Home Makala Magonjwa yasiyoambukizwa hatari kwa Tanzania

Magonjwa yasiyoambukizwa hatari kwa Tanzania

967
0
SHARE

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WATAALAMU wa afya duniani wanaonya kuwa juhudi za makusudi zinahitajika kupambana na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza (NCD’s) kwani yanazidi kugharimu maisha ya watu wengi.

Wanasema magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza yanazidi kuwa tishio duniani katika miaka ya sasa, tofauti na miaka ya nyuma ambapo yale ya kuambukiza ndiyo yalikuwa tishio. Magonjwa hayo ni pamoja na yale ya moyo, kisukari, saratani na mengineyo.

Wataalam hao wanaeleza kuwa, vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo ndivyo ambavyo huchukua sehemu kubwa ya vifo vyote vinavyosababishwa na magonjwa yasiyoambukiza (Non Communicable Disease) duniani kwa asilimia 31 ya vifo vyote duniani.

Inakadiriwa kuwa magonjwa ya moyo husababisha vifo vya takriban watu milioni 17.3 wa rika mbalimbali kila mwaka duniani kote. Wataalamu wanaonya kwamba idadi hiyo huenda itaongezeka hadi kufikia watu milioni 25 ifikapo mwaka 2030, iwapo jamii haitachukua hatua za kukabiliana na magonjwa hayo.

Nchi zenye uchumi wa chini na kati, ikiwamo Tanzania ndizo zinazotajwa kuwa katika hatari zaidi ya wananchi wake kupata maradhi haya ikilinganishwa na nchi zilizo na uchumi wa juu. Katika mtandao wake, Shirika la Afya Duniani (WHO), linaeleza kuwa magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza husababisha vifo vya takribani watu milioni 38 kila mwaka duniani.

Kwa mujibu wa mtandao huo, karibu robo tatu ya vifo hivyo ambayo ni sawa na milioni 28, hutokea katika nchi zenye kipato cha kati na chini, ikiwamo Tanzania. Mtandao huo unafafanua kuwa vifo milioni 16 sawa na asilimia 82 hutokea mapema kabla ya umri wa miaka 70 katika nchi hizo.

Kwa msingi huo, magonjwa ya moyo yanatajwa kuwa sugu kutokana na kusababisha vifo vya idadi kubwa ya watu huku kundi kubwa linalotajwa katika hatari ya kupata magonjwa hayo ni lile la vijana na watoto. Awali, nguvu kubwa ya serikali na mataifa mbalimbali makubwa duniani iliwekezwa katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza lakini sasa zimeanza kujipanga kupambana na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza.

Hali ipoje nchini

Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Profesa Mohamed Janabi anasema watanzania wengi wanatembea wakiwa hawajijui afya zao.

“Wengi hawana mwamko wa kupima afya, matokeo yake hufikishwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya, JKCI mwaka 2012 tulifanya utafiti na kugundua kwamba robo tatu ya watanzania wanaugua magonjwa ya moyo.

“Kama nilivyosema awali wengi hawakuwa wanajua hadi tulipowapatia majibu yao ambapo walionesha hali ya kushangazwa, tulikuta asilimia 30 ya watu waliopimwa walikuwa wakisumbuliwa na shinikizo la damu, asilimia 26 walikuwa wana mafuta mengi mwilini na 26 wengine walikutwa na uzito uliokithiri, viashiria ambavyo vinatajwa kuwa ni mojawapo ya vichocheo vinavyosababisha magonjwa ya moyo,” anasema.

Anasema utafiti mwingine walioufanya kwa wilaya ya Kinondoni pekee hivi karibuni, waligundua zaidi ya asilimia 50 ya wakazi wa eneo hilo wanasumbuliwa na magonjwa ya moyo ikiwamo shinikizo la damu na hawajijui.

 Historia ya JKCI

Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Profesa Mohamed Janabi anasema walianza kufanya upasuaji mwaka 2008 hadi 2014 wakitumia chumba cha upasuaji na ICU ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI).

