Home Makala Mahakama ya Mafisadi iweke kando siasa

Mahakama ya Mafisadi iweke kando siasa

732
0
SHARE

Na Tobias Nsungwe

TAKRIBANI miezi nane sasa tangu Rais John Magufuli, atawazwe kuwa rais wa Tanzania baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu mwaka wa jana.

Rais huyu amekuwa taa ya mabadiliko kwa Watanzania chini ya kauli mbiu yake ya Hapa Kazi tu. Amekwisha watamkia wapinzani wake kwamba wampe fursa ya kutimiza ahadi zake alizozitoa wakati wa uchaguzi na wajiandae kumtathmini baada ya miaka mitano.

Staili ya uongozi wake imewafurahisha wananchi wengi na kuwaudhi wachache ambao walizoea kutamba na kuishi kwa kuiibia Serikali kwa mbinu kiujanja ujanja au kwa kushirikiana na wahujumu uchumi, kwa jina lingine –mafisadi.

Ujasiri wake umeelezwa kwamba unaanza kurudisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na hivyo kuamsha matumaini ya walio wengi waliokuwa wakiona keki ya taifa ikiliwa na wachache.

Mwanafasihi wa zamani wa Ufaransa, Andre Gide anasema: “Mtu hawezi kugundua bahari mpya asipokuwa na ujasiri wa kuwa tayari kupoteza uwezo wake wa kuona mwisho wa ufukwe.” Mara nyingi Rais Magufuli amesema kuwa yeye amejitoa sadaka; atapambana na wabadhilifu—atatumbua majipu bila kmwangalia mtu usoni.

Magufuli alianza kwa kuwawashia moto wanaokwepa kulipa kodi, na sasa vigogo wengi wamejikuta matatani, huku mapato ya Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yakiongezeka sana. Amebadili mtizamo wa watumishi wa umma na  hivyo kuimarisha utendaji na uwajibikaji.

Rais alikwishafuta safari za nje kwa vigogo wa Serikali na taasisi zake, isipokuwa kwa kibali maalumu. Hivi karibuni Rais Magufuli alitangaza kwamba mafao yake yatakatwa kodi, hivyo kufuta kelele za Wabunge waliokuwa wakitaka mafao yao yaendelee kusamehewa kodi kwa kisingizio kwamba fedha zao zinawasaidia wapiga kura, na kwamba fedha hizo huwasaidia kuchangia katika shughuli mbali mbali za kijamii.

Wabunge wengi hawajafurahishwa na uamuzi ule, lakini kwa Watanzania wengi, ni kicheko na faraja kwao kwani wanapenda kuona kiongozi wao akiwa mlinzi wa fedha zao za kodi ambazo kwa miaka mingi wameamini na kulalamika kuwa zilikuwa zinaliwa na wachache.

Mpigania haki za binadamu wa Marekani, Mchungaji Jesse Jackson, anasema kukiwa na ujasiri, juhudi na ari, viongozi wanaweza kubadili mambo. Rais Magufuli ameanza kwa kuonesha ari ya kupunguza matumizi ya Serikali na hasa kupambana na ubadhilifu wa mali ya umma kupitia mitandao mbali mbali waliyojiundia kupitia wapambe wao.

Serikali bado ina kazi ya kuvunja mitandao ya wezi inayoshirikiana na taasisi, au watu binafsi kuiba.

Mwanafalsafa wa Uingereza, Francis Bacon, aliyeishi kati ya Karne ya 16 na 17, aliwahi kusema matumaini ni chakula kizuri cha asubuhi, lakini ni chakula kibaya cha jioni.

Mambo yanayotajwa kuwa kikwazo kwa maendeleo ya Tanzania, ni pamoja na kurithi uchumi mbovu toka kwa wakoloni. Uwiano usioridhisha kati ya bidhaa ambazo Tanzania inauza nchi za nje na zile inazonunua kutoka nje. Nchi inakosa elimu ya kutosha ya sayansi na teknolojia, hivyo kukosa wabunifu wa kutosha kushindana na wataalamu toka nchi zingine.

Inaelezwa kwamba bado nchi haijawekeza vya kutosha katika kilimo ambacho ndicho kinaweza kutoa ajira kubwa na ya uhakika kwa vijana wanaohitimu katika shule za sekondari na vyuo kila mwaka. Ukosefu wa viwanda ni sababu nyingine ya Tanzania kubaki nyuma kiuchumi hata baada ya miaka 52 ya Uhuru.

Katika miaka yote hiyo, na hasa baada ya Azimio la Arusha mwaka 1967, viongozi waliongoza vita dhidi ya ujinga, umasikini na maradhi. Viongozi wote tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere, walikuwa pia wanapiga vita rushwa, ubadhirifu na ufisadi kwa ujumla.

Katika mambo ambayo yametajwa sana kuzorotesha juhudi za kupambana na umasikini Tanzania ni ufisadi, na mafisadi walijikita kila kona. Ndiyo maana Rais Magufuli ameamua kuiongezea nguvu vita dhidi ya rushwa kwa kuanzisha Mahakama maalum ya Mafisadi.

Rais Magufuli ametimiza ahadi aliyokuwa akiisema kila mara wakati wa kampeni za kuingia Ikulu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka jana. Tayari Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande, ameutangazia umma kwamba Mahakama hiyo itaanza kufanya kazi mwezi huu.

Tayari timu ya majaji imeundwa, mahsusi kwa kazi hiyo na kwamba wameanza kujiandaa jinsi ya kushughulika na kesi hizo za kifisadi. Mahakama hiyo itawasaidia Watanzania kujua hasa fisadi ni nani, ili kuondoa dhana ya kunyosheana vidole.

Watanzania wana hamu kubwa ya kujua mafisadi watapewa adhabu gani pindi wakipatikana na hatia. Bila shaka Mahakama hiyo haitaendeshwa kwa hisia au porojo za mitaani, itajikita katika sheria.

Mahakama ya Mafisadi ni zao la wanasiasa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Matumaini ni kwamba Mahakama hiyo haitatumika kukomoa wanasiasa wa mrengo mwingine.

Tabia ya baadhi ya wanasiasa kutaja majina ya wenzao kuwa ndio mafisadi, ni kutaka kuvuruga mwenendo mzima wa utoaji haki unaotaka mtu asihukumiwe kabla ya kusikilizwa.

Kuitumia Mahakama hiyo kuchafuana kwa malengo ya kisiasa, ni kama kuwahukumu watu wasio na hatia kwa ‘kuharakisha hukumu’. Wanasheria wanasema haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa. Wanasheria pia wanasema haki iliyoharakishwa kutolewa ni haki iliyozikwa—justice hurried is justice buried.

Kuna tofauti kati ya sheria na mila. Ipo vilevile tofauti kati ya sheria na mtazamo, au hisia za watu. Sheria inaendeshwa kwa kufuata utaratibu na kanuni, ili kuhakikisha haimadhibu mtu asiye na hatia.

Mitazamo na hisia huwafanya watu kuchukua sheria mikononi mwao, kama vile kuchoma vibaka. Wanasiasa waache kuingiza hisia zao katika Mahakama ya Mafisadi, kwani kamwe majaji hawatakubali kuendesha kesi kwa hisia. Sivyo walivyojifunza.

Ni matumaini yetu kwamba Mahakama hiyo haitajali vyama, itikadi, wala hadhi ya watuhumiwa. Ufisadi hauna chama, kabila, rangi, utajiri wala umasikini.

Nasema sitegemei kuona Mahakama hiyo ikiendeshwa kwa chuki, au kupokea shinikizo kutoka kwa mtu yeyote.  Mahakama hii mpya iachwe ifanye kazi zake kwa uhuru.