Home Latest News Majanga hujenga nidhamu kisiasa, kiuchumi na kijamii

Majanga hujenga nidhamu kisiasa, kiuchumi na kijamii

351
0
SHARE
Watoto wakinawa mikono kwa sabuni kwa kutumia maji yanayotiririka.

NA ALOYCE NDELEIO

KATI ya vitu ambavyo vimekuwa vinakwamisha ustawi wa maendeleo ya binadamu ni hofu ambapo wataalamu wa falsafa na saikolojia wanabainisha kuwa  zipo aina kadhaa za hofu. 

Kwa maana hiyo, hofu huhesabika kama ugonjwa unaohitajika kupatiwa tiba na ndio maana binadamu hutafuta namna ya kuzidhibiti hofu anazokumbana nazo. 

Kwa kawaida hofu inaweza kumkumba mtu binafsi na hivyo kuwa mzigo kwake na mara nyingi huwa ni mzigo ambao humshinda na hivyo ili kuutua mzigo huhitaji dhana shirikishi za kimaisha. 

Wakati janga la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid 19) likiwa limeenea duniani licha ya kuathiri nchi nyingi za katika mabara yote Afrika, imekuwa na ahueni kidogo kwani kiwango cha madhara kimeonyesha kuwa ni kidogo ikilinganishwa na maeneo mengine duniani. 

Madhara ambayo yametokana na janga la Corona yamesababisha kuwepo kwa hofu ya kifo. Kila mtu  anaogopa kifo. Hata kwa wale ambao hufanya mambo ya kuogofya kwa madai kuwa hawaogopi kifo kama kujitoa mhanga na ambao huhesabika kama watu waliokata tamaa katika janga kama hili hakuna ambaye anaweza kusema kuwa haogopi. 

 Aina nyingine ya hofu ni ya kukataliwa  ambayo hii huwalazimu watu wanaoangukia katika kundi hili kuwa wanajihami kwa kutafuta mbinu za kupendwa. 

Wengine huenda mbali, hutumia fedha au mamlaka wanayokuwa nayo kukirimu ili waweze kupendwa au kukubalika ndani ya jamii na hata mara nyingine kwa wenza wao. Hofu hii inapowatoka hujiita washindi kwani huonekana kuwa wanapendwa na wanakubalika. 

Hofu nyingine ni ya umasikini. Wanaoangukia katika kundi hili hulazimika kutumia mbinu nyingi ambazo si halali  kuondokana na hofu hiyo. Walio wengi hujikuta wakiiba, kupora na hata kufanya ufisadi na hata kufanya biashara haramu kama ya mihadarati. 

Kadhalika kuna hofu ya kuugua. Hii huwasumbua watu wengi. Mtu yeyote yule anapougua huwa hana raha na huhangaika kudhibiti ugonjwa wenyewe ili aondokane na mashaka pamoja na kuokoa matumizi ya ziada ya rasilimali anazokuwa nazo hasa fedha. 

Hofu mbaya zaidi ni ya kupingwa. Mara nyingi aina hii ya hofu huangukia kwa watu wanaotakiwa kuwajibika kwa jamii hususani viongozi. 

Kutokana na wengi kuwa wanakumbwa na hofu ya aina hii huwa wanatumia mamlaka waliyo nayo kudhibiti aina na mbinu zozote zile zinazoonesha kuwa zinaweza kutumika kumpinga. 

Katika tawala za kidikteta hali ya udhibiti huwa ni dhahiri na mara nyingi hutumia  kanuni ya  ‘maamuzi yanatokana ndani ya mamlaka na sio nje ya mamlaka’ hali  hii huwafanya wanajamii kukosa sauti kueleza au kujieleza. 

Ni katika aina hii ya hofu viongozi wengi wanaona njia ya kudhibiti upande mwingine unaokinzana na mamlaka hiyo hutumia vyombo vya dola kudhibiti mienendo na hata kutafuta mbinu za kudhoofisha wanaowaona kuwa ni wakinzani wao wakubwa. 

Haishangazi ndani ya Afrika kuona kuwa  viongozi wa vyama vya upinzani wakiwa wanafunguliwa mashtaka au kuwekewa vizuizi au vifungo vya nyumbani hali ambayo inakuwa ni vigumu kwao kufanya shughuli za kisiasa. Aidha viongozi wengi hukumbana na vipigo.

