Home Latest News MAFISADI WANGAPI WASALIA CCM?

MAFISADI WANGAPI WASALIA CCM?

773
0
SHARE

NA JULIUS MTATIRO

SIKU moja baada ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, kuondoka CCM na kuhamia Chadema, uamuzi ambao ulifanyika Oktoba 30, 2017, Rais JPM akiwa Mwanza, alitoa kauli kwamba mafisadi wanakimbia CCM na kuhamia Chadema. Kauli hii kama zilivyo nyingine, inaibua tafsiri pana na kwa hiyo ina hadhi ya kufanyiwa mjadala wa kina.

Mshangao?

Kauli ya JPM ina maana nyingi sana. Maana mojawapo ni kuwa vita ya kupambana na ufisadi imeshatushinda kama taifa na kuwa Serikali na CCM imeshindwa kupambana na mafisadi waliojazana CCM. Huu ni mwaka wa pili JPM yuko madarakani, Serikali yake inapaswa ieleze ni kwa namna gani imepambana na mafisadi walioko ndani na nje ya CCM. Tunaposema kupambana na ufisadi hatusemi iwe mwanya wa kuwaonea watu, hapana! Tunazungumzia kupambana na mafisadi kweli kweli, wawe wapo CCM, Chadema, CUF na kwingineko.

Dhana ya kupambana na ufisadi inapaswa kufanywa na vyombo huru na vyombo huru havipo. Mathalani tunayo Takukuru, lakini haiwezi kuwachukulia hatua vigogo wakubwa waliowahi kujihusisha na ufisadi bila kujua Rais wa nchi anataka nini.

Tanzania haijawa na mfumo wa kitaasisi ambao unaruhusu mahakama na bunge vijitegemee na vifanye maamuzi yake bila kuionea aibu Serikali. Ukiwa katika nchi ambayo bunge na mahakama vimefinywangwa kikatiba na madaraka yake kwa kiasi kikubwa yanategemea Serikali inataka nini, taasisi za kawaida kama vile Takukuru haziwezi kupambana na mambo makubwa kwenye rushwa na ufisadi. Vivyo hivyo, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jeshi la Polisi na zinginezo –haviwezi kufanya kazi zake kwa weledi na kwa kujitegemea.

Je, ndani ya CCM bado wamo mafisadi?

Kauli ya JPM kuwa mafisadi wanakimbilia Chadema inamaanisha kuwa Tanzania haina vyombo huru vya kupambana na mafisadi. Rais anaposema mafisadi wanatoka CCM na kukimbilia Chadema ana maana kuwa huko CCM mafisadi wamejazana na hawana mtu wa kuwachukulia hatua na kwamba kimbilio lao ni chama kingine?

Na je, kauli hiyo ina maana kuwa vyombo vya kupambana na mafisadi au vimeshindwa kazi yake, au vinamsikilizia atoe amri ya “kamata yule mwache huyu?” Ndiyo maana miaka miwili ya JPM imekuwa na mafanikio walau katika kuziba sehemu ndogo ya mianya ya rushwa, lakini zoezi hilo si endelevu kwa sababu linamtegemea zaidi yeye binafsi kuliko taasisi.

Taasisi za Serikali haziwezi kupambana na mafisadi bila kujua Rais anataka nini, maana kama mafisadi wamo CCM na baadhi yao wanakimbia kwenda nje ya CCM ina maana (tafsiri yangu) kwamba wengine Rais anawafahamu, wengine ni marafiki zake, wengine ni wanachama wake na wengine ni viongozi wenzake.

Katika hali ya namna hiyo lazima vyombo vya kupambana na ufisadi vimuachie kazi hiyo Rais peke yake ili visije kukosea, maana kwa mamlaka makubwa ya rais wa Tanzania kikatiba, unaweza kumhoji mtu fulani kwa tuhuma za ufisadi, au ukamkamata fulani ndani ya CCM, ukajipata matatani, maana unayemkamata anaweza kuwa na ukaribu na rais na tena ikawa rais hakuwa anataka akamatwe. Au unayemkamata anaweza kuwa mtu muhimu kwa uteuzi ujao wa Rais na kwa hiyo ukamwondolea Rais uhuru wa kuteua watu anaowataka.

Mifano halisi ya mapambano ya ufisadi

Tujifunze ili tuwe taifa la watu wanaokubali makosa yao. Mapambano ya kweli ya ufisadi huwa hayaangalii nani alifanya ufisadi, yanaangalia sheria inasema nini.

Nchi zinazopambana na ufisadi hazichagui mtu, cheo chake, chama chake n.k. kama kuna viongozi wastaafu – marais, Makamu wa Rais, mawaziri wakuu, mawaziri, majaji wakuu, maspika wa bunge, wabunge, wakuu wa majeshi na wanajeshi waandamizi, wakuu wa polisi, magereza, JKT na maofisa waandamizi wa majeshi na wana tuhuma za rushwa na ufisadi, hakuna kinga, huhojiwa na kufikishwa mahakamani. Hatua hiyo ya kumkata kila mtu ndiyo inafanya vita yetu dhidi ya ufisadi inapotushinda.

Hakuna sheria inayotoa kinga kwa rais wa nchi kutenda makosa ya wizi na ufisadi au kuhujumu uchumi wa nchi. Haipo sheria inayomkinga Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Waziri, Jaji Mkuu, Spika wa Bunge, Majaji, Wabunge, Viongozi wa vyombo vya usalama wala wakuu wa mashirika na taasisi za umma na binafsi. Sote tuko chini ya sheria moja na kama sheria ni msumeno hebu ifanye kazi yake.