“Katika kipindi hicho cha miaka saba tulifanikiwa kufanya upasuaji kwa wagonjwa wastani wa 50 kila mwaka. Hivyo kwa kipindi cha kuanzia 2008-2014 tuliweza kuwafanyia upasuaji jumla ya wagonjwa 350.

“Wagonjwa wengine 250 walisafirishwa kwenda India kwa mwaka.   Gharama ya mgonjwa mmoja wa moyo kumpeleka India pamoja na msindikizaji wastani ni millioni 29 (gharama za upasuaji, ticketi na posho),”anasema.

Anasema ilipofika Septemba 5, mwaka 2015 ndipo serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Dk. Jakaya Kikwete ilipoanzisha rasmi taasisi hiyo ya JKCI.

“Tangu kuanzishwa kwa taasisi hii idadi ya wagonjwa tunaowaona imeongezeka, kwa mfano mwaka 2015 tuliona wagonjwa wapatao 54,000. Kwa mwaka huu (2016) toka Januari hadi Septemba idadi imeongezeka na kufikia wagonjwa 91,000 ambao tumewaona na kuwapatia huduma,” anasema.

Wagonjwa wengi ni watoto.

Profesa Janabi anasema ingawa wameweza kuwahudumia wagonjwa wengi lakini jambo linalowasikitisha ni kuona kwamba idadi kubwa ni watoto wadogo.

“Watoto wadogo wanachukua asilimia 85 ya wagonjwa wote tuliowahi kwa tuliowafanyia upasuaji, wengi wanazaliwa na matatizo ya tundu kwenye moyo, mishipa kuziba. Zaidi ya 10,000 huzaliwa na tatizo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi hiyo, Sulende Kubhoja anasema kila mwaka watoto zaidi ya 10,000 nchini huzaliwa kila mwaka wakiwa na ugonjwa wa moyo. Anasema hata hivyo wazazi wengi hushindwa kubaini mapema iwapo watoto wao wanasumbuliwa na magonjwa hayo na hivyo hucheleweshwa kufikishwa hospitalini kupatiwa matibabu.

Dk. Kubhoja anasema tatizo hilo ni kubwa na kwamba kwa siku katika kliniki wanapokea watoto zaidi 30 na kuendelea kuwafanyia uchunguzi na matibabu.

“Duniani inakadiriwa kuwa watoto wanane kati ya 1000 wanaozaliwa kila mwaka huwa na maradhi hayo. Hapa JKCI wapo ambao baada ya uchunguzi huwa tunawakuta na  tundu kwenye moyo, wengi tumewafanyia upasuaji kwa njia ya kisasa ya kuziba tundu pasipo kufungua kifua,” anasema. Anasema pamoja na JKCI hospitali nyingine zinazofanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo ni Bugango, Mwanza, KCMC iliyopo Kilimanjaro

“Tunatarajia pia kuanza kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo mkoani Dodoma kuanzia 2017.

“Lakini uchunguzi wa awali kabla ya mama kubeba ujauzito ni wa muhimu, hasa katika kipindi cha miezi ya kwanza ya ujauzito wake kwani tatizo linapogundulika mapema huwa ni rahisi kutibika kuliko akikaa muda mrefu,” anasema.

Nini husababisha magonjwa ya moyo Profesa Janabi anasema mfumo wa sasa wa ulaji wa vyakula si mzuri ndiyo maana watu wengi wanapatwa na tatizo la magonjwa ya moyo hasa kwa watu wazima.

“Ulaji mbovu kama vile mafuta mengi kwenye chakula, ulaji wa chumvi nyingi, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe na uzito uliokithiri ni kati ya mambo ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa mtu kupata tatizo hili, watu kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara, kina mama kutopata chanjo zote kipindi cha ujauzito,” anasema.

Anasema hata hivyo yapo magonjwa mbalimbali yanayoweza kupelekea mtu kupata ugonjwa huo kama vile kisukari na shinikizo la damu ambayo wakati mwingine huwa yanarithiwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.