Home Habari Magufuli: Mnisamehe

Magufuli: Mnisamehe

1675
0
SHARE

*Wasomi wahamaki

NA MWANDISHI WETUKATIKA kuonesha kuwa anajali umuhimu na masilahi ya elimu nchini, Rais Dk. John Magufuli mwishoni mwa wiki iliyopita, aliwataka wasomi wamsamehe kutokana na hatua yake ya kuwateua kwa wingi viongozi na wahadhiri wao.

Akiwa ndani ya ukumbi wa mikutano wa Nkrumah, uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wakati wa mdahalo wa miaka mitatu ya uongozi wake, Rais alisema ameamua kuwateua wasomi wengi kwenye serikali yake kwa kuamini kuwa watamsaidia.

“Mnisamehe  sana kwa kuendelea kuteua viongozi wenu wengi kutoka kwenye vyuo vikuu. Hata jana (Oktoba 31, mwaka huu) nimemteua kule Ardhi, nateua sana, nateua hivyo kwa sababu nina amini angalau mtanisaidia vizuri.”

Katika maombi yake hayo pia Rais Magufuli aliomba vijana anaowateua wavumiliwe kwa baadhi ya matendo yao kwani damu zao zinachemka.

“Nimeteua sana vijana, inawezekana kuna makosa watakayokuwa wanayafanya ni kwa sababu ya kuchemka damu, naomba muwavumilie.”

Kwa upande wa wanawake alisema ameteua akina mama wengi, lakini anashangaa kusikia kila mwanamama anayemteua ni hawara yake.

“Nimeteua akina mama wengi, na siku hizi kila mwanamama unaemteua ni hawara yako na mimi nitaendelea kuwateua tu na saa nyingine wanaofanya hivi ni akina mama wenyewe, sijui wanataka niteue wanaume tu!” alihoji.

 

WASOMI WAHAMAKI

Baadhi ya wasomi wameonekana kushangazwa na utaratibu wa kuwaondoa wasomi wengi vyuoni na kuwahamishia ndani ya Serikali, hatua inayoweza kudhoofisha elimu ya juu nchini, lakini pia wanaamini kazi ya msomi ni kubuni na kupendekeza mambo ya msingi.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu, Agustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu alisema wasomi kazi yao kubwa ni kukosoa, kubuni na kupendekeza kwa kuwa hawajaandaliwa kutenda mara nyingi hushindwa kutekeleza majukumua yao ipasavyo.

Alisema uzoefu unaonesha kuwa mchango mkubwa wa wasomi ni katika kufikiri na kubuni mbinu zinazoweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za jamii.

“Pili kukosoa na kuchambua yale yanayoendelea ili kuona udhaifu upo wapi, ubora upo wapi na nini kifanyike. Kwa hiyo msomi ni mtu wa kukosoa na kushauri nini kifanyike,” alisema.

Alisema katika dhana ya utendaji hakuna uhakika iwapo wasomi wamejiandaa au wameandaliwa kutenda.

“Katika awamu zilizopita wasomi wamejikuta katika nafasi za kutenda na kuonesha dhahiri kuwa hawakujiandaa au hawakuandaliwa katika kutenda. Hivyo mara nyingi hukwama kiutendaji na hata ule uwezo wao walioandaliwa wa kukosoa, kuchambua na kubuni unapotea.

“Hilo ni tatizo kwa wasomi wenzangu, kwa sababu kama unakwenda mahala ambapo si kubuni na kukosoa… zaidi ni kutenda yale unayoagizwa, hujikuta katika wakati mgumu na tija yao haiwezi kuonekana vya kutosha kwani eneo la nguvu zao sio katika uteuzi.

“Ndio maana nilishawahi kusema kama siwezi kukosoa, kushauri na kubuni afadhali nisiteuliwe kwa sababu itakuwa ni vigumu kutumia uwezo niliojengewa kisomi ambao ni kukosoa, kuchambua, kupendekeza na kubuni ili kuboresha. Kila mara kwenye sera zetu kuna udhaifu na kazi ya msomi ni kuonesha ule udhaifu ili kuwasaidia wale watendaji,” alisema Profesa Baregu.

Hoja ya Profesa Baregu pia iliungwa mkono na Mhadhiri Mwandamizi Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abdul Sherif ambaye alisema msomi sifa yake kubwa anatakiwa kuwa huru.

Alisema msomi anatakiwa aweze kufikiria suala fulani kwa upana na kwa usomi wake achague lile lililokuwa la kweli na apendekeze.

“Sasa mtu kama huyo ukishamuweka serikalini umembadilisha sifa yake. Yaani anakuwa kama mashine kwa kupitia usomi wake, lakini sio kwa uwezo wake kiakili kutenda. Tumeona wengi walioteuliwa kutoka nje ya serikali walikuwa wanaheshimika kama wasomi, lakini walipokuja serikalini wameshindwa kufanya vizuri,” alisema.

Aidha, alisema licha ya kuwepo kwa wimbi hilo la wasomi kuteuliwa serikalini, teuzi hizo haziwezi kuathiri vyuo watokavyo wahadhiri hao kwani sasa wapo wasomi wengi.

“Ninavyoona ni kwamba wanateuliwa kwa sababu wasomi ni wengi na vyuo vikuu ni vingi, tofauti na zamani, hivyo kuwachagua wachache kwenda serikalini sidhani kama itaathiri. Tatizo ninaloona ni kwamba nini tofauti kati ya msomi wa chuo kikuu na mfanyakazi serikalini,” alisema.