Kisa cha Mahalu na Rais Mkapa

Itakuwa ni kujidanganya eti tunapambana na ufisadi kwa kuweka tahadhari eti watu wanapokuwa CCM hatusemi ni mafisadi, ila wakiondoka tunasema ni mafisadi. Kauli za namna hii zinamaanisha kuwa vita dhidi ya ufisadi imeshatushinda na imetushinda kwa sababu mnyororo wa ufisadi nchi hii ni mrefu mno. Balozi Costa Mahalu aliwahi kushtakiwa mahakamani enzi za Rais JK,  akituhumiwa kufanya ubadhirifu mkubwa katika ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia.

Wakati Mahalu akitizamwa kama mtuhumiwa mkubwa wa “ufisadi” na “mtumiaji mbaya wa madaraka” kesi ile ikaushangaza umma pale Rais Mkapa alipopanda kizimbani na kutoa ushahidi kuwa yeye Mkapa alikuwa Rais wakati jengo hilo linanunuliwa na kwamba hakukuwa na ubadhirifu wowote kwani alijiridhisha kuwa lilinunuliwa kwa akufuata taratibu zote na kwa gharama iliyopitishwa na Serikali ya Tanzania na kuwa Mahalu hakulifanya jambo hilo bila kuishirikisha Serikali. Wakati mahakama za jamii (za mitaani) zinamhukumu balozi Mahalu kwa kashfa ile bila kujua ukweli halisi, mahakama ikaja kupewa ukweli tofauti na Mahalu akarejesha heshima yake.

Kwa lugha nyingine, kama Mahalu angelikuwa anazama, angelizama na Rais Mkapa. Hata kama Mkapa asingepelekwa gerezani kama Mahalu (ikiwa Mahalu angelikutwa na hatia) heshima ya Mkapa ingelishuka zaidi, kwani angelituhumiwa kwa ushahidi kuwa wakati wa uongozi wake hakuchukua hatua dhidi ya ubadhirifu.

Tunashughulikia mafisadi wakishaondoka CCM?

Hawa watu ambao leo wanakimbilia upinzani halafu Serikali na CCM vinawaita mafisadi, ni watu ambao hata zilipotolewa tuhuma zao wakati hawajahama, CCM iliwalinda na hatukuwahi kuona vijana wa CCM wala viongozi wa CCM wakijitokeza hadharani na kusema kweli mtu fulani ni fisadi, waliwalinda na kuficha ukweli wowote.

Wako wana CCM walioshiriki kwenye kashfa  kubwa kama  Escrow, Ununuzi wa Rada, Ndege ya Rais, IPTL na nyinginezo; hadi leo wana CCM hao wamo CCM, wengine ni wabunge, mawaziri, wakuu wa taasisi za umma na viongozi wakubwa wa Serikali, bunge na CCM. CCM haiwachukulii hatua kwa sababu ya kuogopa kuparaganyika au kujiparaganya.

Watu hawa wakishahama CCM ndipo inasemwa walikuwa ni mafisadi. Hii ni dalili tosha kuwa CCM haina meno ya kuwauma mafisadi, inakaa nao huko ndani hadi waondokapo. Na unaweza kujiuliza, hao wanaoitwa mafisadi kwa sababu wameondoka CCM, wanapoondoka CCM wanakimbilia Ulaya? Mbona wapo hapa hapa Tanzania.

Ukweli ni kuwa tunashindwa kuwachukulia hatua wakiwa ndani ya CCM kwa sababu mambo mengi ambayo wanatuhumiwa kuyafanya na umma unayatafsiri kama ufisadi, ni mambo ambayo ikiwa wataguswa nayo, watawataja mpaka wakubwa wao ambao ni baadhi ya viongozi wakubwa wastaafu wa ngazi mbalimbali. Tukifika hapo tunahofia kuwa CCM itapasuka vipande vipande na ndipo tunakaa kimya na vita ya ufisadi inakufa.

Serikali itaje orodha ya mafisadi

Kama kauli ya Rais ni dhahiri, kuwa mafisadi wanaikimbia CCM na kwenda Chadema, nimekaa na kujiuliza kuwa hadi sasa ikulu ina orodha ya mafisadi wangapi waliokimbia na wangapi wamebakia CCM? Na kwa sababu Rais wetu ni msema kweli na mpenzi wa Mungu, ni lini atatoa hadharani orodha ya mafisadi waliokimbilia Chadema na wale waliobakia CCM ili umma uwatambue?

Tunapogeuza vita dhidi ya ufisadi kuwa michezo ya kisiasa au njia ya kuwachapia wale wanaoondoka CCM, tunakuwa tumepoteza mwelekeo na vita yenyewe. Kama tunapambana na ufisadi hebu tuifanye vita hiyo bila kuangalia cheo cha mtu, chama chake, kabila lake, dini yake, kipato chake n.k. Tuyafanye mapambano dhidi ya ufisadi kuwa vita ya kufa au kupona na vita inayopiganwa na taifa zima kwa njia za wazi na shirikishi kwa kila mtu.

(Julius Mtatiro ni Mchambuzi na Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtafiti, Mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF). Simu; +255787536759 (Whatsup, Meseji na Kupiga)/ Barua Pepe; juliusmtatiro@yahoo.com)