Home Habari kuu Magavana Kenya wanaomaliza muda wajipanga kurudi uongozini

Magavana Kenya wanaomaliza muda wajipanga kurudi uongozini

375
0
SHARE

Isiji Dominic

KATIBA ya Kenya iliyopitishwa mwaka 2010, ilibuni nyadhifa za magavana ambao jukumu lao litakuwa kuongoza kaunti hivyo kuondokana na mikoa ambapo awali kulikuwa na mikoa nane zikisimamiwa na wakuu wa mikoa walioteuliwa na rais.

Katiba mpya iliyopitishwa baada ya machafuko ya kisiasa yaliyotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007/08, kaunti 47 zilibuniwa zikiongozwa na magavana ambao hupigiwa kura na wananchi kila unapofanyika uchaguzi mkuu.

Endapo gavana atafariki dunia au kuondolewa na wajumbe wa baraza la kaunti na kuidhinishwa na Bunge la Seneti na Mahakama au akapatikana na makosa ya jinai, naibu gavana ataapishwa na kuendelea na majukumu ya kuongoza kaunti.

Aidha kwa mujibu wa Katiba mpya, gavana ataruhusiwa kukaa madarakani kwa mihula miwili ya miaka 10 kama ilivyo rais na hataruhusiwa kugombea nafasi hiyo tena. Hivyo kama atataka kusalia uongozini, atalazimika kugombea nafasi nyingine kama vile urais, ubunge au mjumbe wa baraza la kaunti.

Ukizingatia nafasi ya ugavana ni ya juu kiutawala na kimamlaka, nafasi yenye hadhi inayotajwa kwa gavana aliyemaliza muda wake wa mihula miwili ni urais au naibu urais.

Magavana ambao wanamaliza muda wao tayari wameshaanza kujipanga mwaka 2022, ambapo Kenya inatarajiwa kuingia kwenye uchaguzi mkuu kumchagua rais wa awamu ya tano atakayemrithi Uhuru Kenyatta.

Mwishoni mwa mwaka jana, takribani magavana 15 walikutana jijini Nairobi na inadaiwa walijadili ni mgombea gani kumuunga mkono mwaka 2022 au kuunda chama chao na kumteua moja wao kuwa mgombea.

Tayari, Gavana wa Muranga, Mwangi wa Iria, amesajili chama kipya ambayo anadhamiria kuitumia kujiendeleza kisiasa baada ya 2022. Magavana wengine ambao wameonyesha nia ya kumrithi Rais Uhuru ni Hassan Joho (Mombasa), Amason Kingi (Kilifi) na Wycliffe Oparanya (Kakamega).

Katika taarifa yake, Joho alisema hataki kuona maisha yake ya kisiasa yakiishia kwenye ugavana hivyo anaangalia uwezekano wa kuwania urais mwaka 2022.

Haishangazi kuona magavana wanaohudumu muhula wao wa pili na wa mwisho wakipendekeza kwenye ripoti ya jopo kazi ya Building Bridges Initiative (BBI), wakiunga mkono serikali ya majimbo itakayomaanisha serikali kuwa na ngazi tatu; ya kitaifa, kaunti na majimbo.

Takribani magavana 22 kikatiba hawataruhusiwa kuwania nafasi zao tena na uwezekano wa mabadiliko ya Katiba unawapa fursa kuikumbatia serikali ya majimbo ambayo itawawezesha kuwa na nyadifa ya juu kiuongozi.

Ukizingatia sio magavana wote wanaomaliza muhula wao wa pili wana ushawishi kisiasa kuwania urais 2022, tayari wameshapiga darubini kusimamia mabilioni yaliyopo chini ya serikali za kaunti kupitia serikali ya majimbo.

Baadhi ya magavana hawa wanaamini BBI inaweza kuwapa mwanya kuendelea kubaki kwenye siasa endapo itatoa pendekezo ya ama nafasi nyingine za kuchagulia au uteuzi.