Home Habari ‘MAGUFULI ANATUTISHA’

‘MAGUFULI ANATUTISHA’

1006
0
SHARE

GABRIEL MUSHI NA MANENO SELANYIKA


KAULI na matamko kadhaa yaliyopata kutolewa na Rais Dk. John Magufuli katika siku za hivi karibuni, yametajwa kuwa ni hatua ya kuwatisha wanasiasa wa upinzani, RAI linaripoti.

Hofu hiyo imeoneshwa na baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani na kuungwa mkono na baadhi ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa.

Mwenyekiti wa  Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ni miongoni mwa wanasiasa wa upinzani walioonesha hofu ya kutishwa na kauli kadhaa za Rais, hasa ile aliyoitoa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais Magufuli, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, anadaiwa kuwaonya wabunge wa chama hicho ambao wana ushirikiano na wabunge wa upinzani na kudai kuwa, wapo baadhi yao wamekuwa wakitoa siri za chama.

Anadaiwa kwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa, hafurahishwi na kitendo cha baadhi ya wabunge wake kugawa dakika zao kwa wabunge wa upinzani.

Kubwa zaidi ambalo limeonekana kuwashtua wapinzani ni hatua ya kuwaonya wabunge wa CCM, waliokuwa na mpango wa kwenda kumtembelea Lema alipokuwa mahabusi katika gereza la Kisongo, jijini Arusha.

Imeelezwa kuwa, Mwenyekiti huyo wa CCM alikiita kitendo hicho kuwa ni usaliti mkubwa kwa chama hicho na kwamba yeye ndiye aliyeamua vikao vya Bunge kutorushwa mubashara.

Akizungumzia maagizo hayo ya Mwenyekiti wa CCM kwa wabunge wake, Rungwe alisema, anaona hali inazidi kuwa mbaya katika uongozi wa awamu hii ya Tano, kwani Serikali iliyopo imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kutumia vitisho ili kufifisha ukuaji wa upinzani nchini kwa kutumia zaidi nguvu ya dola.

Katika mazungumzo yake ya ana kwa ana na RAI mapema wiki hii, Rungwe anasema hali ya utulivu na amani iliyopo nchini imetokana na mila pamoja na desturi iliyoenziwa tangu utawala wa ukoloni.

Anasema kwa kuwa Tanzania imekuwa na ongezeko kubwa la watu kutoka milioni 10 wakati wa uhuru hadi zaidi ya milioni 40 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, ni dhahiri kuwa, lazima pawepo na mabadiliko ya kiteknolojia na kisiasa.

Mwenyekiti huyo, ambaye aligombea nafasi ya urais mwaka 2015, anasema chama kilichofanikiwa kushika dola kinaendesha nchi kwa vitisho, kukatishana tamaa na kusahau kwamba, nchi imefikia hapa kwa nguvu na akili za kila Mtanzania.

“Kwa matatizo yanayowakabili wananchi wa Taifa hili kwa sasa, anayepaswa kutupiwa lawama ni CCM, kwa sababu wao ndio wametanguliza mbele maslahi binafsi na kuwasahau wananchi.

“Hali hii si nzuri hata kidogo, kwa sasa Serikali imekuwa ndio wafadhili wa chama kilichopo madarakani, mimi na wenzangu ambao ni vyama vya mageuzi hatuwezi kukubali hali hii, tutawapinga hadi watakapojitambua kwamba wanakiuka taratibu na kunyima haki za raia,” alisema.

Alisema hali iliyopo sasa kisiasa si shwari, kwa sababu Serikali inanyima watu uhuru, hasa baadhi ya viongozi huzuiwa kutoa maoni yao na kupaza sauti kwa umma, kitu ambacho kitaleta athari kubwa kwa wananchi hapo baadaye.

Rungwe amewataka viongozi wanaofukuzwa katika nafasi zao kwenye vyama vya siasa kutokata tama, kwa sababu ni haki yao kufanya mabadiliko kwa ajili ya wananchi wao na wasitishwe wala kuwekewa hofu miongoni mwao.

“Ni haki Kikatiba kutoa maoni yako na maoni hayajalishi yanaunga mkono au kupinga, sasa wenzetu ukienda against (kinyume) unaondolewa unaonekana ni msaliti. ‘This is not a crime’ (huu si uhalifu), hivi ndivyo Taifa linavyoendeshwa, ni lazima kuwepo na wanaopinga, si kila jambo utakalo wewe kila mtu alikubali,” anasema.

Kwa upande wake Lema, ameandika waraka kwa Rais na kumweleza kuwa, ameogopeshwa na kauli za Rais na kuhoji ni wapi Taifa linakwenda.

“Mh. Rais nimeogopa sana kwa kauli yako, je, Taifa linakwenda wapi, hivi ni kweli sisi wabunge ni maadui? Kama viongozi tutafakari utengano ni moja ya njia ya kuimarisha vyama vyetu, basi bila shaka tutakuwa tunalitendea Taifa ubaya.

“Dhambi hii ikikomaa, basi ni hakika kwamba lugha za udini, ukanda na ukabila hazitaacha kukomaa, ni muhimu sasa kujenga utamaduni wa kuhimiza mshikamano kwa kitaifa bila kujali itikadi kama kweli tunawapenda masikini na wanyonge….”alisema Lema.

Kwa upande wao wasomi, wanabainisha kuwa, kauli za Rais kama ni za kweli, zinawanyima uhuru wabunge wake pamoja na kutishia uhai wa siasa za upinzani nchini.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, ameliambia RAI kuwa, matamko aliyoyatoa Rais yanawanyima uhuru wabunge, jambo ambalo moja kwa moja linafifisha uhuru wa Bunge.

“Katika mihimili mitatu ya dola, Serikali, Bunge na Mahakama, haitakiwi mhimili mmoja uingilie mwingine… inatakiwa kila mmoja uwe huru kutumikia wananchi. Sasa matamshi aliyotoa najumuisha kuwa, mhimili wa Serikali kuingilia mhimili wa Bunge ambao ni kinyume cha Katiba na sheria kwa sababu wabunge wapo chini ya mhimili wa Bunge ambao una mchanganyiko wa chama tawala na upinzani, kwa pamoja wanastahili kuwa huru kuendesha mambo yao.

“Kuanza kuwatisha au kuwapa masharti jinsi ya kuzungumza ndani ya Bunge kwamba usimpe nafasi mbunge wa upinzani, kuingilia hilo au mbunge wa CCM kumtembelea mbunge wa upinzani gerezani kama mbunge mwenzake ni jambo la ajabu sana, yote aliyotamka ni kama kuwatisha wabunge wa CCM na hata wale wa upinzani kwa lengo la kuwaondolea uhuru, hii maana yake Bunge halipo huru kama mhimili wa dola, jambo ambalo katika misingi ya demokrasia na utawala bora ni tatizo kwa nchi na Taifa,” alisema.

Hoja hiyo ya Profesa Mpangala pia iliungwa mkono na Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Gerhe Kahangwa,  ambaye alisema mtazamo alio nao Rais Magufuli kwa upinzani ni mwendelezo wa mtazamo aliokuwa nao hata alipokuwa waziri serikalini.

Alisema Magufuli amekuwa miongoni mwa watu ambao wanaitazama CCM kama chama kitakachotawala milele,  kwamba upande mwingine hakuna kilicho cha maana, watu au mawazo ya maana.

“Mtazamo huu ameuendeleza hata kipindi hiki, lakini anayo maoni yake na wengine wanaweza kuliona tofauti, ila kwangu naona si mtazamo sahihi kwa sababu hivi vyama ni vyombo ambavyo tumeviunda sisi Watanzania, licha ya kuwa katika vyama tofauti Watanzania bado wanaunganishwa na mambo mengi, ikiwamo utu, kwani ni watu ambao wana mahusiano ya kindugu.

“Unaweza kuwa wa CCM na mwingine wa chama chochote, lakini ninyi ni ndugu… mmoja anaweza kupata matatizo mwenzie akamjulia hali na hawa wote kabla ya vyama ni ndugu, vyama vipo na vinaweza kutoweka, lakini Utanzania wetu utabaki kama ulivyo.

“Mfano, katika familia ya Mwalimu Nyerere kulitoka mwasisi wa chama, lakini mtoto wake alikuwa mbunge wa upinzani, hilo halikufarakanisha uhusiano wa baba na mwana na sidhani kama mmoja angepata shida mwenzie asingekwenda kumwona kama Mtanzania.

“Sidhani kama Mwenyekiti wa chama anaweza kuwa hospitalini halafu Mwenyekiti mwingine asiende kumuona au bungeni wanapojadili jambo kwa maslahi ya Taifa  mwenzie asimpe muda… huwa tunasema tusigombanie fito tunajenga nyumba moja,” alisema.

Alifafanua kuwa, vitisho hivyo ambavyo vinaonekana kulenga upinzani huwa vinasababisha watu kutoshirikiana hata kwenye sherehe kutokana na matamko yanayotolewa na viongozi waliopo kwenye mamlaka.

“Rais alipokuwa kwenye ziara Bukoba Mjini, Mbunge wa Chadema aliheshimu mamlaka kwa kuwa Rais ni mamlaka, hata alipokwenda Mtwara Mjini, mbunge wa jimbo hilo alimpa ushirikiano katika ukaguzi wa miradi hadi Rais akamtania kuwa huyu sura ni CUF lakini moyo ni CCM.

“Hivyo tumuombe Rais atuunganishe sisi Watanzania kuliko kutuwekea mipaka, mwasisi wa Taifa letu ndiko alikotujenga tuwe wamoja, kwa sababu tunatofautiana kwa dini, lakini haiwi sababu ya kuangaliana vibaya ndani ya familia. “Niwaombe wazee wa Taifa hili, Maaskofu, Kardinali na Masheikh wamuonye Rais, ajenge misingi ya umoja katika Taifa letu kuliko kujenga uhasama. Hata katika Wimbo wa Taifa tunamuomba Mungu adumishe uhuru na umoja, ni sala ya Taifa na neno umoja hilo lipo katika nembo ya Taifa na Rais aliapa kulinda Katiba, hivyo azingatie hilo,” alisema.

RUNGWE KUJIUNGA NA UKAWA

Katika kuhakikisha anapingana kwa vitendo na mwenendo wa baadhi ya viongozi wa juu wa Serikali, Rungwe alisema yuko tayari kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Alisema ameonesha nguvu kubwa ya kisiasa kwenye uchaguzi mkuu uliopita na kwamba anaamini akiunganisha nguvu ya pamoja na vyama vya Chadema kinachoongozwa na Freeman Mbowe, CUF na NCCR-Mageuzi kinachoongozwa na James Mbatia, wanaweza kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi.

“Chauma kipo tayari kuungana na  Ukawa, hivi karibuni kikao cha chama chetu kiliamua kupitisha makubaliano ya kuungana na Ukawa, hadi sasa tuna asilimia 99.9 ya kuungana na wenzetu.

“Sisi tulichelewa tu kutokana na sababu mbalimbali, mojawapo ni kwamba, chama bado kilikuwa hakijafahamika na kujiimarisha, lakini hadi sasa sisi ni sehemu ya Ukawa kwa sababu hata katika mchakato ulipoanza wakati wa Bunge la Katiba tuliwaunga mkono.

“Bado hatujachelewa, fikra zetu ni moja na umoja ni nguvu, kwa sababu tumeona mifano katika nchi za wenzetu kule Afrika Magharibi, hata nchi ya Jamhuri ya Watu wa Kongo waliungana na wamefanikiwa,” anasema Mwenyekiti huyo.