Home Habari Magufuli awatisha Mawaziri

Magufuli awatisha Mawaziri

1517
0
SHARE

imageNA MWANDISHI WETU

KASI ya Rais John Magufuli na Waziri Mkuu wake Kassim Majaliwa katika kuagiza, kutekeleza na kusimamia mambo inatajwa kuwa mwiba mkali kwa mawaziri  walioteuliwa wiki iliyopita.

Tangu aingie Ikulu na baadaye kumteua Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wake, viongozi hao wameonekana kuwa makini katika utendaji wao wa kila siku, ambapo katika kipindi kifupi wameweza kuibua uoza mwingi kwenye baadhi ya Idara na Taasisi za Serikali.

Hatua hiyo yenye kujali zaidi masilahi ya Watanzania, inatajwa kuwasumbua mawaziri wengi, ambao wanalazimika kuiga mienendo ile ile ya wakubwa zao ili waonekane kuwa wanaendena na kasi ya Rais Magufuli.

Katika muda wa wiki moja wa kuteuliwa kwao, mawaziri wengi na manaibu wao wamekuwa wakihaha kuzunguka huku na kule ikiwa ni pamoja na kufanya ziara za kushtukiza kama alivyofanya Rais Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa.

Katika ziara hizo za kushtukiza wanazozifanya, mawaziri hao wamekuwa wakitoa maagizo na matamko mazito huku wakitaka kuonana na baadhi ya watendaji wa idara na taasisi zilizo chini ya wizara zao kwa maelekezo zaidi.

Baadhi ya mawaziri ambao wanapambana kukabiliana na kasi ya Rais Magufuli ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye ameahidi kuvilea vyombo vya habari.

Nape alisema hakuteuliwa kwa ajili ya kuvifungia vyombo vya habari, badala yake anaamini jukumu lake kama Waziri ni kushirikiana navyo katika kuliletea Taifa maendeleo.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa naye ni miongoni mwa mawaziri walioanza kazi nje ya ofisi zao kwa kutembelea mtambo wa maji wa Ruvu Chini na Ruvu juu.

Akiwa huko aliagiza Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco), kuhakikisha hadi kufikia Juni mwakani wananchi wengi zaidi wanapata maji kutoka idadi ya sasa ya watu 148,000 na kuwa watu milioni moja.

Mawaziri wengine walianza na kasi ya ziara za kushtukiza zenye lengo la kuuaminisha umma kuwa hawakuchaguliwa kwa makosa ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba ambaye alikuwa mkoani Morogoro kulikokuwa na mapigano ya wakulima na wafugaji.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, Selemani Jaffo alikuwa wilayani Bahi mkoani Dodoma, alitangaza vita kwa wakurugenzi wote wa mamlaka ya miji na mitaa watakaoshindwa kukusanya mapato kwenye maeneo yao.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Naibu wake Dk. Hamis Kigwangala wao walifanya ziara ya kushtukiza ndani ya Hospitali ya Amana, iliyopo Ilala, jijini Dar es Salaam.

Dk. Kigwangala alidai kuwa wameanza kutumbua majipu madogo na kwamba mtumishi yeyote aliye chini ya wizara yao kama anajiona hataweza kuendana na kasi yao ajiondoe mwenyewe.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alikuwa wizarani kwake, ambapo bila kuchelewa aliwataka Wakurugenzi na wakuu wa Idara ndani ya wizara yake kukitumia kipindi cha siku saba kuandaa mpango kazi wa mwaka ujao, pamoja na kutoa taarifa za fedha za mwaka uliopita.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ifikapo Januari 1, mwakani iwe imekamilisha mradi wa umeme wa gesi wa Kinyerezi 1.

Wachambuzi wa mambo wanaifananisha aina hiyo ya utendaji kazi na uoga unaowalazimisha mawaziri hao kufanya kitu ili kumridhisha mtu aliyewateua.