Home Makala MALAWI: KIFUNGO CHANYEMELEA RAIS BANDA

MALAWI: KIFUNGO CHANYEMELEA RAIS BANDA

1239
0
SHARE

LILONGWE, MALAWI


Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa nchi ya Malawi imekuwa ikitikisika kutokana na kashfa kubwa ya ufisadi iliyopachikwa jina la ‘Cashgate.’ Kashfa hii iliibuliwa katika kipindi cha Rais aliyeondoka, Joyce Banda ambaye alishindwa katika uchaguzi wa May 2014.

Kashfa hii ambayo kutokana na kiasi kikubwa cha fedha zilizochotwa na udogo wa nchi na uchumi wake, imekuwa gumzo kubwa miongoni mwa wananchi kiasi kwamba serikali ya Peter Mutharika ilishindwa kuinyamazia.

Imeitwa Cashgate kutokana na kiasi kikubwa cha fedha taslimu zilizofichuliwa na kukamatwa kutoka majumbani na ndani ya magari ya watumishi wa serikali wa vyeo vya juu, hali kadhalika wafanyabiashara.

Hadi sasa watu kadha wamefikishwa mahakamani na kushitakiwa, na wengi wamehukumiwa kwenda jela kwa makosa ya ubadhirifu wa fedha za umma.

Wakati kashfa hii ilipoibuka Septemba 2013 serikali kadha za wafadhili wa nje walisitisha misaada yao katika bajeti ya serikali ya Malawi, hali iliyosababisha upungufu mkubwa wa mzunguko wa fedha, huku imani kwa wawekezaji nchini ikishuka sana.

Ukaguzi wa kina uliofanywa mwaka 2014 kuhusu ufisadi huo uligundua kwamba zaidi ya Dola za Kimarekani 32 milioni zilipotea kutoka hazina ya nchi hiyo katika kipindi cha miezi sita tu ya mwaka 2013.

Lakini makisio ya hivi karibuni yanaonyesha wizi wa fedha za serikali umekuwa ukifanyika tangu 2009 na kwamba zaidi ya Dola za Kimarekani 280 milioni huenda zikawa zimeibiwa.

Kesi zilizotinga mahakamani zilitoa hukumu za vifungo gerezani vya vipindi tofauti kwa jumla ya watu 13 wakiwemo watumishi wa serikali na wafanyabiashara. Lakini ilionekana wazi kwamba wahusika wakuu bado hawajahukumiwa au hata kutiwa mbaroni.

Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali Mary Kachale amesema hali hii itabadilika wakati kesi za wahusika wakuu, zilizoanza kusikilizwa mapema mwaka huu zitakapoanza kutoa matokeo.

Kesi hizi zinatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwaka huu ingawa wengi wanaona hili haitawezekana kutokana na ucheleweshaji wa mara kwa mara.

Ushahidi uliotolewa mahakamani na Leonard Kalonga, Naibu Mkurugenzi wa zamani katika Wizara ya Utalii, ulimtaja Paul Mphwiyo Mkurugenzi wa Bajeti kuwa ndiye mhusika mkuu katika uchotaji huo. Yeye mwenyewe Kalonga alikuwa tayari anatumikia kifungo jela baada ya kupatikana na hatia ya utakashaji fedha (money laundering).

Kalonga alisema Mphwiyo ndiye alikuwa kinara katika ufisadi huo na alidai kwamba yeye (Mphwiyo) ndiye alitenga asilimia 60 ya fedha kwenda katika matumizi ya kilichokuwa chama tawala cha Rais Joyce Banda – Banda’s People’s Party (PP), na asilimia 40 nyingine ya fedha ziligawanywa kwa wahusika wengine – watumishi wa umma.

Wakati wa wizi huu Rais Joyce Banda alikuwa anaiandaa nchi kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika May 2014.

Kalonga aliiambia mahakama katika ushahidi wake kwamba fedha hizi ndizo mgombea urais Joyce Banda alikuwa akitapanya katika kampeni katika kutaka kuungwa mkono – wakati mwingine akitoa fedha taslimu kwa wahudhuriaji wa mikutano yake ya kampeni.

Ushahidi huu wa Kalonga na mashahidi wengine (ambao nao tayari wanatumikia vifungo jela kwa wizi huo huo) umeongeza hisia kwa watu wengi nchini humo kwamba Rais wa zamani Joyce Banda ndiye alikuwa mnufaika mkuu wa fedha za kashfa hiyo ya Cashgate na huenda ndiye aliubariki mpango mzima wa uchotaji.

Lakini hadi sasa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaomuunganisha rais huyo wa zamani na ufisadi huu ingawa maswahiba wake kadha wa karibu wamehusishwa moja kwa moja.

Joyce Banda mwenyewe mara kwa mara amekuwa akikana kuhusika, lakini tangu aondoke Malawi Septemba 2014 baada ya kushindwa uchaguzi hajakanyaga tena nchini humo.

Ametaja sababu kadha kwa nini hajarejea nchini, lakini Wamalawi wengi wanahisi kutorejea kwake kunatokana na hofu ya kushitakiwa.