Home Latest News MADIWANI CHADEMA WAZIDI KUTOROKEA CCM IRINGA

MADIWANI CHADEMA WAZIDI KUTOROKEA CCM IRINGA

976
0
SHARE

NA FRANCIS GODWIN, IRINGA

WAKATI kampeni  za uchaguzi mdogo wa madiwani unaofanyika kwenye kata 43 nchini zikiendelea kwa vyama vilivyosimamisha wagombea kuendelea kujinadi kwenye kata mbalimbali.

Katika kata ya Kitwiru jimbo la Iringa mjini mambo yamebadilika baada ya aliyekuwa mgombea Ubunge  jimbo la Iringa mjini katika Uchaguzi wa mwaka 2015, Frederik Mwakalebela(CCM) kuonekana kuwa na ushawishi mkubwa huku diwani wa Chadema kata ya  Kihesa,  Edga Mgimwa akijiuzulu na kujiunga na CCM .

Mbele  ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa chama hicho, Livingstone Lusinde, Mwakalebela  ameonyesha kuendelea  kukubalika  zaidi Iringa mjini.

Mwakalebela  akiwa  jukwaaani aliwaomba  wananchi wa  Kitwiru  kutopoteza  muda kumchagua mpinzani  katika kata hiyo na kuwataka kura zote kumpa Baraka Kimata wa CCM.

“Nawaombeni sana kama  mlivyoonyesha kunikubali  naomba kura  zenu  zote  mpeni Kimata  ili  kwa  kushirikiana na Rais Dk. John Magufuli aweze  kuleta maendeleo,” alisema Mwakalebela.

Pamoja na Mwakalebela pia tukio kubwa jingine ambalo limeonekana kutikisa kampeni hizo ni kitendo cha kujiuzulu kwa aliyekuwa  diwani wa Chama cha Demokrasia na Maendelea (Chadema) Kata ya  Kihesa,  Edgar Mgimwa na wanachama wengine sita kuhama chama hicho na kujiunga CCM kwa kile walichobainisha kuwa ni kuchoshwa na ubabaishaji ndani ya  chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Tukio hilo ni mfululizo wa madiwani wa chama hicho kujiunga na CCM kwani takumbukwa kuwa miezi kadhaa iliyopita madiwani wengine watatu wa chama hicho walijiunga na CCM akiwamo diwani wa kata ya Kitwiru, Baraka Kimata huku wengine wakiwa ni  Leah Mleleu na Husna Daudi waliokuwa madiwani wa viti maalumu.

Baada ya kutangazwa kwa uchaguzi wa marudio wa kata hiyo, Kimata aliyejiunga CCM muda mfupi baadae alishinda kura za maoni na kusimamishwa kwa tiketi ya chama hicho kuwania tena udiwani wa kata hiyo utakaofanyika Novemba 26, mwaka huu.

Akitetea uamuzi wa CCM kumsimamisha tena, Kimata kuwania udiwani katika kata hiyo aliyoiongoza kwa miaka miwili akiwa Chadema, Lusinde alisema; “Kwa kuwa Chadema walisema mtu kwanza, chama baadae ndio maana tumemrudisha Kimata ili tuone unafiki wao,”.

Pamoja na kwamba Kimata alijiunga na CCM muda mfupi baada ya kujitoa Chadema, Leah na Husna walipokelewa na Polepole katika tukio lililokwenda sambamba na kumpokea diwani wa kata ya Kihesa na wanachama wengine sita wa Chadema.

Akiwapokea madiwani na wanachama hao, Polepole alisema mwaka 2015 CCM walifanya kosa la kizembe lililosababisha jimbo la Iringa Mjini liende tena kwa, Mchungaji Peter Msigwa na wapoteze Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa wapinzani wao hao.

“Tukiri tulifanya makosa ya kizembe akapata ubunge, lakini leo nimekuja Iringa kumpa ujumbe mzito Mchungaji Msigwa kwamba ajiandae kurudi kanisani akachunge kondoo wa bwana,” anasema na kuongeza kuwa.

“Huyu Mbunge ndiye yule aliyewahi kusema mtu yoyote atakayemuunga mkono Edward Lowassa anastahili kupimwa akili, cha kushangaza baada ya muda mfupi alikuwa mmoja wa viongozi wa Chadema aliyemuunga mkono kiongozi huyo lakini hadi leo, hajaenda kupimwa akili,” alisema.

