Home Latest News Majembe yatakayorejea EPL 2019-20

Majembe yatakayorejea EPL 2019-20

1930
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

UKIWA ni ukingoni mwa ligi kuu mbalimbali barani Ulaya, tayari macho na masikio ya mashabiki wa kandanda ulimwenguni yameshahamia katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.

Dirisha hilo litafungulia wiki ijayo, kwa maana ya Mei 16 na linatarajiwa kufungwa Agosti 8, mwaka huu.

Kama ilivyo kawaida, huwa kuna tetesi za usajili, taarifa zinazowahusisha wachezaji kusaini mikataba mipya na klabu zao au hata kuzikimbia na kutimkia kwingineko.

Katika hilo, makala haya yanakuibulia mastaa waliowahi kuchemka Ligi Kuu ya England (EPL) lakini huenda wakarejea nchini humo msimu ujao baada ya kung’ara huko walikokwenda.

Hatem Ben Arfa: Anaichezea Rennes ya Ufaransa lakini aliwahi kukipiga Newcastle United ya EPL. Licha ya ‘kufulia’ kipindi fulani, kwa sasa nyota imeng’aa tangu alipotua Rennes mwaka jana.

Huku mkataba wake wa sasa ukitarajiwa kufikia tamati majira ya kiangazi, klabu za Southampton na Brighton zimeanza kumfukuzia.

Mario Balotelli: Mtukutu wa Kiitaliano, ambaye kwa kipini alichokaa England, alizichezea klabu kubwa mbili nchini humo; Manchester City na Liverpool.

Tangu aliporejea Ufaransa, mambo yameonekana kumnyookea kwani alifanya vizuri akiwa na Nice, kabla ya Marseille kumchukua.

Balotelli atamaliza mkataba wake wakati wa majira ya kiangazi na tayari ameshapata ofa mbalimbali za kurejea EPL, kubwa ikiwa ni ile ya kocha Rafael Benitez anayemtaka pale Newcastle.

Yaya Toure: Kiungo wa zamani wa Manchester City ambaye kwa sasa hana timu timu baada ya kuachana na Olympiacos ya Ugiriki mwishoni mwa mwaka jana.

Hivi karibuni, nyota huyo raia wa Ivory Coast alitangaza kuwa hana mpango wa kustaafu licha ya umri wake wa miaka 35.

Kuelekea dirisha la usajili la kiangazi, tayari Crystal Palace na Burnley zimeonesha nia ya kumtaka, kila moja ikiamini uzoefu wake katika eneo la kiungo utaisaidia kukabiliana na mikikimikiki ya EPL msimu ujao.

Memphis Depay: Alikuwa winga wa Man United enzi za Louis van Gaal pale Old Trafford. Jose Mourinho alipotua, Depay akauzwa mwanzoni mwa mwaka juzi.

Kinyume cha matarajio kuwa nyota huyo alikuwa amekwisha, kwa sasa ni tishio huko Ufaransa, akiwa ndiye anayeiongoza safu ya ushambuliaji ya Lyon na hata ile ya timu ya taifa ya Uholanzi.

Haitashangaza kumuona EPL msimu ujao kwani Everton wanahaha kuisaka saini yake na kuna kipindi Liverpool nao walitajwa kummezea mate kiaina.

Rafael: Beki wa pembeni wa zamani wa Manchester United, ambaye ni raia wa Brazil. Naye anaweza kurejea England baada ya kiwango kizuri alichonacho sasa akiwa na Lyon ya Ufaransa.

Tayari West Ham wameshaonesha nia ya kumpa Mbrazil huyo tiketi ya kurejea katika mikikimikiki ya EPL, moja kati ya Ligi Kuu ngumu barani Ulaya.

Jadon Sancho: Huyo ni winga anayetamba Bundesliga akiwa na ‘uzi’ wa mahasimu wakubwa wa Bayern Munich, Borussia Dormund.

Itakumbukwa kuwa Sancho alianzia safari yake ya maisha ya soka akiwa na Watford aliyojiunga nayo akiwa na umri wa miaka saba. Akiwa na miaka 14, alihamia Manchester City lakini nako alishindwa kupenya kikosi cha kwanza.

Kwa sasa, mwanasoka huyo wa kimataifa wa England ni habari nyingine huko Ulaya na saini yake inawaniwa vikali na vigogo wa Chelsea, Man United, Liverpool na Man City.

Reiss Nelson: Mshambuliaji wa Arsenal anayecheza kwa mkopo katika klabu ya 1899 Hoffenheim inayoshiriki Bundesliga.

Msimu huu unaoendea ukingoni umekuwa mzuri kwake kwani tayari ameshapachika mabao saba katika mechi 19, hivyo moto huo unaweza kuwashawishi Arsenal kumrejesha EPL.

Licha ya kutakiwa na klabu kadhaa za Ufaransa na Italia, amekuwa akisistiza kuwa anataka kurudi Emirates na kujipigania namba katika kikosi cha kwanza cha kocha raia wa Hispania, Unai Emery.