Home Habari MAKUNDI YANAITESA CCM

MAKUNDI YANAITESA CCM

2229
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU


MVUTANO na mnyukano wa maneno unaoendelezwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, dhidi ya kada wake Bernard Membe, unachangiwa zaidi na uwapo wa makundi ya kimkakati ndani ya chama hicho. RAI linachambua.

Makundi hayo ambayo kiasili yalianza tangu awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi hii na kukolezwa zaidi katika harakati za kumsaka Rais wa awamu ya tatu na baadae awamu hii, yanadaiwa kuwa mwiba mkali kwa chama hicho, hasa katika safari ya kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Pamoja na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuhamia upinzani na kuwapo kwa harakati kadhaa ndani ya CCM za kuyavunja makundi hayo kwa kuwaondoa kiaina kwenye ulingo wa siasa za kiushindani baadhi ya makada waliokuwa na ushawishi ndani ya CCM, bado nguvu na nyayo zao zinaishi ndani ya chama hicho.

Kundi lililokuwa tishio ndani ya chama hicho ni lile lililobatizwa jina la Mtandao, ambalo lililosambaratika mwaka 2015 mara baada ya Lowassa kuhamia Chadema.

Pamoja na kundi hilo kusambaratika, wachambuzi wa mambo wanadhihirisha kuwa vivuli vya mwanamtandao mmoja mmoja bado vipo na vitakisulubu chama hicho hasa katika nyakati za kuelekea uchaguzi Mkuu.

Tayari kivuli cha Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Membe kimeshaanza kuibuka na kinaonekana kukitesa chama hicho, hatua iliyomsukuma Dk. Bashiru kusimama hadharani na kukikemea kwa matamko na maagizo kadhaa.

Ipo dhana kuwa baadhi ya makundi hayo hayafurahishwi na mwenendo wa mambo ndani ya chama na Serikali na tayari wameshaanza kupandikiza watu wao kukikosoa chama na serikali ndani na nje ya Bunge.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa  mwaka 2015, uliompa nafasi Rais Dk. John Magufuli kuiongoza nchi,  huku Membe akiishia katika hatua ya tano bora, mwanasiasa huyo aliyekuwa akichuana vikali na Lowassa amekuwa kimya.

Ukimya wake huo umeonekana kama njama na mbinu za chini kwa chini za kumkwamisha Mwenyekiti wa CCM, hasa katika Uchaguzi Mkuu ujao, hatua iliyomsukuma Dk. Bashiru kutangaza hadharani kumuita Membe aende ofisini kwake kujieleza juu ya tuhuma hizo.

Muda mfupi baada ya agizo hilo la Dk. Bashiru, mjadala mkali ulianza kwenye mitandao ya kijamii na kumuibua Membe ambaye alimjibu kiongozi huyo wa chama kwa kumshangaa.

Membe ambaye alijibu mapigo kwa kuandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwa kuushangaa  utaratibu uliotumika kumwita akibainisha kuwa pengine ni ugeni wa kazini wa Bashiru, lakini akaahidi kwenda kumwona mara baada ya kurejea kutoka safari ya nje ya nchi.

Membe alikwenda mbali zaidi kwa kumtaka Dk. Bashiru pia amwite mmoja wa watu waliotoa tuhuma hizo.

Dk. Bashiru naye alijibu mapigo kwa kumwambia Membe kuwa kumpa sharti la kukutana naye si utaratibu wa chama hicho na kumtaka ajifunze hekima na busara kutoka kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Mnyukano huo umewalazimisha wakongwe wa chama hicho kuibuka na kumkosoa DK. Bashiru kwa hatua yake ya kumwita Membe hadharani, kinyume na utaratibu, ingawa nae tayari ameshamjibu kwa kuwataka wastaafu watulie ili wakiweke chama sawa.

Miongoni mwao ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa ambaye alisema kuwa njioa aliyoitumia Dk. Bashiru iko nje ya utaratibu wa chama chao pale kinapohitaji kushghulikia tuhuma dhidi ya mwanachama wake.

Kauli hiyo ya Msekwa aliitoa katika mahojiano yake na gazeti la  Mwananchi, pamoja na mambo mengine alisema alichotakiwa kukifanya Dk. Bashiru ni ama kumpigia simu au kumwandikia barua ya kumtaka afike ofisini kwake.

Akizungumzia makundi yanavyokitesa chama hicho, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala ambaye alisema mvutano ulioibuka hauna misingi maalumu zaidi ya kudhihirisha kuwa bado chama hicho kina makundi.

