Home Michezo Kimataifa Madrid msimu ujao acha kabisa

Madrid msimu ujao acha kabisa

1632
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

MSIMU uliomalizika hivi karibuni uliwashuhudia wakiondoka mikono mitupu. Taji la La Liga lilitua kwa wapinzani wao wakubwa, Barcelona.

Pia, waliambulia patupu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakiondoshwa na Ajax, wakati ubingwa wa Copa del Rey ulitua Valencia.

Waliumaliza msimu wakiwa wamepoteza mechi 18 katika michuano mbalimbali, rekodi mbovu kuwahi kuwatokea tangu msimu wa 1995-96.

Kipigo kilichoonekana kuwakera mashabiki wa timu hiyo ni kile cha mabao 5-1 kutoka kwa Barca katika mchezo ulioondoka na kibarua cha kocha Julen Lopetegui.

Hivyo basi, mabosi wa klabu hiyo ya jijini Madrid wamepania vilivyo kuhakikisha majanga hayo hayajirudii msimu ujao.

Sehemu ya mpango huo ni kocha wao, Zinedine Zidane, kufanya usajili wa ‘kufa mtu’ katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.

Ikiwa ni miaka mitano imepita tangu Madrid walipofanya usajili wa bei mbaya, walipochukua James Rodriguez kwa Pauni milioni 63 akitokea Monaco, wanataka kurudia matanuzi yao sokoni.

Tayari wameshaanza na beki wa Porto, Eder Militao, nyota wa Santos, Rodrygo Goes, huku straika wa Frankfurt, Luka Jovic, naye akitajwa kuwa njiani kwa Pauni milioni 52.4.

Wakati huo huo, Madrid wameendelea kushikilia msimamo wao wa kumng’oa Eden Hazard pale Chelsea, ikielezwa kuwa wako tayari kuweka mezani kitita cha Pauni milioni 88.

Habari inaongozana na ile inayosema Madrid hawana mpango wa kutemana na kinda wa PSG raia wa Ufaransa, Kylian Mbappe.

Hata hivyo, orodha ya wanaotakiwa Santiago Bernabeu haiishii hapo kwani kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Sky Sports, bado Madrid wanaamini watafanikiwa kuinasa saini ya kiungo wa Manchester United, Paul Pogba.

Katika kile kilichowapa kasi Madrid, miezi miwili iliyopita, Pogba alisema kuichezea timu hiyo, tena chini ya Mfaransa mwenzake, Zinedie Zidane, ni moja ya ndoto zake kubwa.

Ukiacha hao, Madrid ina orodha ndefu ya mastaa wake wanaorejea wakitoka kucheza kwa mkopo katika klabu mbalimbali.

Ni orodha inayowajumuhisha James Rodriguez anayetokea Bayern Munich na Mateo Kovacic aliyekipiga kwa mkopo pale Chelsea.

Bayern hawajaonekana kutaka kumnunua moja kwa moja Rodriguez, ambaye wangeweza kukamilisha dili hilo kwa euro milioni 42.

Kama Arsenal watazembea licha ya kuonesha kumtaka, ukweli ni kwamba Napoli na Juventus nao zinamtolea macho, zikionesha kuvutiwa na huduma ya nyota huyo raia wa Colombia.

Kwa upande mwingine, wakati nyota hao wakiwa kwenye rada za rais wa Madrid, Florentino Perez, tayari ameshampa ruksa Zidane, akimwambia anaruhusiwa kutimua yeyote asiyemtaka kikosini.

Tayari rais wa zamani wa Madrid, Ramon Calderon, ameshaonesha wasiwasi wake juu ya hatima ya Gareth Bale, akiamini huenda akapigwa bei.

Akiizungumzia hatima ya Bale, kocha wake, Zidane, anasema: “Sijui kitakachotokea. Mimi ndiye mwenye uamuzi wa mwisho juu ya atakayecheza na atakayekuwa benchi lakini lolote linaweza kutokea mwakani.:

Pia, isisahaulike kuwa mwishoni mwa mwezi uliopita, rais Perez alikiri kuwa nahodha wake raia wa Hispania, Sergio Ramos, aliomba kuondoka.

Licha ya ombi lake kukataliwa, klabu kadhaa za Ligi Kuu ya China zimeanza kumtolea macho mlinzi huyo kisiki anayesifika kwa kuwatuliza washambuliaji wasumbufu.

Aidha, ni wazi mlinda mlango wao, Keylor Navas, ataondoka, hasa baada ya gazeti la AS kuripoti kuwa Madrid wameshamwambia aende tu.

Jeuri ya Madrid katika eneo hilo la lango inatokana na uwepo wa kipa wa kimataifa wa Ubelgiji aliyejiunga nao akitokea Chelsea, Thibaut Courtois.