Home Makala Kimataifa Makubaliano ya kugawana madaraka kukomesha mzozo Sudan?

Makubaliano ya kugawana madaraka kukomesha mzozo Sudan?

772
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

Baraza la kijeshi na viongozi wa upinzani nchini Sudan, wamesaini makubaliano ya kugawana ya uongozi wa Taifa hilo baada ya kukamilika mazungumzo yaliyoanza juzi ya kumaliza mzozo wa kiutawala nchini humo.

Makubaliano hayo yanatoa fursa ya Taifa hilo kuongozwa na Serikali ya mseto katika ya jeshi la nchi hiyo na raia kwa kipindi cha miaka  mitatu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu utakaowezesha kupatikana kwa uongozi wa kidemokrasia na wa kiraia.

Taarifa kutoka nchini sudani zilizoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari duniani zinadai kuwa jeshi litakuwa madarakani kwa miezi 21 ya kwanza kisha litakabidhi uongozi kwa utawala wa kiraia kwa muda wa miezi 18 itakayofuata kabla ya kutanyika Uchaguzi Mkuu wan chi hiyo.

Taifa hilo liko katika mgogoroi mkubwa ambao ulianza kwa wananchi wa taifa hilo kuandamana kupinga bei hali mbaya ya uchumi kabla ya kuungwa mkono na jeshi la nchi  hiyo na hatimaye Rais Al Bashir akalazimika kuondoka madarakani Aprili mwaka huu.

Licha ya Rais huyo kuondoka madarakani Sudan imeendelea kushuhudia maandamano ya kutaka jeshi kukabidhi madaraka kwa raia jambo lililosababisha maujai ya mamia ya waandamanaji.

Swali kubwa kwa sasa ni je, utilianaji saini huo utakomesha mzozo huo unaodidimiza juhudi za taifa hilo kutoka katika migogoro ya muda mrefu?

Sababu ya migogoro

Kabla ya kuondolewa madarakani Rais Omar Al Bashir baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa walidai kuwa sababu kubwa ya mgogoro huo kuendelea kuwapo nchini humo ni kutokana na kuendelea kuwapo Madarakani ingawa hiyo ni sehemu tu ya chanzo cha mgogoro hu lakini kwa kiwango kikubwa si sababu kuu ya mgogoro huo.

Moja ya sababu kubwa za Sudan kuingia katika mgogoro huo ilianza miaka kadhaa iliyopita baada ya kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na Marekani jambo ambalo lilifanya Taifa hilo kuanza kudhoofika kiuchumi na wananchi wake kuwa na hali mbaya ya kiuchumi na kukosa huduma muhimu pamoja na kuzorota kwa hali ya kisiasa.

Baadhi ya sekta muhimu sekta za Afya, elimu na Kilimo ambacho kilikuwa sehemu kubwa ya uzalishaji mali nchini humo zikaanza kuathirika kutokana na vikwazo hivyo. Sekta ya miundombinu nayo iliathirika kwa kiwango kikubwa huku kukishuhudiwa shirika la usafiri wa anga la nchi likitetereka kabisa.

Hali hii ilizidi na kuzikumba sekta za maji pia, fedha na hata utalii pia viliathirika licha ya jitihada kadhaa zilizofanywa na serikali ya nchi hiyo ikishirikiana na mataifa rafiki kutoka bara la Asia lakini bado hali ilizidi kudorora na kufikia hapa ambapo mgogoro huu unaibuka ukiwa ni zao la kuwekwa kwa vikwazo vile miongo kadhaa iliyopita.

Maombi kutoka jumuiya mbalimbali kuiomba Marekani kuondoa vikwazo dhidi ya Sudan ikaamua kupunguza baadhi ya vikwazo kwa kutumia kigezo kuwa ni kuimarika kwa hali ya usalama na utulivu nchini humo hasa katika jimbo la Darfur eneo ambalo kwa kipindi kirefu lilijenga sifa mbaya ya kuwa na migogoro isiyokwisha wenyewe kwa wenyewe.

Baadhi ya maeneo ambayo yaligubikwa na vurugu zilizoambatana na umwagikaji damu kama vile Abyei, Blue Nile, Kordofan ya Kusini yakarudi kuwa na utulivu. Wakati huu ilikuwa ni kabla ya Taifa hilo kugawanyika na kuwa mataifa mawili ya Sudan na Sudan Kusini.

Kutokana na kushamiri kwa migogoro ya wenyewe baadhi ya wanaharakati wakadai kuwa migogoro ni ya kupandikizwa kwa nia ya kuliingiza taifa hilo katika vurugu kubwa za kisiasa na kutoa fursa kwa baadhi ya mataifa kufanya biashara katika jimbo la Darfur.

Katika miaka ya karibuni hali ikawatofauti kutokana na kupungua kwa migogoro hasa katika maeneo maeneo ambayo yalikuwa yaliyokuwa yakikabiliwa na vurugu za mara kwa mara.

Mwanzoni mwa vuguvugu lililomwondoa Al Bashir madarakani baadhi ya wachambuzi walionya kuhusu kutopuuzwa kwa maandamano yaliyoanza kama njia ya kupinga ongezeko la bei ya mkate na hali mbaya ya chumi katika Taifa hilo na kwamba ikiwa hali hiyo itaachwa iendelee ingeweza kuleta madhara makubwa ambayo yangesababisha kutoweka kwa amani kwa baadhi ya maeneo.

Inaelezwa kuwa kiasi cha miaka mitano iliyopita Taifa hilo liliitisha mjadala wa kitaifa uliojulikana kama “National Dialogue” ambao ulitajwa kama mwarobaini wa matatizo yote ya nchini humo. Ingawa mwisho wake haukupewa kipaumbele kikubwa bado matokeo ya mjadala huo yalionekana kuwa yangeweza kuwa suluhu ya haya yote yanayoendelea nchini humo ikiwa ungetekelezwa kama ilivyokusudiwa.

Mjadala huu ulihusisha makundi muhimu nchini humo ikiwamo vyama vya siasa, makundi ya waasi, makundi ya kidini, asasi za kiraia, taasisi za serikali na binafsi a ambapo mapendekezo kadha wa kadha yalitolewa ikiwamo mfumo mpya wa Serikali na namna ambayo taifa hilo lingeweza kujiongoza ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kupokezana madaraka.

Hiyo inatajwa kuwa hatua muhimu kuwahi kufikiwa na Taifa hilo na kwa kuzingatia kuwa linaelekea katika Uchaguzi Mkuu hapo mwakani uchaguzi ambao unawekwa rehani na hali inayoendelea hivi sasa.

Maandamano yaliyomwondosha madarakani Al Bashir na vurugu za hivi sasa zinatajwa kuwa hatari kwa ustawi wa Taifa hilo kwa sasa na maisha ya baadae kwa watoto na kwamba hali hiyo si suluhisho la hali ya kisiasa wala kiuchumu bali ni vurugu zinazolenga kuibomoa Sudan iliyokuwa imeanza kusimama.

Jambo linaloshauriwa sasa ni raia wa taifa hilo wao wenyewe kuamka na kutambua kuwa Sudan ni yao wenyewe na kuona wnachokifanya ni hasara kwao na vizazi vyao vya sasa na vijavyo na kwamba kuendeleza vurugu bila kujali maslahi ya taifa lao hakutaijenga Sudan badala yake kutaibomoa na madhara yake yatamkumba kila raia siyo viongozi wala wananchi pekee.