Home Habari Magufuli aombwa kutupia macho ardhi

Magufuli aombwa kutupia macho ardhi

1332
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI

JUMUIKO la Maliasili Tanzania (TNRF), limemwomba Rais John Magufuli kutia mkono katika mashamba aliyoyafutia hati kwa mujibu wa sheria baada ya wawekezaji na wamiliki wa mashamba hayo kushindwa kuyatumia ipasavyo.

Pia Jumuiko hilo limesema ipo haja ya mikataba mibovu ambayo ipo kwenye ardhi kufumuliwa kama ambavyo Rais Magufuli alivyofumua mikataba mibovu iliyoingiwa kwenye sekta ya madini.

Hatua hiyo imekuja baada ya TNRF kubaini kuwa asilimia kubwa ya mashamba hayo yaliyofutiwa hati hadi sasa hayajareshwa kwa wananchi au kuchukuliwa hatua nyingine kama inavyotakikana.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa jumuiko hilo, Zacharia Faustine wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mafunzo yaliyoandaliwa na TNRF kwa kushirikiana na Taasisi ya Tanzania Land Alliance (TALA), kwa lengo la kuwanoa waandishi namna ya kuripoti masuala ya ardhi na maliasili.

Alisema Jumuiko hilo na masharika mengine zaidi ya 18 wamekuwa wakishirikiana katika eneo la maliasili na hasa ardhi na wanaona kazi nzuri inayofanywa na Serikali katika kutafuta utatuzi wa migogoro ya ardhi.

“Ninatamani kuona Rais wetu anaagiza kuangaliwa upya mikataba ambayo imeingiwa katika ardhi na ile ambayo itaonekana hafai basi ifumuliwe kwa maslahi ya Watanzania wote,” alisema Faustine.

Aidha, alisema licha ya Rais Magufuli kutetea wanyonge na kufuta hati za mashamba hayo hadi sasa bado hayajawafikia wakulima.

“Tunashukuru nia na dhamira njema ya Rais wetu katika kuhakikisha baadhi ya mashamba yanarudishwa kwa wananchi wa maeneo husika baada ya Serikali kutangaza kuyarejesha. Hata hivyo wananchi hawajapewa mashamba hayo kwasababu mlolongo wa kisheria nao ni mrefu na ili mashamba hayo yakabidhiwe kwa wananchi kuna hatua za kisheria ambazo zinapaswa kuchukuliwa.

“Rais aweke mkono wake kwenye mashamba ambayo aliyafuta ili yawafikie wananchi, tumefuatilia yale mashamba yaliyofutiwa bado kuna mkinzano wa kisheria, tupo tayari kuungana naye kuhakikisha mashamba hayo yanawafikia wakulima,” alisema.

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na mmoja wa Maofisa utetezi katika masuala ya sheria za ardhi kutoka TNRF, Masalu Luhula ambaye alisema baadhi ya wawekezaji walichukua maeneo makubwa lakini baada ya kushindwa kuyaendeleza na Rais kuyafutia hati miliki,  kunatakiwa kuandaliwa utaratibu stahiki ili kuyarudisha kwa wananchi.

“Tuko tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha mashamba ambayo yametangazwa kuwa yamerudishwa kwa wananchi kweli yanawafikia ili yatumike kwa shughuli za maendeleo ya Taifa letu,” alisema Luhula.

Aidha, Ofisa Mawasiliano na utetezi kutoka TNRF, Sophia Masuka alitoa wito kwa waandishi wa habari kuandika habari za uchunguzi kwa kutafuta vyanzo sahihi kwa kuangalia maslahi mapana ya nchi ili kutokomeza migogoro ya ardhi nchini.


Naye mmoja wa watoa mada katika mafunzo hayo, Mary Ndaro ambaye pia ni Mratibu wa programu ya Ardhi Yetu (AYP) kutoka Care Tanzania alitoa rai kwa waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuelimsha jamii kuwa mwanamke anayo nafasi ya kumiliki kipande cha ardhi.

“Kuna sababu nyingi ambazo zinachangia wanawake wengi kutomiliki ardhi zikiwemo za masuala ya mila, desturi na tamaduni kwani wapo baadhi ya wanawake kutokana na tamaduni zao hata wakipewa ardhi wanakataa kwa madai kuwa ardhi inamilikiwa na wanaume,” alisema Ndaro.

Itakumbukwa kuwa Januari mwaka huu Serikali ilitangaza kufuta umiliki wa mashamba sita yenye ukubwa wa ekari 12,915 yaliyopo Korogwe mkoani Tanga.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula akiwa ziarani wilayani Korogwe alitangaza uamuzi wa Serikali wa kubadilisha mashamba sita kati ya 14 yanayomilikiwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises Limited (MeTL),
Hata hivyo, Ofisa mtendaji mkuu wa Mohamed Dewji ‘Mo’ alisema kuwa anamwachia Mungu suala hilo.

Aidha, Mei 18 mwaka huu akiwa kwenye ziara mkoani Morogoro, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema watapitia upya mashamba yote yaliyofutwa na Rais mkoani humo.

Alisema kuna mashamba yaliyofutwa na Rais maeneo mbalimbali lakini hayajawekewa utaratibu wa kutumiwa, hivyo kutoa fursa kwa wajanja kujigawia na mengine kuyauza bila kufuata utaratibu.

Waziri huyo alisema katika kuhakikisha mashamba yote yaliyofutwa mkoani humo umezuka mgogoro baina ya wananchi na wamiliki, hivyo Serikali imeamua kupeleka timu kuyahakiki.

Alisema timu hiyo inajumuisha kamishna wa ardhi, kaimu mkurugenzi upimaji na ramani, mthamini mkuu wa Serikali, kamishna msaidizi wa ardhi Kanda ya Kati na wataalamu kutoka idara za mipango miji wizarani.

 “Tutayapitia mashamba yote 15 yaliyofutwa na Rais kujua kilichomo ndani yake na timu ya uhakiki niliyokuja nayo itanilitea mapendekezo namna ya kuyatumia na mengine watapewa wanaostahili si kila mtu,” alisema.