Home Habari MAMA SAMIA ATOA AGIZO ZITO KWA POLISI

MAMA SAMIA ATOA AGIZO ZITO KWA POLISI

615
0
SHARE

NA  FRANCIS GODWIN

MAKAMU wa Rais Mama Samia Suluhu ametoa agizo zito kwa jeshi la polisi nchini kwa kuwataka makamanda wote wa mikoa wa jeshi hilo kuanza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia. RAI linaripoti.

Mama Samia amelitaka jeshi hilo kila mkoa kuhakikisha wanawashughulika na wanaume wanaowafanyia wake zao vitendo  vya ukatili wa kijinsia  na kutoa agizo la kuwajibishwa kwa  makamanda  watakaoshindwa  kazi hiyo.

Makamu wa Rais aliyasema hayo wakati wa hafla ya ufunguzi wa tamasha la 14  la mtandao  wa  jinsia  Tanzania (TGNP -Mtandao ) iliyofanyika kwenye viwanja  vya mtandao huo vilivyopo Mabibo,  jijini Dar es Salaam.

Alisema  pamoja  na  kuwepo kwa harakati mbalimbali  za  kuelimisha jamii  kuondokana na vitendo  vya ukatili kwa  wanawake bado matukio ya ukatili wa kijinsia  yamezidi  kuongezeka na mkoa  wa Dar es Salaam  ni  miongoni mwa  mikoa  yenye matukio mengi ya  ukatili wa  kijinsia.

“Naona  Kamanda wa Kanda Maalumu  ya Dar es Salaam,   Lazaro Mambosasa upo  hapa, naomba  usimamie, nadhani  umesikia taarifa  iliyotolewa  hivi  punde  kuwa vitendo  vya ukatili  wa kijinsia  vipo    hata hapa  Dar es Salaam, sasa  nakuagiza  wewe  na makamanda  wenzako  wote nchini kuwa  serikali haitapenda  kuona  vitendo  hivi  vinaendelea katika jamii  na kama  wewe  utashindwa kuchukua hatua  kwa  kuwawajibisha wa  chini yako  utawajibika  wewe, hivyo anza sasa kupambana  na vitendo hivyo kwa kuagiza  wa  chini yako “alisema.

Hatua  hiyo  inatazamwa kuleta matokeo chanya katika kutokomeza matukio ya  ukatili wa  kijinsia kwa  wanawake  na  watoto  nchini  ingawa baadhi ya mila na desturi zinaruhusu matukio hayo.

“Suala la  mila na  desturi  kwenye jamii  yetu  linapewa  kipaumbele  zaidi  na  kazi ya  mwanaume  ni kuishi kwa upendo  na  mke  wake na sio  kumpiga  mara kwa mara  mwanamke  akipigwa  mara  moja  ama  kuonywa mara moja  inatosha  sio  kumpiga kila wakati ama  kumfanyia  vitendo  vya  kinyama  ….ila  hata  sisi  wanawake  tunapaswa  kuheshimu waume zetu  mimi pamoja na nafasi yangu ya umakamu wa Rais bado mume  wangu nampigia magoti na kumnyenyekea  tuishi kwa  kuheshimiana.”

Alisema   kuwa serikali  iliyopo madarakani inatambua   na kuthamini  umuhimu wa masuala ya  jinsia katika kuchangia na  kuharakisha maendeleo ya nchi  ambapo tangu nchi ipate uhuru  serikali iliweka  misingi thabiti ikiwemo ya  kutunga  sheria, kanuni, taratibu na sera  rafiki na  wezeshi zinazosimamia na kuhimiza  jitihada za kuleta  usawa wa  kijinsia .

“ Sote ni mashahidi  kuwa Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika hivyo  imeridhia mikataba, itifaki na makubaliano mbali mbali ya  kimataifa na kikanda  kuhusu  suala la  kijinsia na uwezeshwaji wa  wanawake  ambao ni utekelezaji wa mpango  kazi  wa mkutano wa Beijing.”

Alisema kuwa hatua  nyingine  ambazo  serikali ya  Tanzania  inachukua ili kuhakikisha  makubaliano na maazimio ya  kimataifa na kikanda yanaakisiwa katika sheria na mipango ya nchi  ni pamoja na kutunga mipango na sheria zinazomlinda na  kumwezesha mwanamke ikiwemo dira ya Taifa  ya maendeleo  2025 na mpango wa  pili  wa Taifa wa maendeleo  wa  miaka  mitano na sheria maalum ya makosa ya  kujamiiana (SOSPA } ya mwaka 1998.

Hata  hivyo anasema kuwa  serikali ipo  kwenye  harakati  ya  kufufua  Benki ya  wanawake  nchini  ili  kuweza  kuwasaidia  wanawake  nchini  kama  njia ya  kuwakomboa  wanawake  hivyo kupitia  benki  hiyo ni lazima  kwa kila mmoja kusaidia  kwa  nguvu zote  kuimarisha  benki  hiyo na  wale  wanaojua  mitaji  ipo  wapi  basi  kujitokeza kuonyesha .

Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Jinsia nchini TGNP –Mtandao Vicensia Shule anasema  kuwa sababu zinazopelekea umasikini huo kukithiri kwa wanawake ni uwekezaji hafifu, miundo mbinu duni, ukuaji mdogo wa Sekta ya kilimo hali ambayo imezidi kudhoofishwa na mgawanyo wa rasilimali usiokuwa sawa uharibifu wa ardhi na athari za tabia nchini.

Kuwa Tamasha la wa Jinsia linalenga kufichua ukosefu wa usawa  unaowakabili wanawake ambao umeweza kuwaathiri katika Sekta ya Afya, Elimu uwakilishi wa kisiasa  na soko la ajira.

Mkurugenzi mtendaji  wa TGNP  Mtandao,  Lilian Liundi  anasema Tamasha  la  mwaka  huu  linaongozwa na mada  kuu  ambayo  ni mageuzi  ya mfumo kandamizi kwa  usawa wa  jinsia na maendeleo  endelevu na  kuwa katika  tamasha  hilo la siku nne  wadau  washiriki watachambua mambo mbali mbali.

Liundi anasema  kuwa  kuwa kwa  ajili  ya  kutambua mchango  wa  mafanikio  ya TGNP Mtandao  uliofanywa na  wanawake  mbali mbali na  taasisi  mbali  mbali  wametumia  tamasha  hilo  kutoa  tuzo kwao.

Kuwa  tuzo  hizo ni kwa  ajili ya  wanachama waanzilishi  wa TGNP Mtandao  ambao  miongoni mwao kuna waliotangulia mbele za  haki  ambao  wote  wamekuwa chachu  ya  mtandao  huo  kwenye  harakati za kupambana na masuala ya  ukatili  wa  kijinsia.

Wanachama hao ni Fides Chale , Marjorie  Mbilinyi, Agripina Mosha, Mary Rusimbi ,Demere  Kitunga, Aseny Muro, Zippora Shekilango, Subira Kilaga  pamoja na hao  pia  wanatambua baadhi ya wanawake  ambao  pia  wamekuwa cha Takwimu hizo ambazo zilitolewa mwaka 2015.