“Kama kuna kambi za Membe, wangemuita na kumuuliza  kama ni kweli au si kweli bila kufanya jambo kuwa kubwa na kuleta mjadala mkubwa wa kitaifa. Sioni sababu. Kama Membe anataka kugombea ni haki yake na Katiba inamruhusu labda ule utamaduni tu wa CCM ndio haumruhusu.

“Ila ukifuata misingi ya demokrasia yule aliyepo madarakani ajitokeze wa kushindana naye, kuwapo kwa mgombea mmoja tu si demokrasia. Dk. Bashiru angetumia njia ambazo hazikuzi suala hilo na kuwa kubwa kiasi hiki,” alisema.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine, Profesa Mwesiga Baregu alisema  Dk. Bashiru anatakiwa kuzingatia ushauri uliotolewa na kiongozi wa zamani wa CCM, Pius Msekwa kwa kuwa ni ushauri mzuri, kwa kuwa kwa uzoefu wa Dk. Bashiru katika mambo haya ni mgeni.

Alisema inawezekana Dk. Bashiru amefanya makosa ya kiutendaji  lakini yamezalisha mtafaruku ndani ya chama hicho.

Alisema mitafaruku iliyojitokeza sasa inaashiria kisasi, kwamba wale waliogombea na Rais Magufuli bado wanautamani urais.

“Licha ya kwamba Rais anawapaka kina Lowassa mafuta kwa mgongo wa chupa, kiuhalisi bado wanamtesa.

“Membe naye anajipanga kugombea ila wao wenyewe wanaonesha hofu kabisa. Kwa maana hiyo makundi yaliyomsapoti Lowasa na Membe yapo,” alisema.

Alisema kwa kuwa makundi hayo yalikuwa na nguvu, ndiyo hayo yanayompa shida Rais Magufuli ambaye naye anatarajiwa kugombea ngwe ya pili ya uongozi wake kama ilivyo utamaduni wa CCM.

“CCM wanapata shida kuwashawishi na kuwaweka pamoja makada wake. Maana inaonekana hakuna uhakika wa kuwapo kwa makundi yanayomuunga mkono Mwenyekiti wao kwa hiari yao si kwa nguvu. Ndio tatizo linalokitesa nchama hicho,” alisema.

MEMBE KUTEGWA

CCM ina utamaduni wa kumuachia mwanachama aliyeshinda uchaguzi wa Rais apitishwe kugombea urais bila ya ushindani ndani ya chama na kauli ya Dk Bashiru inaonekana kulenga katika kuendeleza utamaduni huo.

Hata hivyo Membe anaonekana kutegwa kama ilivyokuwa mwaka 2014, ambapo alikuwa mmoja wa wanachama sita wa CCM waliofungiwa kwa muda kujihusisha na siasa kwa madai ya kuanza kampeni za urais mapema akiwa pamoja na Lowassa,  Frederick Sumaye, William Ngeleja, January Makamba na Stephen Wasira.

Itakumbukwa kuwa Membe alikuwa mmoja wa wanachama 38 wa CCM waliochukua fomu kutaka kugombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2015, lakini aliishia tano bora alipoenguliwa na Halmashauri Kuu.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu Membe amekuwa hajishughulishi na siasa zaidi ya kuonekana katika shughuli za kijamii.

Dk Bashiru anakariri taarifa zinazomtuhumu Membe kuwa anafanya vikao ya kutafuta urais kabla ya muda na ndio maana anataka aende ofisini kwake kujibu tuhuma.

“Iweje watu waseme kwamba wewe (Membe) unafanya vikao vya kutafuta kura za 2020..kwamba unataka kumkomesha Rais Magufuli, halafu unakaa kimya tu? Sasa mimi nakualika uje ofisini kama ni mwanachama wa kweli aliyetoa ahadi ya uanachama wa CCM.”

KAULI MBILI ZA DK. BASHIRU

Katika hatua nyingine  Dk. Bashiru amelitumia sakata hili kutoa kauli mbili tofauti zote zikibeba nia ya kumwita Membe.

Awali alisema  alimwita Membe akiwa kama mmoja wa kada wa chama na mtu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje ambaye pia ni mwananchama wa CCM.

Alisema yeye kama Katibu wa chama ana haki ya kukutana na viongozi wa sasa na wa zamani kwa nia ya kujadili masuala ya kuimarisha chama.

