Home kitaifa MAJANGILI WAHAMIA KWENYE NYUKI

MAJANGILI WAHAMIA KWENYE NYUKI

1070
0
SHARE

NA FRANCIS GODWIN, IRINGA


KASI ya kutokomeza vitendo vya ujangili nchini imeanza kuzaa matunda baada ya baadhi ya watu waliokuwa wanajihusisha na vitendo hivyo kuhamia katika biashara halali ya
kwa njia za kisasa. RAI linaripoti.

Hatua hiyo imekuja baada ya wakala wa  huduma  za  misitu Tanzania (TFS) Kanda ya  nyanda za  juu Kusini, Hifadhi ya mazingira  ya asili  ya  Kilombero (KNR) na maafisa ufugaji nyuki kutoa elimu kwa wananchi wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.

Wakizungumza na RAI baadhi ya wakazi wa Kata ya Udekwa wilaya ya  Kilolo  mkoani Iringa  waliokuwa wakijihusisha na ujangili wamesema sasa wameamua kuachana na vitendo  vya ujangili pamoja na uharibifu wa  mazingira.

Festo  Mhanga alisema kutokana na  kutokuwa na  elimu  na shughuli  ya uhakika  ya  kumpatia kipato alijiunga na baadhi  ya watu wanaojishughulisha na vitendo vya ujangili kwa  lengo la  kutafuta  fedha.

Watu hao walikuwa wakijihusisha na  vitendo  vya  ujangili katika  hifadhi  ya  Kilombero, lakini baada ya  kupewa  elimu ya  ufugaji  wa  nyuki  wa kisasa yeye  pamoja wenzake wameamua kujikita kwenye ufugaji  wa  nyuki na  samaki.

Alisema kikundi  chao kilikuwa ni hatari kwa ujangili, lakini sasa  kimekuwa  ni  kikundi  cha kulinda raslimali  za Taifa.

“Siku   zote binadamu  anapokosa kazi  ya  uhakika  ya  kujipatia  pesa hutafuta  shughuli  nyingine  itakayomsaidia  si  wote  hupenda kujiigiza katika vitendo  vya ujangili  ila  unakuta umejiunga  na makundi  ambayo  si  sahihi  baada ya  kukosa pesa  na  elimu  ya utambuzi wa kujua nini  cha  kufanya.

“Mimi  hapa  kijijini   nilihamia  tu  kati ya mwaka 2000 na  baada ya  kufika  nilikuta  nyama  ya  pori inauzwa kama  nyama  ya  kawaida  na wananchi wanaingia kufanya ujangili bila kuogopa ndipo  nikajiunga “ alisema  Mhanga

Alisema pamoja na kuingia kwenye kuuwa wanyama  pori baadhi  yao walikuwa wakiingia  katika  hifadhi   hiyo  kukata  miti  na kutengeneza  mizinga  ya  kufugia  nyuki ndipo wataalam  wa hifadhi  hiyo walipofika wilayani hapo na kutoa  elimu ya  ufugaji  nyuki na  uhifadhi  bora  wa  mazingira.

Mhanga  alisema pamoja na  kuwa  katika  kikundi  cha  wafugaji nyuki  kijijini  hapo  bado amejiongeza  kwa  kununua  mizinga yake 14  na  mzinga  mmoja  huvuna  asali  lita 20  na  kila  lita  moja  ya  asali huuza kwa Sh. 4000, hata hivyo hawana soko la uhakika.

Aidha, alisema ufugaji wa nyuki hata  bila ya kuwa na soko  la uhakika bado  unalipa  zaidi  kuliko  shughuli  za  ujangili  hali iliyochangia wananchi waliokuwa wakijishughulisha na vitendo  hivyo pamoja  na uharibifu  wa mazingira katika hifadhi   hiyo kukimbilia kwenye ufugaji nyuki.

Aliiomba serikali  kuangalia  uwezekano  wa  kuwaunganisha  wafugaji  hao  na soko  la  asali.

“ Bado asali yetu  inakosa  soko  kutokana na  kutokuwepo  kwa soko la uhakika pamoja na kiwanda  cha  kuchakata  asali  ili kuwa na ubora.

