Home Makala Makundi, tamaa ya maisha mazuri vinavyowagharimu wanafunzi wa vyuo vikuu

Makundi, tamaa ya maisha mazuri vinavyowagharimu wanafunzi wa vyuo vikuu

1303
0
SHARE

NA FARAJA MASINDE

KUMEKUWAPO na wimbi kubwa kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu ambao wamekuwa wakilalamikia hali ngumu ya maisha.

Wanafunzi hao wamekuwa wakilalamikia zaidi juu ya ucheleweshwaji wa fedha za kujikimu hali ambayo imekuwa ikisababisha maisha kuwa magumu kwa upande wao na kujikuta wakifanya mambo wasiyoyatarajia.

Baadhi ya wanafunzi wamejikuta wakifanyabiashara ambayo siyo rafiki na majukumu yao jambo ambalo limekuwa likitajwa kuchangia katika kuporomosha taaluma zao kwenye masomo.

Tafiti zinaonyesha kuwa kwa sasa siyo jambo la ajabu tena kuona mwanafunzi wa kike wa chuo kikuu akijihusisha na vitendo vya kuuza mwili.

Kwenye hilo kumekuwa na sababu mbalimbali kama wanavyobainisha baadhi ya wanafunzi kutoka kwenye vyuo vikuu mbalimbali.

Frank Kahalule, aliyeko mwaka wapili katika Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu (DUCE) kilichoko Chang’ombe jijini Dar es Salaam, anasema kuwa wanafunzi wengi wa chuo wamejikuta wakijiingiza kwenye biashara ya uuzaji mwili kutokana na kuhitaji mambo makubwa kinyume na kipato chao jambo ambalo limepelekea kuhalibu maisha yao.

“Sababu kubwa ambayo imekuwa ikipelekea haya yote ni suala zima la mazingira kwani kuna tofauti kubwa kati ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na wale wa M.U.M kilichoko Mkoani Morogoro sababu kile wanazingatia maadili.

“Wanafunzi wengi wanaosoma kwenye vyuo vilivyoko maeneo ya mjini wamekuwa wakiamini kuwa unaposoma Chuo Kikuu basi ni lazima upendeze.

“Hivyo kwa mantiki hiyo wamekuwa wakihitaji kuwa na simu kubwa kuanzia Sh 200,000, nguo nzuri na mambo yote muhimu ambayo yanagharimu fedha chungu nzima.

“Kazi huja kwamba katika ile fedha inayotolewa na bodi ya mikopo kwa ajili ya kujikimu imekuwa haitambui mahitaji hayo na hivyo hapo ndipo wanafunzi wanapolazimika kufanya kila namna ili kuhakikisha kuwa wanafanikisha kupata fedha hizo,” anasema Kahalule.

Mwanafunzi mwingine ambaye anasoma katika chuo Kikuu cha Kampala Tawi la Dar es Salaam, Janeth John, anaitaja sababu nyingine inayopelekea wanafunzi kujiingiza kwenye biashara ya kuuza miili yao na hatimaye kuharibikiwa kuwa ni pindi wanapokwenda kupanga mtaani.

“Wengi wa wanafunzi pindi wanapoenda kupanga mitaani wamekuwa wakitaka kuwa na kila kitu ndani kwa maana ya TV, radio, Sofa, kabati na vitu vingine.

“Hivyo kulingana kwamba fedha inayotolewa na bodi ya mikopo kwaajili kujikimu ni ndogo na haitambui kama mahitaji hayo hapo ndipo wanapojikuta wakifanya kila kitu ili kuhakikisha kuwa mipango yao inafanikiwa.

“Hivyo wengi wamejikuta wakiumia kwani wanataka kutumia kila wanaloweza ikiwamo kuuza miili yao ili tu kuhakikisha kuwa wanapata vitu hivyo, kwani wengi wamejikuta wakisahau mambo yao ya msingi yaliyowaleta na kujikuta wakibeba majukumu mengine ambayo walipaswa kuyafanya wakiwa tayari na masiha yao,” anasema Janeth.

Arnold Michael anayesoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye pia ni miongoni mwa wanafunzi wanaotumia Hosteli za Mabibo, anasema wanafunzi wengi sasa wamekuwa wanakimbilia maisha kwani kadiri siku zinavyozidi kwenda na wao wamekuwa wakilazimisha kuendana nayo.

“Hata hivyo kuna kundi jingine ambalo hili limekuwa likijihusisha na vitendo visivyopendeza kwa wanafunzi kutokana na kile wanachodai kuwa ni ucheleweshwaji wa fedha za kujikimu au boom kwa lugha nyingine na hivyo kujikuta wakiishi mazingira magumu.

“Na hali hii imekuwa ni mbaya sana hasa kipindi hiki ambapo wanafunzi wengi wamekuwa wakichelewa kupata mikopo ya kujikimu.