Kadhalika katika hali ya kujihami na kuhakikisha masilahi yao hayaingiliwi au kuguswa hofu hii huwafanya kutafuta aina ya warithi ambao watakuwa wanahakikisha kuwa wanayatekeleza maagizo yao. 

Warithi wa aina hiyo wanaweza kuwa wenza wao au wana wao na mara nyingi huwapa madaraka ya juu ambayo pindi inapofikia hatua ya kujiona kuwa wameshatosheka kutawala huwakabidhi mamlaka ya kiutawala. 

Aidha warithi wengine wanaweza kuwa ni kundi la kihafidhina ambalo kimsingi huwa halipendi mabadiliko na mara nyingi huwa na mawazo mgando kwamba ndilo kundi teule na hakuna jingine. Kundi la aina hii linaweza kuwa ni chama cha siasa. 

Kwa maana hiyo itakuwa ni vigumu kwa viongozi wa aina hiyo kuguswa pindi  wanapokuwa nje ya utawala na huendelea kutumbua maisha wakiwa wamevuna jasho la wavuja jasho katika mazingira ya kukufuru. 

Katika mazingira ambayo huwa hakuna mlango wa kutokea kwa maana ya kuwepo kwa njia za kidemokrasia za kuwawajibisha  viongozi wa aina hiyo basi watu huendelea kugugumia maumivu bila ukomo. 

Kimsingi viongozi wa aina hiyo wanapokuwa na hofu ya kupingwa au kukataliwa mara nyingi hujenga chuki dhidi ya wakinzani wao na hilo huwa dhahiri. 

Mara nyingine kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano kunaweza kutumika kuonesha chuki ambazo zimejengwa licha ya kwamba teknolojia hizo nazo hudhibitiwa na walioshika hatamu kwa kutungiwa sheria. 

Hata hivyo wale wanaogugumia maumivu wengi wao wakiwa ni wavuja jasho  maumivu yao huyatulizia katika sanduku la kura. 

Hata hivyo katika mazingira ya uhalisia kuhusu majanga ni kwamba jambo linalowezesha kuondoa hofu ni nidhamu ya kufuata maelekezo na ushauri.

Ukweli unabakiwa kuwa baadhi ya maelekezo yamekuwepo lakini hakuna ambao wamekuwa wakiyazingatia licha ya kuwepo kitaifa na kimataifa.

Suala la kunawa mikono kwa maji yanayotiririka limekuwepo na hata kuwepo siku ya kimataifa ya usafi wa mikono  ambayo huadhimishwa Mei 5 na siku ya kimataifa ya kunawa mikono kwa sabuni Oktoba 15  kila mwaka.

Watoto wa shule ndio wamekuwa wakishiriki katika maadhimisho ya siku hiyo na hivyo wao kuwa wanalifahamu zaidi zoezi hilo na umuhimu wake kuliko  watu wazima.

Leo hii baada ya  kutokea kwa janga la Corona, nidhamu imejengeka kwa watu kunawa mikono ikiwa ni moja ya njia ya kujikinga dhidi ya hofu ya kuambukizwa ugonjwa huo.

Nidhamu pia imeonekana katika mikusanyiko na hususani katika maeneo mbalimbali kuanzia mikutano ya kisiasa na masuala ya michezo na katika usafiri wa umma na hivyo kujenga nidhamu katika usafirishaji wa abiria.

Dhana ya utii wa sheria bila shuruti ambayo imekuwa ikisisitizwa na mamlaka zinazosimamia usalama barabarani  imekuwa ukitekelezwa na madereva na makondakta wao kwa kutozidisha abiria.

Hali hiyo inatokana na kujihadhari na hofu ya kuadhibiwa kwa  kutozwa faini na wakati huo huo kujikinga kwa kuhofia maambukizi ya Corona.

Hofu ya kupingwa kutokana na utekelezaji wa mbinu mbalimbali za kijiepusha na maambukizi ya magonjwa hiyo imekuwa haipo kwa kuwa  kila mmoja anataka uhai wake.

Kwa bahati mbaya imekuwepo hofu ya kubaguliwa au kunyanyapaliwa kwa wale  waliopata maambukizi na baadaye kupona hofu hiyo inatokana na baadhi  ya watu kutoelewa uhalisia  wa maambukizi ya Corona.

Kimsingi hakuna taifa linalopenda mzigo unaotokana na majanga  hivyo pale yanapotokea ikiwemo nidhamu katika kuchukua tahadhari inakuwa sahihi inakuwa ni mwitiko chanya na wenye tija kwa jamii yote.