Home Makala Magonjwa yasiyoambukiza janga jipya linaloitafuna dunia

Magonjwa yasiyoambukiza janga jipya linaloitafuna dunia

325
0
SHARE
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Faustine Ndugulile

Na MWANDISHI WETU

MAGONJWA yasiyoambukizwa (NCDs) ni janga lililogeuka tishio ulimwenguni kote kwa sasa tofauti na miaka ya nyuma, ambapo magonjwa ya kuambukizwa hasa yale ya ngono ndio yalikuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya afya ya jamii.

Mbali na kuwa ni tishio kwa dunia nzima lakini imeonekana kama kikwazo kilichokuja kurudisha nyuma mikakati ya maendeleo ya kiuchumi kwa nchi zinazoendelea na zile za uchumi wa kati kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu wasio na uelewa dhidi ya magonjwa haya.

Magonjwa haya yanatajwa kuchagiza tatizo la umasikini hasa kwa nchi za dunia ya tatu kutokana na kugharimu nguvu kazi, kufuta matumaini ya uwajibikaji kwa waathirika pamoja na kuwafanya watu kutumia gharama kubwa za matibabu katika kipindi kikubwa cha maisha yao pasipo mafanikio.

Ninapozungumzia magonjwa yaliyo kwenye kundi la NCDs hapa najumuisha magonjwa kama kisukari, kansa, matatizo ya afya ya akili, magonjwa ya mfumo wa upumuaji pamoja na mfumo wa mishipa na damu.

Kwa mujibu wa ripoti ya mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa Septemba 27 mwaka 2018 jijini New York nchini Marekani, ilibainika kuwa watu 7 kati ya 10 duniani hufa kwa magonjwa ya moyo, kansa, kisukari na magonjwa ya mapafu.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa hadi mwaka jana, magonjwa yasiyoambukizwa yamekuwa yakichangia asilimia 71 ya vifo vyote duniani sawa na wastani wa vifo vya watu milioni 41 kila mwaka kote ulimwenguni.

Ambapo inakadiriwa kutokana na athari za NCDs wastani wa watu milioni 15 wapo hatarini kukatisha maisha yao kila mwaka huku takribani waathirika 800,000 wakitajwa kujinyonga kwa mwaka kutokana na changamoto za afya ya akili na msongo wa mawazo.

Takwimu hizo zinabainisha kuwa athari ya magonjwa yasiyoambukizwa inazidi kuwa kubwa zaidi hasa kwa watu wa umri kati ya miaka 30-70, ambapo inaelezwa kila baada ya sekunde mbili mtu mmoja wa kati ya umri huo hufa kwa NCDs.

Wakati ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2010 ikionyesha kuwa asilimia 47 ya watu 100 hufariki kutokana na magonjwa hayo, dunia inatarajia vifo 60  kati ya 100 vitatokana na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kuanzia mwaka 2020.

Pia ripoti hiyo inaonyesha endapo hatua mahususi hazitachukuliwa za kupambana na kudhibiti magonjwa hayo, hadi mwaka 2020 takwimu zitapanda kutoka waathirika wa NCDs asilimia 47 mpaka asilimia 60 ya waathirika wa NCDS na vifo vitapanda kutoka asilimia 60 mpaka asilimia 73.

Mbali na kuwepo kwa sababu nyingi zinazotajwa kuongeza tatizo na athari za NCDs lakini sababu kuu tano ambazo ni ulaji mbaya, madhara ya tumbaku, uchafuzi wa hewa, utumiaji wa pombe kali pamoja kutofanya mazoezi ndio zinaonekana kuwa chanzo kikubwa cha magonjwa haya.

Ili kupunguza athari za magonjwa yasiyoambukizwa kwenye jamii baraza la umoja wa mataifa lilikuja na baadhi ya maadhimio yanayoweza kuwa na msaada mkubwa katika kupunguza tatizo hilo.

Maadhimio hayo yanalenga zaidi katika kuhamasisha serikali zote ulimwenguni kuzingatia utoaji wa huduma bora za jamii, uwekaji mazingira rafiki ya upatikanaji wa huduma za kijamii pamoja kuchukua juhudi za makusudi kuzuia athari za kiafya zinazotokana na shughuli za kiuchumi.

