ambalo lilipelekea mtoto kulia na kuchanganyikiwa kila wakati kutokana na ukali wa mzazi hatua ambayo inafanya hata kushindwa kufua nguo zake.

“Hivyo utakuta wenzake uvumilivu unawashinda wanafikia hatua ya kukwambia kwamba ‘Madame tunakuomba uzungumze na huyu mwenzetu’, basi hapo ndipo utagundua mambo mengi mazito hadi unashindwa kufahamu kwamba huyu ni mzazi wake kweli au laa!,” alisema Mshauri huyo wa wanafunzi

KUACHANA WAZAZI

Alisema kuwa kutalikiana kwa wazazi nako kumekuwa ni sababu nyingine ya wanafunzi wengi kusoma kwa mateso na akili kuvurugika, kwani hata pale anapobaki mzazi mmoja au watoto kuishi na mama au baba wa kambo nayo imekuwa ni hatari kwa kuwa wengi wanasoma kwenye mazingira ya machozi.

“Kuna baadhi ya wazazi ambao wanafanya wanafunzi kujinyanyapaa kabisa, kwani mfano kuna mwanafunzi alilazimika kuairisha kabisa mwaka kwani alikuwa akipitia mateso makali kutoka kwa mama wa kambo, alikuwa akimpiga kila wakati licha ya kiwango chake cha elimu alichonacho hatua ambayo ilimlazimu kuahirisha mwaka.

“Hata hivyo jambo la kushukuru ni kwamba amekuwa ni mtu mwenye uwezo mkubwa, anayejiweza darasani hatua ambayo imefanya ajiamini zaidi licha ya kwamba nyumbani anaishi ‘mazingira magumu’ hivyo tuliweza kumpa ushauri na kumwambia apige moyo konde jambo ambalo ametuelewa.

“Kwani wakati akiwa ngazi ya sekondari alikuwa akiishi vizuri shida ilianza tu baada ya kufika huku juu ndiko changamoto ilikoanzia japo kwa sasa amezoea na karibu anamaliza chuo licha ya kuchapwa nyumbani,” alisema Paulina.

Hata hivyo Paulina anakiri kabisa kuwa kwa wanafunzi kukaa nje ya hosteli za chuo ni changamoto kwani kunawafanya kutumia gharama kubwa pia suala la muda.

“Unajua mfano hapa kwetu chakula kama ubwabwa maharage ni Shilingi 800 hadi Shilingi 1,000 fikiria kama mtoto amepanga na anahitaji kula aina hiyo ya chaukula nyumbani? Jambo ambalo litamchukua gharama kubwa pamoja na muda mrefu hali inayoleta uchovu pia hata ubora hauwezi kulingana na na kile kinachotayarishwa hapa wakati mwingine kukosekana kwa utulivu huko mitaani na umeme wa kusuasua nako ni changamoto ambayo tunatambua fika kwamba unawakabili wanafunzi wetu waliko mitaani.”

WANAOSHINDWA KUMUDU

Alisema kutokana na kuwapo kwa changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili wanafunzi wanaoishi mitaani na wengine hususan ile ya ada ya pango na mahitaji mengine muhimu, chuo hicho cha Dar es Salaam kimeanzisha mfuko maalumu unaotimiza miaka mitatau sasa, ambao una lengo la kuhakikisha wanafunzi wenye changamoto wanasaidiwa.

“Mfuko huu tukishajiridhisha kwamba mwanafunzi huyu anashida, basi tunamuingiza kwenye orodha ya mfuko huu na kuanza kumtafutia wafadhili mfano Mfanyabiashara, Mohammed Dewji anasomesha jumla ya wanafunzi 63,” alisema.

Wakati hali ikiwa hivyo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais wa Serikali ya Wanafunzi katika Chuo Kikuu Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Agustino Evarist alisema kuwa changamoto ya ukosefu wa mabweni imekuwa ni moja ya tatizo sugu chuoani hapo.

Alisema tatizo hilo limekuwa mwiba kwa baadhi ya wanafunzi hali inayosababisha wengi wao kuishi kwenye nyumba za kupanga bila mikataba.