Mdhahiri Mwandamizi wa UDSM, Dk. Benson Bana alitilia shaka utendaji wa wasomi pindi wanapoteuliwa na kushikishwa nyadhifa serikalini.

Alisema wimbi la teuzi hizo linaonesha sura mbili kwamba mamlaka ya uteuzi inayowateua ina imani kuwa wataziba pengo linaloonekana serikalini na pili Rais wa sasa anajaribu kuondoa dhana iliyozoleleka na kuweka fikra mpya.

“Sasa utatoa wapi watu kama sio vyuo vikuu? ila vyuo vikuu pia vinawahitaji sana hao wasomi, hivyo kinachoonekana wanaacha mapengo vyuoni na kwenda kuyaziba serikalini, lakini ni lazima tutambue kuwa  kuziba pengo la Mhadhiri si jambo la siku moja, linachukua muda.

“Vilevile sina hakika sana kama utendaji bora unatokana na mhadhiri kutoka chuo kwa sababu na wao wanakwenda kujifunza pia huko serikali, hii dhana kuwa vyuo vikuu vinakuwa na watendaji bora kuliko kwingine si sahihi kwa sababu unaweza kuwa Profesa lakini usijue kuandika stori, ila mwandishi mwenye uweledi vilevile anaweza kushika nyadhifa,” alisema.

Itakumbukwa kuwa Oktoba mwaka huu, hoja hii iliibuliwa na aliyekuwa Katibu wa Mwalimu Julius Nyerere, Samuel Kasori ambaye alishangazwa na tabia ya wasomi nchini kukimbilia katika siasa.

Akichangia mjadala katika mdahalo wa kumbukizi ya miaka 19 ya Tanzania bila Mwalimu Nyerere, Kasori alihoji kuna nini wanachokifuata kwenye siasa.

Alisema Nyerere angekuwa hai angekuwa akiwatazama wasomi hao na kuwahurumia kutokana na jinsi wanavyopenda kusifiwa ovyo, jambo alilodai kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa akilichukia.

Alisema baadhi ya wasomi Tanzania na Afrika wanawaangusha kwa kufurahia nafasi za kuteuliwa za kisiasa.

“Tujiulize tunaoingia kwenye vyama vya siasa kule tunakwenda kutafuta nini kwa ajili ya watu wetu. Baadhi ya wasomi mmekuwa ni watu wa kujikomba komba” alisema Kasori.

“Angalia Serikali ina maprofesa wengi wasomi wengi kwa nini walikubali nafasi hizo za kisiasa ili iweje au kutafuta nafasi za kuabudiwa”

Alisema kwa muda aliokaa na Mwalimu Nyerere alijifunza kuwa ili uwe kiongozi unahitaji msaada.

Alibainisha kuwa wasomi nchini wamekaa kimya kwa mambo mengi ikiwamo viwanda vilivyokuwepo wakati wa mwalimu Nyerere kufa.

“Mkienda huko kwenye nafasi mnazopewa mnakwenda kunyamazishwa, kuna wasomi wanatoka vyuoni haraka na kuingia kwenye siasa, Mwalimu hakuwa mtu wa kupenda kusifiwa sifiwa hovyo kama tunavyofanya siku hizi.” Alisema.

BAADHI YA WASOMI WALIOTEULIWA

 1. Mhahidhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Kitila Mkumbo aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
 2. Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam Prof. Paramagamba Kabudi (Waziri wa Katiba na Sheria)-.
 3. Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Bashiru Ali (Katibu Mkuu wa CCM)-
 4. Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) – Taaluma na Utafiti, Prof. Lazaro Busagala (Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki, TAEC).
 5. Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Kilimo – Sokoine (SUA), Prof. Damian Gabagambi (Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Taifa, NDC,)
 6. Dkt. Deodatus Michael Mutasiwa (Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma).
 7. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dkt. Ave Maria Semakafu (Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia)
 8. Dk. Aziz Mlima aliteuliwa Balozi Malaysia (aliwahi kuwa balozi katika nchi hiyo aliteuliwa na JK kuchukua nafasi ya Sisco)

 

 1. Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk. John Jingu, (Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

 

 1. Dk. Faraji Mnyepe aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

 

 1. Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM), Dk. Ngenya Athuman Yusuf (Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania – TBS).
 2. Dk. Festus Limbu aliteuliwa kuwa Mwenyekiti baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi (NEEC).
 3. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Dk. Arnold Kihaule (Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa – NIDA).
 4. Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (St. Augustine University) kituo cha Arusha, Dk. Adelardus Kilangi aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

 

 1. Profesa Raphael Chibunda aliteuliwa kuwa makamu Mkuu Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kabla ya uteuzi alikuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Sayansi na Teknolojia (Wizara ya elimu).

 

 1. Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa Makenya Maboko (Mwenyekiti Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolijia (Costech).

 

 1. Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Florens Luoga (Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania -BoT).

 

 1. Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma – UDOM, Prof. Idris Suleiman Kikula (Mwenyekiti tume ya madini).

 

 1. Dk. Florens Turuka kuwa katibu Mkuu, ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

 

 1. Mhadhiri na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri, Profesa Andrew Pembe kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi shirikishi Muhimbili (Muhas).

 

 1. Mhadhiri mstaafu UDSM, Profesa Humphrey Moshi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ushindani Tanzania (FCC).

 

 1. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Dk. Sophia Kongela akiteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mkurugenzi shirika la nyumba la taifa.
 2. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Dk. Maulid Banyani akiteuliwa kuwa Mkurugenzi shirika la nyumba la taifa.