Anasema anaamini kuwa wapinzani wanojiunga na CCM ni dhahiri kuwa wanaridhishwa na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM unaosimamiwa na Rais Dk. John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Akizungumza kwa niaba yao, Diwani wa Kihesa anasema kuwa hajutii uamuzi wa kujitoa Chadema na kujiunga CCM kwasababu anaridhishwa na jinsi siasa zake zinavyoendeshwa na namna Serikali ya awamu ya tano inavyoshughulikia kero mbalimbali za wananchi.

“Kimsingi mimi nilikuwa CCM kabla ya kugombea udiwani katika kata hii mwaka 2015, nilifuatwa na Chadema Julai 2015 na kuombwa kugombea, kuna matatizo makubwa ndani ya Chadema, hakuna demokrasia na kimekithiri kwa ubabe, kwahiyo nimeamua kurudi nyumbani,” alisema Mgimwa.

Upande wake Polepole amekuwa akiwahimiza wananchi wa kata huzika ambao ndiyo wapiga kura kuhakikisha kuwa wanachagua CCM na kwamba licha ya uchache wao lakini wamekuwa wakitazamwa kwa jicho la karibu na, Rais Magufuli na CCM kwa ujumla.

“Tunatambua kuwa changamoto kubwa za kata hii ni pamoja na shida ya maji, changamoto ya daraja la Kitwiru hivyo tunapenda tuwahakikishie kuwa hiyo yote ni kazi yetu, ipo ndani ya Ilani yetu hivyo tutaziagiza mamlaka zinazohusika ili ziweze kushughulikia,” anasema Polepole.

Akiomba kura kwa wananchi wa kata hiyo Kimata alisema kuna kila dalili Mchungaji Msigwa akabaki  pekee yake katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 kwa kuwa hataki kuambiwa ukweli, huku akielezea mvutano uliopo ndani ya Chadema.

“Nilipokuwa Chadema nilikuwa na mvutano mkubwa na wa muda mrefu wa kiutendaji na mbunge wa jimbo la Iringa Mjini kwasababu ni mtu asiyeambilika, hataki ukweli na anayeamini anajua kila kitu, nilikuwa pia Katibu Mwenezi wa Chadema Jimbo na hii iliniweka katika mazingira magumu sana,”.

Mkoa  wa  Iringa ni kata  Mbili zinazorudia  uchaguzi kata ya  Kitwiru iliyoko Iringa mjini baada ya  Diwani  wake  kujiuzulu na kujiunga na CCM na Kimara Wilaya ya  Kilolo ambako diwani wa CCM alifariki dunia.

Katika  uchaguzi   huo  mgombe wa CCM ni Amon Kikoti  mkazi wa kijiji cha Uruti ndani ya Kata hiyo, Chadema imemsimamisha Tumson Kisoma wa mjini Iringa.

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Christopher Magala amewataka wapiga kura wa kata hiyo kujihadhari na matapeli wa kisiasa wanaobadili rangi za hoja zao kila kukicha.

“Kabla Rais Magufuli haijaingia madarakani hoja zao zilikuwa rushwa, ufisadi, ubadhilifu wa mali za umma na nyingine nyingi. Baada ya hayo yote kuanza kushughulikiwa katika awamu hii ya uongozi, wamebadilika na sasa  wanatetea watu wanaojihusiha na vitendo hivyo, nchi haihitaji viongozi wa aina hiyo,” anasema Magala.

Akimuombea kura mgombea huyo, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto alisema; “Kikoti ana sifa za kuwa msaidizi wangu kwa kuwa ni mwadilifu, mwaminifu na mchapakazi, hivyo mchagueni yeye,” alisema Mwamoto.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Zainabu Mwamwindi alisema kata ya Kimala ni kata iliyoongozwa na CCM kwa miaka yote itakuwa miujiza kama watakengeuka.

Akiomba kura kwa wananchi hao, Kikoti alisema atakuwa tayari kutembea kwa miguu kwenda kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa vijiji vya kata hiyo na kuziwasilisha katika mamlaka zinazohusika kwa utatuzi.

“Nitaanzia pale alipoishia diwani aliyetutangulia mbele za haki, nitafanya kazi kwa maarifa na juhudi zangu zote ili kero zilizopo katika kata hii zishughulikiwe ndani ya muda stahiki, uwezo huo ninao,” alisema Kikoti.