Pia tahadhari kwa mtu mmoja mmoja ziliwekewa mkazo ikiwemo kuzingatia ushauri wa kiafya, kufanya mazoezi, kuongeza uwekezaji wa chanjo na kinga pamoja na wazazi kutoa kipaumbele cha unyonyeshaji wa vichanga badala ya kutumia vyakula vya viwandani.

Maadhimio hayo ya kupiga vita janga la magonjwa yasiyoambukizwa yanalenga kuokoa nguvu kazi, gharama za maisha na kufufua matumaini ya kizazi kijacho.

Ajenda ya maadhimio hayo ilikuja kwa kutambua kuwa sekta takribani zote  ikiwemo viwanda, usafirishaji, kilimo, biashara, ufugaji na mazingira kila moja kwa nafasi yake inapelekea kwa namna moja au nyingine visababishi vya magonjwa haya kwa binadamu.  

Taarifa zinaeleza, iwapo hatua zitachukuliwa dunia itaweza kuokoa maisha ya wastani wa watu milioni 8.2 kutoka nchi masikini na kuweza kuchangia zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 350 ifikapo mwaka 2030 ambapo kila dola moja inayowekezwa kupambana na NCDs itaweza kuzalisha dola saba mwaka 2030.

Hata hivyo nchini Tanzania, taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) imekuwa ikifanya kazi na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika tafiti za uchunguzi ambazo zimeonyesha kuwa kasi ya kukua kwa magonjwa yasiyoambukiza ipo juu.

Ongezeko la wagonjwa wa saratani ni moja ya tishio kubwa hapa nchini huku asilimia 50 ya wagonjwa wote wa saratani wanaotibiwa katika taasisi ya taifa ya saratani Ocean Road Dar es Salaam  wakitajwa kutokea mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa maana ya Mwanza, Kagera, Shinyanga, Mara, Simiyu na Geita.

Takwimu ambazo zilimgusa Rais na kuamua kuiagiza NIMR  kufanya utafiti kwanini mikoa ya Kanda ya Ziwa inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa saratani nchini.

Februari 4 mwaka 2019 wakati dunia ikiadhimisha siku ya saratani duniani, WHO ilitoa takwimu ambazo zilifafanua kuwa mwaka 2018 kulikuwa na jumla ya kesi mpya za saratani milioni 18.1 huku miongoni mwao watu milioni 9.6 wakipoteza maisha.

Takwimu hizo pia zilionyesha kwamba asilimia 70 ya wagonjwa wa saratani waliopoteza maisha kwa ugonjwa huo wanatoka nchi masikini huku hatari kubwa kabisa ya kupata saratani ikiwa inawakabili wavutaji sigara na wanywaji wa pombe.

WHO linakadiria kuwa kufikia mwaka 2035 idadi ya wagonjwa wa kisukari duniani itafikia watu milioni 592 na Tanzania itakuwa na wagonjwa zaidi ya milioni 3.

Ulaji usiofaa umetajwa kuwa tatizo kubwa kwa mujibu wa tafiti ambapo asilimia 97 ya Watanzania waliohojiwa iwapo wanakula mbogamboga na matunda zaidi ya mara tano kwa siku, asilimia 2.5 tu ndiyo walisema wanakula wengi hawali.

Kwa ujumla sababu nyingi za ongezeko la magonjwa haya zinagusia mfumo mbaya wa maisha sambamba na maendeleo ya teknolojia ya mionzi, viwanda na ongezeko la matumizi ya programu zinazopatikana kwenye simu janja na tarakilishi.

Japo elimu inaendelea kutolewa kila uchwao kuihamasisha jamii kubadili mfumo wa maisha ili kuepuka kujiweka katika mazingira hatarishi yanayochagiza ongezeko la NCDs lakini bado changamoto ni kubwa hasa kwenye nchi za kusini mwa jangwa la sahara Tanzania ikiwa mojawapo.

0768864097, shida.yohana@gmail.com