“Iwapo  tutasaidiwa  kuwa na mashine  zetu  za  kuchakata  asali  na  kuzipaki  tunaweza  kupiga  hatua  zaidi  na asali   yetu  kuwa na ubora maana ya kwetu  ni  nzuri  kutokana na mazingira tunayofugia nyuki ni ya  asili  ambayo yapo mbali na mashamba  ya  wananchi, “ alisema.

Akizungumzia kukoma kwa vitendo hivyo vya ujangili, Diwani  wa  kata ya  Udekwa, Peter  Mbosa alisema  awali  katika  kijiji  cha Udekwa ambacho  ndicho   kilikuwa  kikiongoza  kwa vitendo  vya  ujangili  ilikuwa ni nadra kuwakuta wanaume mitaani.

Alisema waliokuwa wakionekana mitaani zaidi ni  wanawake na  watoto huku  wanaume  wakikimbia na  kwenda  kujificha  kwa  hofu ya  kukamatwa kwa  vitendo vya ujangili.

“Kijiji  cha  Udekwa  kimebadilika  sana   siku  hizi  baada ya  wananchi  kupewa  elimu ya ufugaji  nyuki na samaki   sasa  unaweza kuona  wanaume  wanatembea  kifua  mbele, hawaogopi  kama  zamani kwa  kuwa  hakuna anayejishughulisha  tena na vitendo  vya ujangili.

“Uchumi  wa  wananchi  kwa  sasa  umezidi  kukua kutokana na  kasi ya  ufugaji  wa  nyuki na  sehemu kubwa  ya  wananchi  wanaendelea kujiunga na vikundi vya  ufugaji  nyuki na samaki  na kupitia  vikundi  hivyo  suala la doria  shirikishi  katika  hifadhi  imeongezeka na wananchi  wenyewe  sasa  wanalinda  hifadhi   hiyo,” alisema.

Aidha, Afisa ufugaji nyuki katika  shamba  la  nyuki  Udekwa, Nuru  Nema alisema shamba linalotumika kwa ufugaji huo lipo  ndani ya hifadhi ya mazingira  asili  Kilombero  na  lipo  chini ya wakala wa  huduma  za  misitu Tanzania (TFS) kanda ya  nyanda za  juu  kusini  (TFS SHZ) na kusimamiwa na mhifadhi  wa  hifadhi ya mazingira  ya asili  ya  Kilombero (KNR).

Alisema  shamba  hilo  lilianzishwa  mwaka 2013 likiwa na jumla ya  mizinga 360.

“Wakati  shamba linaanzishwa  hapakuwapo na wataalam wa  ufugaji nyuki, lilikuwa  likisimamiwa na wataalam  wa  misitu  kabla ya mwaka 2015  kupata  wataalamu  wanne wa  ufugaji  nyuki  wakiwa ni maafisa  wawili na  wasaidizi  wawili  ambao  kwa  kushirikiana na  uongozi wa  hifadhi waliweza  kuifanya kazi   hiyo licha ya changamoto  mbalimbali  zilizokuwa zikijitokeza kwa manzuki  na ubora mdogo  wa  mizinga  sasa zimekuwa  zikipatiwa ufumbuzi.

“Sasa  shamba  lina  mizinga ya nyuki 412 kati ya  hiyo mizinga 96 ina  nyuki ndani, pia tumefanikiwa kuongeza idadi ya  makundi  kutoka 40  yaliyokuwepo  hadi  kufikia makundi 96 mwaka 2016/2017 baada ya juhudi  za  kusambaza mizinga kufanyika,” alisema.

Alisema idadi ya mavuno ya  asali pia imeongezeka kutoka kilo 60 kwa mwaka hadi  kufikia kilo 120 kwa  mwaka 2015/2016 na  kilo 300 mwaka 2016/2017.

“Uuzaji  wa asali  iliyochujwa  na  kufungashwa  vizuri  umesadia kituo cha  KNR  kuongeza mapato  katika kuchangia pato  la mwaka kikanda, uchakataji wa nta ambao awali ulikuwa  haufanyiki. Mwaka 2016/2017  tumevuna jumla ya  kilo 12 za  nta pia tumesimamia vikundi  vitano  vya wananchi  wanaojishughulisha na ufugaji  wa  nyuki  kwa  vijiji vitano vinavyozunguka  hifadhi.

“Tunatarajia kujenga jengo la  kuchakata  mazao  ya  nyuki na  ofisi ambalo lipo katika mchakato chini ya usimamizi wa TBA na ofisi ya KNR. Ujenzi rasmi  utaanza  mwaka 2018,” alisema.

Aidha, alisema wamelenga kuongeza idadi ya makundi kwa  kuhamisha  mizinga upande wa  Morogoro  kama  watapewa ridhaa kutoka kwa  meneja  wa kanda kwa kuwa Morogoro kuna na joto lisilofaa kwa  ufugaji wa nyuki  ukilinganisha na Udekwa-  Kilolo.

“Suala la kuvisimamia  vikundi  vya  kijamii  katika  ufugaji  wa  nyuki kisasa  ni  moja kati ya  mkakati  wa  kudumu. Tumepanga kuendelea  kutoa elimu kwa jamii kujikita  zaidi  katika ufugaji  wa  nyuki  ili kumaliza uharibifu wa mazingira  na ujangili katika  hifadhi  nkwa kuvifikia vijiji  vyote 22 vinavyozunguka  hifadhi  hiyo,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu  wa  wilaya ya  Kilolo,  Asia Abdalah akiwa katika   ziara  yake  na kamati ya  ulinzi  na usalama  katika  hifadhi   hiyo ya mazingira  ya  asili  ya  Kilombero, aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kuilinda hifadhi hiyo kwa kuwafichua wenzao  wanaohifadhi majangili.

“Tutaendelea kupita katika  vijiji  vyote  vinavyo zunguka   hifadhi  hii  na  kuwachukulia  hatua  kali  wananchi ambao  wanawahifadhi  wageni  ambao  si  wema  wenye  lengo la  kushirikiana na  wananchi kufanya  ujangili kwenye hifadhi,” alisema.

Aidha, Mhifadhi  Mkuu  wa hifadhi  ya mazingira ya asili ya  Kilombero, Elia  Mndeme  alisema hifadhi  hiyo  yenye  ukubwa wa hekta 134,511   ilipandishwa hadhi kuwa  hifadhi ya  mazingira ya  asili Agosti 17 mwaka  2007 na  kutangazwa  katika gazeti la  serikali  namba 182 kuwa   hifadhi  hiyo imetokana na muungano wa  misitu  ya  hifadhi tatu ambayo ni Matundu, Lyondo na  west Kilombero scarp

Alisema  hifadhi  hiyo  inajumuisha  wilaya mbili  ya  Kilolo  mkoa  wa Iringa na Kilombero  mkoa  wa  Morogoro  na  kuwa  hifadhi   inazungukwa na  vijiji 21 ambavyo  vimegawanyika katika  kanda  kuu  nne kwa  ajili ya  kurahizisha  usimamizi  na kutaja  kanda  hizo  kuwa ni Udekwa , Ukwega, Mpofu  na Namwawala

Akielezea  katika  kukabiliana na ujangili  alisema  wameanzisha  doria  shirikishi kwa  kuwashirikisha  watumishi  wa wakala  wa huduma  za  misitu (TFS) hifadhi  ya Taifa  ya milima ya Udzungwa (UMNP) kikosi  cha kuzuia ujangili (KDU), askari  mgambo  wa  kijiji (VGS) na kamati  za mazingira  za  vijiji (VNRC’S ) lakini pia kutokana na mpango  kazi kamati  hizo  kila robo  mwaka  zinapaswa  kufanya  doria  zisizopungua 17.

“Hifadhi imeendelea  kuweka  mazingira  rafiki kwa  watalii  wa ndani na nje  ili  kuwavutia  wageni  kufika  kutembelea  hifadhi. Sasa tumeweka  utaratibu  wa  kutowatoza  kiingilio  wanafunzi wa  shule za msingi na sekondari  ili  kuwavutia na  kuwafanya  wapende uhifadhi  wa mazingira na utalii,” alisema.

Hata hivyo, Mshauri  wa maliasili mkoa  wa Iringa, Alloyce  Mawere alisema kuwa  mkoa  huo unazohifadhi kubwa  za Ruaha, Kitulo, Udzungwa  Scarp na  hifadhi ya  Mazingira  asili ya Kilombero  na  kuwa  moja kati ya  jitihada  zinazofanywa na mkoa  katika  uhifadhi  wa mazingira  ni  kuendelea  kuwaelimisha  wananchi  kuachana na  shughuli  zinazochangia  uharibifu  wa mazingira  katika maeneo  ya  hifadhi   hizo .