“Hivyo tamaa ya maisha mazuri, makundi yamewafanya wanafunzi wengi hasa wa kile kukikuta wakiharibu mstakabali wao wa maisha kwa kushindwa kuishi kufuatana na mazingira, kwani baadhi yao wamejikuta wakienenda kinyume na maadili yao kutokana tu na kufuata mkumbo wa namna ya kuishi.

“Wengi wanashindwa kufanya yaliyowaleta chuo na badala yake wanajishughulisha na mambo mengine yasiyo ya msingi na hivyo kujikuta hata kwenye masomo wakifanya vibaya,”anasema Michael.

Hata hivyo wanafunzi wengine wanaosoma katika chuo kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) wamekuwa wakichukulia suala la kuchelewa kwa fedha za kujikimu kwa mtazamo tofauti na hivyo kujikuta wakifanya mambo yasiyofaa.

Kwani wengine wamekuwa wakijiona kama watu wasiothaminiwa huku wakichukuliwa kitendo cha kuuza mwili kwa wanafunzi wa kike kama hali ya kujinasua.

“Unakuta inafikia mahali mpaka sisi wanaume tunapitia mazingira magumu unadhani itakuwaje kwa hao dada zetu, hivyo wanatumia njia hiyo kama sehemu ya kujiokoa kulingana na wengi kutoka kwenye familia duni ambazo pia ziko mbali na wao.

“Hivyo maisha yetu ni magumu mno hasa kipindi hiki ambacho fedha za kujikimu zimekuwa zikichelewa ikiwanganisha kuwa wapo waliopanga mtaani, hivyo mtu unajikuta tu ukiingia mtaani,” Anasema.

Hata hivyo baadhi ya wanafunzi wenyewe wa kike wanaielezea hali hiyo ya kutumia miili yao kupata fedha kutokana na kukosa fedha ya kujikimu kimaisha na hivyo kujikuta wakitumia kila njia inayowezekana ili kujinasua.

“Unajua asilimia kubwa wengi tumetoka kwenye familia za kawaida na hivyo inakuwa ni ngumu kutegemea familia ikutumie fedha za kujikimu na badala yake inabidi ufanye unavyoweza kama mwanamke ili kuhakikisha kuwa unafanikisha maisha ya kila siku kwani kuna muda unakuwa huna namna zaidi ya kujiingiza mtaani.

“Ni wazi kwamba wasichana wa chuo tunajiuza hatufanyi kusudi ila kutokana tu na kucheleweshewa fedha za kujikimu ndo unajikuta mtu unalazimikia kwenda kwenye klabu na baa kubwa nyakati za usiku kwaajili ya kufanikisha maisha,” Anabainisha mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakupenda jina laek liandikwe gazetini anayesoma katika Chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph tawi la Kibamba.

Njia ya mitandao

Kwa mujibu wa utafiti uliotolewa na mtandao wa Time wa nchini Marekani, umebaini kuwa wanafunzi wanaotaka kujiunga na vyuo wamekuwa waakitumia mtandao wa kijamii wa Instagram kwa kuchagua vyuo wanavyotaka kujiunga navyo.

Utafiti huo uliendelea kubainisha kuwa wanafunzi hao walifikia hatua hiyo baada ya kushindwa kujua maisha halisi ya vyuoni ikiwamo kutambua vitu vidogo vidogo kuhusu vyuo wanavyofikiria kujiunga navyo ikiwamo kujua hali halisi ya maisha ya wanafunzi wa kawaida vyuoni.

Wanafunzi hao walienda mbali zaidi na kudai kuwa baadhi ya vipeperushi ambavyo vimekuwa wengine wamesema vipeperushi vinavyotolewa na vyuo vingi havijibu maswali ya hali halisi ya maisha vyuoni na ndio maana wengi wameamua kutumia Instagram ili waweze kuchunguza wenyewe maisha ya kawaida ya kila siku vyuoni yakoje, kujua kama vyuo hivyo vitawafaa.

Hata hivyo hali hiyo ni tofauti na hapa nchini ambapo wanafunzi wengi wanatumia mitandao hiyo ya kijamii au utandawazi kwa namna tofauti ambayo imekuwa na matokeo hasi badala ya chanya.

Kwani mitandao hiyo inatajwa kama moja ya njia nyingine ambayo inatajwa kutumiwa na wanafunzi hao ambapo kwenye mitandao hiyo kunaelezwa kuwapo na makundi maalumu yanayojihusisha na biashara hiyo.

Mitandao ya kijamii kama, WhatsApp, Facebook na Instagram kumekuwa na makundi ambayo yamekuwa ni maalumu kwa ajili ya kufanya biashara hiyo.

