Home Habari Malengo SADC yafanane – Mhadhiri

Malengo SADC yafanane – Mhadhiri

1049
0
SHARE

Leonard Mang’oha

WAKATI Tanzania ikiendelea na maandalizi ya mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), umetolewa wito kwa nchi hizo kuwa na malengo yanayofanana.

Akizungumza Dar es Salaam, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja, alisema nchi wanachama wa SADC zinaweza kufanikiwa ikiwa zina malengo yanayofanana.

Alisema mara nyingi mikutano ya aina hiyo inalenga kufuatilia, kutathmini mambo ambayo walikubaliana katika mikutano iliyotangulia kama yameweza kufikiwa au la.

“Kwamba tumeshakaa kwa pamoja kwa muda, moja, mbili, tatu tumeyafanya, lakini matokeo yake ni moja, mbili, tatu. Lakini moja, mbili, tatu hatujayafanya, matokeo yake ni haya, ndiyo madhumuni ya mkutano huu,” alisema Profesa Semboja.

Alisema mkutano huo pia utamwezesha Rais Dk. John Magufuli ambaye amekuwa akihimiza maendeleo ya viwanda, kukutana na viongozi wenzake katika jumuiya hiyo kuona jinsi gani wanatimiza azma hiyo.

“Katika nchi hizi masikini, hakuna nchi ambayo imefikiria itapata maendeleo bila kujiendeleza kiviwanda, kwa hiyo hilo si lengo la nchi ya Tanzania pekee, ni lengo ambalo lipo katika nchi zote masikini zinazotaka kuendelea. Sasa jitihada zao badala ya kuzitazama kwa nchi moja moja, inabidi sasa tuzitazame tukiwa kwa pamoja.

“Tukisema tuzitazame kwa pamoja maana yake ni kwamba kuna sehemu tutakuwa na uwezo mkubwa na fursa ya kushiriki kikamilifu, ikiwa kwamba wengine wakituruhusu kwamba ninyi Tanzania endeleeni na jambo hili, sisi tutawategemea ninyi na sisi Tanzania tuwaambie wengine katika hili tutawategemea.

“Kwa hiyo faida yake kubwa tukiwa kwa pamoja na kwa mfano sasa hivi mkutano huu kufanyika Tanzania, licha ya hizo siku mbili ambapo viongozi wengi watakuja hapa nchini, nazungumzia ile ‘impact’ ya sisi kujionyesha katika SADC tupo, na kwamba kama tumesahaulika, tukumbukane na tushirikiane,” alisema.

Profesa Semboja alisema lengo la kuwa katika jumuiya hizo ni kutaka kufaidika katika masuala ya uwekezaji, uzalishaji mali na biashara, na kwamba kupitia jumuiya hio nchi hizo zitatengeneza soko kubwa la pamoja ambalo litaongeza ufanisi wa kibiashara miongoni mwa wanachama.

“Tanzania iko katika hizi jumuiya, tunasema za kimkoa ambazo moja ni Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ya pili ni hii ya SADC, zote zina nia ya kujenga umoja katika masuala mengi ya kiuchumi.

“Mfano Tanzania ni nchi moja ambayo inaweza ikaunganisha SADC na EAC. Kwa hiyo ule utaratibu wa kusema kwamba tutafanya muunganisho wa umeme kutoka Zambia kupitia Tanzania mpaka Kenya, unaweza ukaunganisha EAC na SADC, Tanzania sasa inaweza kuunganisha hizi bodi mbili,” alisema.

Aliongeza kuwa uimara wa jumuiya hiyo pia utasaidia kupatikana kwa umeme wa uhakika miongoni mwa mataifa wanachama kwa kuruhusu miradi mikubwa iliyopo katika baadhi ya mataifa wanachama kutumika katika nchi nyingine mwanachama.

Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa SADC utakaofanyika Dar es Salaam Agosti 17 na 18, ukitanguliwa na vikao mbalimbali kuanzia Agosti 6.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema pamoja na mambo mengine, mkutano huo utajadili changamoto ya majanga ya vimbunga ya vimbunga Kenneth na Idai.

“Inapotokea machafuko, majanga, basi huwa ni sehemu ya mjadala katika mkutano huo. Kwa hiyo hata vimbunga Kenneth na Idai vilivyoleta madhara vitakuwa sehemu ya masuala yatakayojadiliwa,” alisema.

Mkutano huo utatanguliwa na maadhimisho ya Wiki ya Viwanda ya SADC yatakayohusisha shughuli mbalimbali ikiwamo maonesho ya viwanda, huku Tanzania ikijiandaa kutumia jukwaa hilo katika utekelezaji wa ndoto yake ya viwanda.

Alisema katika mkutano huo, Rais Magufuli atakabidhiwa kijiti cha kuongoza jumuiya hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja ujao baada ya Rais wa Namibia, Hage Geingob kumaliza muda wake.

Kwa mara ya mwisho mkutano huo ulifanyika nchini mwaka 2003 chini ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa.