Home Habari kuu ‘Magufuli ana hasira’

‘Magufuli ana hasira’

2084
0
SHARE

MAGUFULI1NA GABRIEL MUSHI

UAMUZI wa Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela, umetajwa kuwa ni wa kibabe uliotawaliwa na hasira.

Mwanzoni mwa wiki hii, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Kilango na Katibu Tawala wa mkoa huo  Abdul Dachi kwa kile alichokiita taarifa zisizo sahihi za wafanyakazi hewa katika mkoa wake.

Alitoa agizo hilo Machi 15, mwaka huu siku ambayo aliitumia pia kuwaapisha wakuu hao wa Mikoa.

Rais Magufuli aliwapa siku 15 kuhakikisha wanabaini idadi ya  wafanyakazi hewa kwenye mikoa yao.

Kilango akiwa Mkuu wa mkoa wa Shinyanga aliwasilisha taarifa ya kutokuwa na wafanyakazi hewa kwenye mkoa wake ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa agizo hilo.

Wakati Mkuu wa Mkoa akitoa taarifa hiyo, kikosi kazi cha Ikulu kilitumwa kufanya uchunguzi na kubaini kuwapo wafanyakazi hewa 45, hiyo ikiwa ni awamu ya kwanza ya uchunguzi  ambao ulionesha wafanyakazi hao wameigharimu serikali kiasi cha Sh. milioni 339.9.

Kutokana na uamuzi huo wa ghafla wa Rais, wasomi, wanasiasa na wachambuzi wa mambo wamesema baadhi ya maamuzi ya kiongozi huyo wa nchi yanatia shaka.

Kwamba ameanza kuonesha wazi kuwa ni kiongozi mwenye kutumia hasira na jazba katika kuamua baadhi ya mambo ya msingi.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala alisema katika uongozi kuna viongozi wa aina mbili.

Alisema aina ya kwanza ni ya kiongozi ambaye akielezwa jambo au kupewa ripoti anatulia na kuifanyia utafiti zaidi ndipo anachukua hatua, lakini aina ya pili ni ya kiongozi ambaye akielezwa jambo anachukua maamuzi papo hapo.

“Aina ya kiongozi wa pili ni ya mtu mwenye uamuzi wa hasira kwa sababu  anachukua maamuzi papohapo bila kutulia na kulifanyia upembuzi. Namuona Rais wetu yupo katika kundi hili.

“Ni kweli kuwa mkuu wa mkoa alistahili adhabu kutokana na kosa alilofanya kwa sababu  huwezi kukubali kirahisi taarifa ulizopewa, lakini adhabu hii ilikuwa ni kubwa sana kwa Kilango kwa kuwa lilikuwa ni kosa la kwanza,  alistahili kupewa  onyo kwanza.

“Niseme, Magufuli ana hasira au munkari,” alisema Profesa Mpangala.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, alisema maamuzi aliyotoa Rais Magufuli ni ya hasira kwa sababu maagizo aliyoyatoa kwa wakuu wa mikoa si madogo, yanahitaji uweledi zaidi.

“Nilishangaa kuona akitengua uteuzi huo kwa suala hilo kwa sababu watumishi hewa wapo wa aina nyingi na zipo taasisi za serikali ambazo zinatakiwa kufanyia kazi suala hilo kiuweledi, kwa mfano kuna wakaguzi wa watumishi na wengine.

“Inaonesha Magufuli anatoa maamuzi ya kisiasa kuliko kitaaluma,  kwa maana kila kitu anaona ni jipu basi hakuna majipu serikalini. Anatakiwa kuzingatia vigezo vya kiukaguzi na kutulia ili kuchukua hatua,  lakini kama anategemea kutuma timu zake za uchunguzi pekee basi nadhani hata hizo ripoti anazopewa zinaweza kuwa za uongo,” alisema Profesa Baregu.

Kwa upande wake  Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho, alisema ni uamuzi wa haraka, lakini Anne Kilango alistahili adhabu aliyopewa kwani alifanya maamuzi ya kukurupuka.

“Kwa upande wangu naona RC alikurupuka kwa sababu anajua kabisa suala la watumishi hewa ni tatizo, lakini alipopewa taarifa kuwa hakuna watumishi hewa  hakushtuka na kuuliza mara mbili.

“Sasa Magufuli alichokifanya ni sahihi kwa sababu Kilango amekuwa mfano kwa watumishi wengine kuwa sasa si kufanya kazi kwa mazoea, huu ni uongozi mwingine lazima kuchapa kazi,” alisema Profesa Shumbusho.

Aidha, kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo, Anna Mghwira alisema pande zote zina makosa katika maamuzi waliyoyafanya.

“Kwa Mama Kilango amefanya maamuzi ya haraka, kwani lazima atambue kuwa suala la watumishi hewa lipo tangu miaka mingi, hivyo kitendo cha kuambiwa hakuna watumishi hewa lazima ushtuke kidogo na ufanye uhakiki.

“Asingetakiwa kukubali kudanganyika kirahisirahisi kuwa kweli hakuna watumishi hewa.   Nchi hii ipo korongoni hivyo watumishi wetu wanatakiwa kuitoa hapa ilipo, wamsaidie Rais Magufuli kwani ana nia njema kabisa.

“Lakini kwa upande wake Rais Magufuli niseme kuwa ana hasira na maamuzi ya haraka vilevile kwa sababu ni ukweli kuwa Mama Kilango amefanya makosa,  lakini muda aliopewa ni mdogo ukilinganisha na suala lenyewe.

“Kiujumla RC alikuwa  hajahudhuria kikao cha Baraza la Halmashauri kwani alikaa muda mfupi tu hivyo ilikuwa ni rahisi kudanganywa, Rais angepaswa kutazama hilo na kiuongozi angempa adhabu ndogo kwa kuwa ni kosa la kwanza na si kuchukua maamuzi ya haraka namna hiyo,” alisema Mghwira.

HISTORIA

Kilichomkuta Kilango ni sawa na kile kilichowahi kumkumba mume wake John Malecela.

Malecela alivuliwa uwaziri wa Kilimo na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, baada ya kumpa taarifa zisizo sahihi za chakula nchini.

Uamuzi huo ulifikiwa mwaka 1974, ambapo Malecela alimwambia Mwalimu kuwa hali ya chakula nchini ni nzuri na hakuna tishio lolote la njaa.

Taarifa hiyo iliyomfanya Rais kutoa ruhusa ya chakula kuuzwa nje.

Katika hali ya kushangaza miezi mitatu baada ya chakula kuuzwa nje, hali ya chakula ilibadilika na kusababisha njaa kali.

Matokeo hayo yalimghadhibisha Mwalimu, ambaye alichukua uamuzi wa kutengua uteuzi wake wa uwaziri na kumpa kazi nyingine ya ukuu wa Mkoa wa Iringa.