Home Uhondo wa Siasa MALAIKA AKIZEEKA ANAKUWA SHETANI

MALAIKA AKIZEEKA ANAKUWA SHETANI

1663
0
SHARE
Zitto Kabwe (kulia) akiwa na baadhi ya waliokuwa viongozi wa ACT- Wazalendo

NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha ACT-Wazalendo kinapita kwenye mapito mazito, kinatafunwa na dhambi ya usaliti na utengano iliyoasisiwa na na waasisi wake miaka kadhaa nyuma.

Wanaokisaliti chama hicho sasa ndio waliohusishwa na usaliti kwenye chama walichojifunzia siasa baadhi yao, hawa walitoka huko wakiwa ni malaika waliotakaswa na utakaso wa dhabihu.

Bahati mbaya malaika hawa wa jana leo wamezeeka na kuzama kwenye ushetani.

Masimulizi ya kale yanaeleza kuwa Shetani alikuwa ni malaika mtiifu mbele za Mungu na alikuwa akishiriki katika masuala mbalimbali yaliyokuwa yakifanywa na bwana wake.

Kwa sababu alikuwa ni malaika mtiifu, alipata nafasi ya kuyajua mengi yaliyokuwa yakimuhusu mkuu wake wa kazi.

Na kwa sababu hakuwahi kuwa na rekodi za uchafu na usaliti, hata malaika wenzake walimpenda na kumwamini, wakijua ni mwenzao na kamwe hawezi kufikiri na kuwaza kuwaasi wao na Mungu wao.

Aliendelea kuwa mtii kwa miaka dahari hadi pale alipoamua kuasi, nadhani aliasi kwa sababu umri ulishamuacha na baadhi ya mambo ya kishetani aliyopata nafasi kuyaona yalimvutia.

Cha kwanza alichokifanya ni kuasi kwa kuamua kutoka kwenye maisha ya raha yasiyo na bughudha, yasiyo na ulevi wala uzinzi na kuamua kujitumbikiza huko.

Akanogewa zaidi na zaidi, akajikuta anatumia uzoefu wake wa kimalaika kuwarubuni binadamu waliokuwa wema, kwa kasi ya ajabu akayafanya matendo ya kidhalimu ambayo hakuwahi kuyafanya kipindi alipokuwa mtiifu mbele za Mungu.

Kwa kiburi cha kuyajua matendo ya kimalaika akaanza uzinzi, akanogewa zaidi na uzinzi hadi kupora wake za watu, hakuona soni wala haya kuendelea kula vyakula alivyokuwa akishiriki kuwakataza wanakondoo wasile.

Pamoja na uasi wake huo kamwe bwana wake hakuwa hakumhukumu na alifanya hivyo kwa sababu hakuwa mtu mwenye visasi, alichofanya ni kuwatuma mitume ili waende duniani  wawaeleze binadamu namna ya kuviepuka vishawishi vya shetani.

Zoezi la kushawishi binadamu kuepuka vitendo vya shetani, linaendelea kufanyika, lakini ugumu bado upo.

Lakini swali la kujiuliza, ni hili, hivi  inawezekana malaika kuwa shetani? Bila shaka jibu lake ni ndio, inawezekana,  tena inawezekana kabisa na inawezekana kwa sababu shetani nae ni malaika kama nilivyotangulia kusema huko mwanzo.

Na hata Kamusi ya Kiswahili Sanifu toleo la pili ukurasa wa 368 inathibitisha kuwa shetani ni malaika anayesadikiwa kuwa amelaaniwa kwa kukataa kufuata amri ya Mwenyezi Mungu, ibilisi, milihoi na rajimi.

Lakini pia inatoa tafsiri tofauti na hiyo ya awali kuwa shatani ni mtu mwenye vitendo vibaya; habithi.

Kwa tafsiri zote mbili zinadhihirisha kuwa shetani aliwahi kuwa malaika wa Mungu, kwa maana alikuwa akitenda na kuzungumza yale aliyokuwa akiagizwa na mkuu wake.

Sijawahi kusikia kama malaika shetani aligeuzwa na kuwa shetani baada ya kuzeeka, kwa maana alikuwa shetani baada ya kuasi.

Shetani bado anaishi, maisha yake yametawala miili ya binadamu, anaishi kwa nyama na damu za baadhi ya binadamu.

Kwa muktadha huu ni wazi shetani anaishi ndani ya baadhi ya wanasiasa waliofanikiwa kujizolea heshima kubwa hapa nchini.

Bahati mbaya shetani amewazidi nguvu, maarifa na ufikiri wanasiasa hawa ambao kabla ya kuzidiwa nguvu na shetani waliwaaminisha Watanzania kuwa wao ndio wamebeba dhamana ya mabadiliko ya wanyonge.

Kwa sababu ya ushetani wao uliozongwa na uasi, uzee na tamaa ya kufanya mambo waliyochelewa kuyafanya ujanani, wamejikuta wakiwa na sura ya binadamu huku ngozi ya miili yao ikigubikwa na ushetani, uongo, chuki, tamaa na unazi.

Hapa ndipo inapokuja dhana ya malaika akizeeka anakuwa shetani. Inasikitisha kuona baadhi ya wanasiasa waliokuwa wakihubiri mabadiliko, leo hii wanageuka na kuwa watumwa wa wale waliokuwa wakiwarushia mawe.

Bila haya wala soni, wanajaribu kujing’ata wenyewe ili kuwafurahisha waliowatuma ambao huenda wamewapa kazi moja tu ya kupiga kiota kilichokuwa na makinda yanayohitaji msaada wao. Unafiki wa wazi huu!!

Sikuwahi kufikiri kama wanasiasa wenye heshima ya kiwango cha kilichowafanya waonekane ni watetezi wa wanyonge leo hii wamegeuka nyoka wenye mate ya sumu, ambayo kwa makusudi wameamua kuwatemea wenzao.

Si dhambi kuwa kibaraka wa wachache, lakini kabla hujaamua kuwa kibaraka wa wachache ni vema wangejiuliza na kurejea kwa Mungu wao ili kupata majibu sahihi ambayo wangetoka nayo hadharani na kuwaeleza Watanzania ukweli wa mambo ulivyo.

Nathubutu kusema, kwa hatua hii ya malaika aliyetegemewa na wengi kuwa mkombozi wa wanyonge  kugeuka na kuwa shetani, ni rahisi sana kwa wanyonge kuendelea kunyonywa na hakutakuwa na wa kuwatetea kwa sababu waliotegemewa wamenogewa na matendo ya kishetani.

Wanyonge waliamini malaika hawa waliokuwa wema, kamwe wasingeasi hata kama makazi yao yalikuwa yamevamiwa na binadamu  waliokuwa na taka midomoni mwao.

Kwamba malaika hawa walikuwa na jukumu la kuitakasa midomo ya wachafu hawa walioamua kurejea kwenye mikono ambayo malaika hawa waliiona ni salama.

Bahati mbaya kwa sababu ya dhambi ya uasi ambayo haiishi, malaika hawa wameamua kuwa mashetani na kwa sababu ya ushetani wao wamekuwa wa kwanza kuwatusi wenzao hadharani Watanzania hawatawasahau kamwe kwa uchafu wenu huu.

Natamani mwale wa moto utokee leo hii na kuwaunguza wanasiasa wa aina hii ya uongo na umbea ambao wanatembea na mateso ya Watanzania.

Hata hivyo, nina imani dhambi yao hii ya usaliti, unafki na ukuda haita waacha salama, badala yake itawamaliza wao na vizazi vyao.