Home Habari MAFAO YA WAFANYAKAZI YAMTIKISA RAIS

MAFAO YA WAFANYAKAZI YAMTIKISA RAIS

5138
0
SHARE
NA HILAL K SUED NA MITANDAO    |   

UTAWALA wa kibabe na kiimla wa Rais wa Nicaragua, Daniel Ortega huenda ukafikia kikomo kutokana serikali yake kushutumia kuchota fedha za wafanyakazi kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii, nchini humo.

Kwa miaka mingi Ortega amekuwa akichota mabilioni ya fedha kutoika kwenye mifuko hiyo kwa ajili ya shughuli zake, ambazo zinaelezwa wazi kuwa hazina tija kwa wananchi wake.

Aprili 18, mwaka huu mambo yalianza kumwendea kombo baada ya kutoa agizo la kupunguza pensheni za wafanyakazi kwa asilimia tano na kutaka makusanyo yaongezwe zaidi.

Wananchi wenye hasira waliingia barabarani kuandamana, hata hivyo vikosi vya polisi na vijana wanaomuunga mkono Ortega walipambana nao kwa virungu na risasi.

Hatua hiyo ilisababisha watu wanaokadiriwa kufikia 40, kupoteza maisha. Mbali na mauaji hayo, lakini pia Serikali imefungia vituo kadhaa vya runinga.

Matumizi makubwa ya nguvu, pamoja na uamuzi wa Ortega kufuta agizo lake hilo kwa pamoja vilisaidia kurejesha utulivu.

Wadadisi wa mambo wanaamini kuwa huo ndio mwanzo mpya wa Ortega na mke wake kuanza kupingwa waziwazi.

Nicaragua ni miongoni mwa nchi chache za Bara la Amerika ya Kusini, ambazo bado zimesalia kuongozwa na tawala za kimabavu.

Ortega alikuwa kiongozi mashuhuri zaidi wa utawala wa “Kimapinduzi ya Sandinista” nchini humo katika miaka ya 1980, lakini alishindwa katika uchaguzi wa 1990.

Baadaye aliingia katika muungano usiofaa na mpinzani wa kihafidhina, muungano ambao ulimuwezesha kurejea madarakani kwa asilimia 38 ya kura mwaka 2006.

Tangu wakati huo ameng’ang’ania madarakani akipambana kuzibomoa taasisi za kidemokrasia nchini mwake.

Katika uchaguzi wa mwaka 2006 alikipiga marufuku chama kikuu cha upinzani hali iliyomsukuma nchi yake kuifuata Venezuela na hivyo kuzifanya nchi mbili hizi za Amerika ya Kusini kutupilia mbali demokrasia na kukumbatia udikteta.

Ortega anatawala kwa kuunganisha matamshi ya mrengo wa kushoto na sera za mrengo wa kulia huku akiiachia sekta binafsi na Kanisa Katoliki kufanya watakavyo ila tu wasiingize nchi katika mzozo na Marekani.

Ameendelea kuwafanya watu masikini kuwa ngome yake kuu kwa msaada wa Dola za Kimarekani bilioni tano anazopewa na Venezuela.

Katika kuimarisha ngome yake, amemteua mkewe Rosario Murillo kuwa Makamu wa Rais, hali inayotajwa kuongeza kasi ya ufisadi.

Wadadisi wa mambo wanasema yote haya yanabeba harufu ya utawala wa kikatili na kifisadi wa ukoo wa Somoza uliopinduliwa mwaka 1979.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini humo wanaeleza kuwa viongozi wengi wababe husahau kwamba tawala za kiimla hupenda kutegemea muonekano wao wa umaarufu wanaoujenga kuliko tawala zile za kidemokrasia.

Wadadisi wanasema Ortega amezidhibiti taasisi za utawala na kuzifanya kuwa kama kinga dhidi ya wananchi wenye hasira. “Katika hali ya namna hii watawala wa kidikteta wanaweza kuanzisha mazungumzo, au kujichimbia zaidi madarakani na kuendelea kupambana.”

Tayari ameonesha ishara ya kutaka mazungumzo na wafanyabiashara na viongozi wa Kanisa Katoliki. Hata hivyo zipo dalili za makundi hayo kudai wigo mpana zaidi katika mazungumzo hayo.

Mazungumzo haya yanaonekana kutohusisha suala la pensheni pekee, kwani lazima mazungumzo hayo pia yajumuishe uchunguzi wa vifo vilivyotokea na ukaguzi huru wa mahesabu ya serikali, hususan fedha wanazopata kama misaada, kurejeshwa kwa uhuru wa kisiasa na marekebisho katika Tume ya Uchaguzi na katika Mahakama ya Juu (Supreme Court).

Hata hivyo wengi wanasema Ortega hawezi kuridhia yote haya. Akiwa na umri wa miaka 72, anaonekana kutaka kumrithisha urais mkewe Murillo na anaamini hataweza kulifanikisha hilo kwa njia za kidemiokrasia na hapo ndipo machafuko yanaweza kuanza.