“Hakuna shaka kwamba vyuo vingi hosteli za ndani zimekuwa ni changamoto hali ambayo inafanya kundi kubwa la wanafunzi kuishi nje ya chuo japo katika hili pia wapo wanafunzi ambao wamekuwa wakipenda pia kuishi katika utaratibu huu wa maisha.

“Hata hivyo jambo linalosikitisha ni kwamba wanafunzi wengi wanaoishi huku mitaani wamekuwa hawapewi mikataba jambo ambalo linafanya wengi wao kuondolewa kinyemela pale wenye nyumba wanapotokea wamewachoka tena pasipokupewa muda wa kujiandaa (notisi) na hii ni moja ya tabu kubwa ambayo tumekuwa tukikabiliana nayo mara kwa mara kutoka kwa wanafunzi wetu hapa.

“Pia hata wale wenye mikataba wakati mwingine wamekuwa wakiondolewa tu kwenye nyumba kutokana na matakwa ya mwenye nyumba jambo ambalo limekithiri sana katika maeneo ya Kigamboni ambako huku kuna kundi kubwa la wanafunzi wa vyuo vingi vilivyoko katikati ya mji,” alisema Evaristi.

Alifafanua kwamba pamoja na wanafunzi hao kuishia kuhamishia makazi yao mitaani huko, bado maisha yao yamekuwa ni ya wasiwasi kutokana na kukosekana kwa usalama wa kuaminika hali ambayo imesababisha baadhi yao kujeruhiwa na vibaka, kuchaniwa kwa nyavu zao za madirisha na kuibiwa baadhi ya mali na vyenzo zao muhimu za kujifunzia.

WATAALAMU WA SAIKOLOJIA

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU) alisema kuwa

“Elimu ya kweli humjenga mwanafunzi kufikiri, kudadisi, kuona changamoto zinazoikabili jamaii yake na hivyo kuchochea ubunifu unaomfanya atafute ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili jamii yake. Lakini ili hilo liwezekane, lazima mwanafunzi awekewe mazingira mazuri ya kujifunzia.

“Mazingira haya ya kujifunzia kwa kawaida yanajenga kwenye hulka zetu binadamu.  Kuna vitu tusipovipata kama binadamu hatuwezi kufikiri vizuri, kwanza kabisa tunahitaji mahitaji ya kutuwezesha kuishi kama chakula, malazi na mavazi. Bila mahitaji haya hatuwezi kuishi, tukiyapata haya kwa kawaida tunakuwa na nguvu ya kutafuta mahitaji mengine tunayoyaona kuwa muhimu.

“Kisaikolojia baada ya mahitaji ya msingi yanayotuwezesha kuishi tunahitaji kujisikia salama mbali na hatari. Lakini bila usalama, kwa maana ya pale tunapokuwa kwenye tishio la maisha yetu tunakuwa watu wenye wasiwasi. Huwezi kuwa mtu mwenye hofu na ukafanya shughuli zako vizuri. Kwa mwanafunzi, ni muhimu sana ajisikie mtu mwenye amani na hakuna kinachompa bughudha. Ukishajisikia salama kisaikolojia huridhika.

“Unahitaji uhuru wa kwenda unakokutaka, bila uhuru utajisikia mtumwa, ingawa kiasi cha uhuru hutegemea mambo mengi kama umri wa mtu na aina ya mazingira tulipo, ukweli ni kwamba tunahitaji kuwa na uwezo wa kuchagua tunayoyataka. Mwanafunzi mwenye uhuru ndiye anayeweza kufikiri. Uhuru ni zaidi ya kujitegemea kwa maana ya kwenda anakokutaka, lakini pia uhuru wa kufikiri.

“Sasa kwa kawaida uhuru ndio hasa msingi wa kuanzisha mahusiano ya karibu na watu, kitu ambacho kinachangia sana kujenga hali ya mtu kujiamini ili aweze kutoa mchango wake katika jamii. Huwezi kuwa na mahusiano mazuri na watu kama una shida na mahitaji yako ya msingi. Mtu asiyejisikia salama kama tulivyoeleza hawezi kuwa na mahusiano mazuri na watu wanaomzunguka,” alisema Bwaya.