“Moja ya haki ya kiongozi kwa nafasi yangu ni ya kukutana na viongozi wa chama, baada ya mimi kuteuliwa kwenye nafasi hii nimekutana na makada na viongozi mbalimbali wa CCM akiwemo Rais mstaafu Benjamin Mkapa, Maria Nyerere, hao wote ni makada kama alivyo Membe.

“Wengine ni Warioba (Waziri Mku Mstaafu, Sinde), Dk Salim Ahmed Salim, Hussein Bashe (Mbunge wa Nzega Mjini), Joseph  Butiku, Nape Mnauye (Mbunge wa Mtama),” alisema.

Alisema pia alikutana na Waziri Mkuu Mstaafu, John  Malecela ambaye alimuhimiza juu ya umuhimu wa kukaa karibu na mabalozi wa nyumba 10 kwani wao ni muhimili wa chama.

“Mzee Malecela alinikumbusha kuwa CCM ingepata tabu kupita uchaguzi wa mwaka 2015 ila ikanusurika kwa sababu ya mchango mkubwa wa ukaribu mzuri wa  mabalozi wa nyumba 10, ndiyo moja ya nguzo za uhai wa CCM ambao walisaidia kupambana na timu Lowassa, timu Membe na nyinginezo zilizotaka kupasua nchi na chama akasema.

“Aliniambia ukaribu wa mabalozi ni muhimu kwani hawana timu Membe wala timu Lowasa timu January Makamba (Mbunge wa Bumbuli) na wengine mnaowajua, akasema mabalozi ndiyo wanakua kazini kusaidia chama lakini timu hizo huwa kazini kutafuta uongozi.

“Sasa iweje mimi kusema nataka Membe aje ofisini kwangu imekuwa jambo kubwa, najua yeye ni kada, tangu niteuliwe hajawahi kunisalimia, ningehitaji busara zake.

“Pia nimesikia mabarabarani huko kwamba anaendeleza makundi,  kazi yangu mojawapo ni kuratibu shughuli zote za kitaifa, sikutarajia kujibiwa mtandaoni na akasema eti mimi ni ‘mgeni wa mambo’,  mimi  ni mgeni wa timu Membe na timu Lowassa, ila  sio mgeni wa CCM.

“Sio mgeni wa kanuni za CCM, ana hiari ya kuja sina mashtaka nae, aje tujadili changamoto zinazowakumba wakulima wa korosho pia tujadili na kuimarisha diplomasia.

“Mbona anakimbilia mashtaka, halafu anachanganya anasema habari ya TIS (Usalama wa Taifa) kwenye mitandao, someni Katiba ya CCM, mimi kazi yangu ni kusimamia taratibu za CCM,  mimi ninahusika na TIS? Someni Katiba kama mimi ninahusika kwa namna yoyote nayo, anajua tangu amekuwa waziri na kada anajua nani anahusika nayo.

“Vilevile anamhusisha Musiba (Cyprian) katika mkutano wangu na yeye, kwanza Musiba ana nini jipya? amemtaja hata naibu katibu mkuu wa Zanzibar, ambaye ni mjumbe  wa sekretarieti, lakini mjumbe huyo anajua taratibu ndiyo maana hapayuki kwenye mitandao,”alisema.

Dk. Bashiru aliendelea kusema. “Chama siyo chombo cha kusimamia wanaharakati wala hatupimi ukweli wa wanaharakati, unajua nchi hii tulifika mahala kakikundi kalijitokeza na kujifanya ndio kako juu ya sheria wakataka kukisambaratisha chama.

“Namhimiza Membe aje sio kwa ajili ya mashitaka aje tujenge chama, simzuii kunijibu kwenye mitandao na anayoyajibu yanatupa nafasi sisi wana CCM kupimana, kasoro mbali mbali, na nimeziona  meseji zake kuwa mimi ni mgeni, hakuna timu nani wala nani ndani ya chama, wote tuna hadhi moja kwa haki ya wananchama,”aliongeza.

Muda mfupi baadae ilisambaa taarifa iliyomnukuu Dk. Bashiru akiweka wazi kuwa endapo Membe hatafika ofisini kwake kabla ya Desemba 17 na 18 atakiomba kikao cha Kamati Kuu na NEC kimwazimie kwa maana ni ukweli usiopungika kuwa Membe na genge lake wanajua kuwa chama hicho kina vyombo vyake na hata serikali pia inavyombo vyake na wanapoamua kusema wanauhakika na wayasemayo na kwamba CCM hii ya Magufuli si kama zile walizozizoea.