Home Maoni Makaburi yamepoteza heshima yake!

Makaburi yamepoteza heshima yake!

2168
0
SHARE

HASSAN DAUDI

UTAMADUNI wa kumzika binadamu aliyefariki ulianzia miaka 40,000 iliyopita lakini hadi leo umeendelea kuishi, ukipewa kipaumbele katika mafundisho ya dini, nikitolea mfano Uislamu na Ukiristo.

Nikianza na Uislamu kupitia Kitabu chake Kitakatifu cha Qur-an, unaupa umuhimu mkubwa mwili wa aliyeiaga dunia, hata kabla ya kupelekwa kwenye ‘nyumba yake ya milele’ (kaburi).

Kuoshwa, kuswaliwa, kusitiriwa kwa vazi la sanda, ni sehemu ndogo tu ya heshima inayopaswa kupewa maiti, ukiacha kuwahishwa kaburini.

Ikiwa haina tofauti kubwa na Qur an, Bibilia nayo inaweka wazi juu ya thamani kubwa aliyonayo marehemu kuanzia anapokuwa kwenye maandalizi ya kuzikwa, hadi pale anapokwenda kupumzishwa.

Ishara ya msalaba na kuwaombea dua marehemu ni mfano mzuri wa maamrisho ya Dini ya Kikiristo katika kuonesha thamani ya walitangulia mbele ya haki.

Kwa mantiki hiyo basi, vitabu hivyo vinakubaliana kwamba thamani binadamu haiishi duniani, bali hata anapokuwa chini ya ardhi.

Hata hivyo, licha ya Uislamu na Ukiristo kuwa na wafuasi wengi ulimwenguni, bado kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa heshima inayopaswa kuelekezwa kwa makaburi ingawa ukweli ni kwamba si wote wanaofanya hivyo ni waumini wa dini hizo.

Si ajabu kukuta maeneo ya makaburi yakifanana kwa kiasi kikubwa na soko kutokana na shughuli za biashara ndogondogo zilizopo.

Mbali ya hilo, yamekuwa yakifanywa kuwa njia ya watembea kwa miguu, au ‘ofisi’ za madalali, au hata kijiwe cha watu wasio na kazi.

Haishangazi tena kuona watu wakijisaidia haja kubwa na ndogo katikati ya kaburi, jambo ambalo si tu kinyume cha mafundisho ya dini, pia halileti taswira nzuri kwa jamii iliyostaharabika.

Katika hilo, safu hii ya Macho Yameona inalinyooshea kidole eneo la makaburi ya Kwa Alimaua, Kijitonyama, Dar es Salaam, kama ambayo ingefanya kwingineko.

Kwa miaka mingi sasa, eneo hilo la makaburi limekuwa halina uzio, jambo ambalo linalifanya liingiliwe na shughuli za wakazi wake, ikikera zaidi tabia ya vijana kuyafanya kijiwe cha kuvutia bangi, kufanya ngono, na kucheza kamari.

Haina tofauti na makaburi yaliyopo Mtaa wa Mbyuni, Mwananyamala Kwa Mama Zakaria, Kinondoni, Dar es Salaam, ambapo hata vitendo vya uporaji vimekuwa vikitokea mara kwa mara.

Jeshi la Polisi limekuwa likipambana kwa nyakati tofauti lakini katika kile kinachoweza kuonekana kirahisi, kuyaweka makaburi hayo ndani ya uzio ingekuwa njia sahihi zaidi na si kukimbinana na wahuni hao.

Pia, kuyawekea uzio kutasaidia kuwadhibiti wale walioyaona makaburi hayo kuwa ni fursa ya kuepuka gharama za usafi. Kwamba bila hofu ya Mungu, asilimia kubwa ya takataka zao za majumbani wamekuwa wakitupa hapo.

Vilevile, Macho Yameona inaamini kuna umuhimu mkubwa wa kufanya hivyo, ikitabiri litakuwa ni suluhisho la vitendo vya kishirikiana ambavyo vimekuwa vikifanywa katika maeneo hayo yenye makaburi.

Aidha, usimamizi wa maeneo ya makaburi nao unapaswa kutazamwa upya kwani vijana wanaofanya kazi ya kuchimba kwa malipo nao wamekuwa na tabia fulani hivi ya ajabu.

Ili tu kujiingizia fedha za mteja wao mpya, wamekuwa wakilazimisha kuzika sehemu zilizojaa kwa kufukua maiti zilizopo. Hakika ni jambo baya na lisilopendeza.

Kama ilivyo ada ya Macho Yameona, imelifikisha hilo machoni mwa mamlaka husika, hivyo ni dhima ya viongozi wake na jamii kwa ujumla kuona ni namna gani tatizo hilo linaweza kupatiwa ufumbuzi.