Mitandao hiyo imetajwa kuongeza matukio ya kubakwa, madawa ya kulevya, utapeli, kutekwa na matukio mengine ya ajabu kwa wanafunzi.

Kweye mitandao hiyo kuna majina ya makundi maarufu kama, Benki ya Utamu, Jicho la Mvulana Liko Fasta, University Tanzania Jokes na mengine mengi ambayo yamekuwa yakiendesha biashara hiyo.

Kitu kinachofanyika kwenye makundi hayo ni kwamba huwekwa picha za wasichana mbalimbali pamoja na mawasiliano ambapo huwa ni kazi ya mwanaume kuingia na kuchagua msichana unayemtaka na kisha kuwasiliana naye ikiwamo kiasi cha fedha.

Miongoni mwa wanafunzi wanaotajwa kuwapo kwenye mitandao hiyo ni wavyuo vya, Chuo cha Usimamizi wa Fedha(IFM), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM), Chuo cha Elimu ya Biashara(CBE), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) na vingine vingi.

Kuishi kwa kamali

Mbali na wasichana hao kukabiliwa na maisha magumu na hata kupelekea kutumia miili yao kama mtaji wakujiongezea kipato cha kuendeshea maisha yao ya kila siku huku wakisubiri fedha za kujikimu(Boom) wanafunzi wa kiume nao wamekuwa wakitumia michezo ya kamali kama sehemu ya kujikwamua.

Vijana wengi wa chuo wamejikuta wakiendesha maisha yao kwa kucheza kamali kwenye mashine zilizoko kwenye baadhi ya baa za jirani na hosteli zao pamoja na mashine za kubashiri matokeo ya michezo mbalimbali ili kuweza kupata fedha ya kuendesha maisha.

“Unajua wakati mwingine unakuwa huna namna ya kufanya ili kuweza kufanikisha maiahs ya kila siku hiyo inakubidi tu uingie mtaani kwaaji ya kujaribu bahati yako kwani tofauti na hapo unaweza ukakosa hata pesa ya vocha.

“Hivyo ukicheza ukibahatika kushinda hiyo ndiyo inakuwa bahati yako, ndiyo maana utakuta vijana wengi nyakati kama hizi ambapo fedha za kujikimu zinachelewa hujikuta wakiishi kwa mtindo huu wa kutegemea kamali.

“Japo jambo linalotusaidia ni kusema tu kwamba hasa sisi wanafunzi wa Hosteli hasa hii ya Mabibo tupo karibu na chuo hivyo hata ukiwa huna nauli unauwezo wa kuamka mapema na ukawahi kipindi, ila ukweli ni kwamba muda mwingi inakubidi ucheze tu kamali kupitia simu yako ili upate chochote kitu,” anasema mwanafunzi huyo.

Mmoja ya wahudumu wa baa iliyopo maeneo ya Mabibo Hostel ambaye hakupenda kuandikwa jina lake kwa kuhofia kibarua chake anasema kuwa amekuwa akishuhudia vijana wengi wakikimbilia kufanya ubashiri ili tu kuweza kujipatia kipato cha kukidhi mahitaji yao pindi fedha zinapochelewa.

“Hii hali imeenda mbali zaidi mpaka baadhi ya vijana kuita sehemu hizi za kamali Ofisi ndogo ambapo wamekuwa wakichukulia (betting) kama biashara yao pindi wanapokumbana na kipindi kigumu jambo ambalo limepelekea kuendelea kuongezeka kwa mashine za kuendeshea michezo ya kamali,” anasema.

Vijana wa kiume kulelewa

Hili linatajwa kama kimbilio jingine kwa wanafunzi wa vyuo kwasasa hasa vijana wa kiume ambao wamekuwa wakitum,ia mwanya huu kuweza kulelewa na wanawake watu wazima ambao wamewazidi umri.

Aina hii ya maisha inaelezwa kama adha kubwa kwa wabnafunzi kwasasa kwani ni janga linaloelezwa kumaliza vijana wengi na hivyo kujikuta baadhi yao wakijitumbukiza kwenye ulevi.

“Vijana wengi wa chuo wanaliona hili kama kimbilio lao ambapo wamekuwa wakipendwa na akina mama watu wazima na hata kufikia hatua ya kuwahonga magari ya kutembelea ili mradi tu maisha yaweze kwenda, japo baadhi yao wamekuwa wakishindwa kabisa kufanya vitu hivi viwili kwa wakati mmoja.

“Kwani wamekuwa wakielemewa kutokana kwamba kinamama hao wamekuwa wakitoa fedha na kila kitu kwa vijana hao huku wao wakiwatimizia mahitaji yao ya ngono na hivyo kujikuta wakiwa watumwa kwa wafadhili wao hao,” anasema mmoja wa wanafunzi hao.

Mwisho