Home Latest News Mambo matano muhimu kwa Rais Magufuli-3

Mambo matano muhimu kwa Rais Magufuli-3

1701
0
SHARE
Rais John Magufuli

NA DK. VERA F. MUGITTU, SCOTLAND

NI vizuri Rais atambue kuwa kuwekeza sana kwenye sekta ya kilimo kuna mipaka yake katika kuleta maendeleo. Ni vizuri kuwekeza pia katika viwanda vya kuzalisha bidhaa nyingine na huduma mbalimbali.

Kufikia mwaka 2008, mchango wa sekta ya kilimo kwenye pato la taifa la nchi ya Malaysia ulishuka toka zaidi ya asilimia 30 mpaka kufikia chini ya asilimia 20. Na mchango wa sekta ya uzalishaji bidhaa za viwandani uliongezeka toka asilimia 27 mpaka 50.

Katika miaka ya sabini serikali ya Malaysia ilifanya uwekezaji wa makusudi katika viwanda kwa kutumia mitaji toka nje na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za kuuza nje ya nchi, hasa bidhaa za teknolojia ya juu(high technology products). Uwekezaji huu ulifanikiwa sana na kuuwezesha uchumi wa nchi hiyo kukua kwa asilimia 10 kwa mwaka katika mwaka 1980.

Mwaka 2008, uzalisaji wa bidhaa za teknolojia ya juu kwa ajili ya soko la nje ulikua toka asilimia 5 ya bidhaa zote zilizouzwa nje na kufikia asilimia 75 kwa mwaka. Hali hii iliendelea hata pale jumla ya bidhaa zote zilizouzwa nje ilipoongezeka toka asilimia 40 hadi 80 ya pato la taifa.

Jambo la kuzingatia hapa ni kujifunza jinsi serikali ya Malaysia ilivyoamua kubadilisha kipaumbele cha uwekezaji wake toka kwenye viwanda vya kilimo kwenda kwenye uzalishaji wa bidhaa nyingine.

Ni vizuri tukumbuke kuwa, kwa miaka 56 sasa nchi yetu imekuwa ikitegemea kilimo kama uti wa mgongo wa uchumi wake. Hivyo sehemu kubwa ya nguvukazi yetu imekuwa ikizalisha bidhaa za kilimo kwa ajili ya chakula na biashara.

Historia inaonyesha kuwa nchi zote duniani zilianza kwa kutegemea kilimo na zilipotaka kuendelea zililazimika kuhamia kwenye vipaumbele vingine. Hii ni kwa sababu kuna ukomo wa matumizi ya nguvukazi katika uzalishaji wa kilimo.

Kwa mfano, ili kulima mahindi ekari moja, muda wa kutayarisha shamba, kupanda, kupalilia na kuvuna, hauwezi kubadilishwa au kufanywa kwa pamoja. Hivyo hata ukiwa na watu tofauti wakufanya kazi hizo, uzalishaji wao ni lazima uwe wa kusubiriana. Pia wingi wao hauongezi ufanisi isipokuwa pale ukubwa wa shamba unapoongezeka.

Hii inamaanisha kuwa lengo la kuongeza ajira kupitia uzalishaji wa kilimo lina kikomo chake kwa sababu wigo wa mgawanyo wa kazi ni mdogo sana. Hivyo ni sahihi zaidi kuwa na watu wachache ambao watalima shamba, watapanda mbegu, watapalilia na kuvuna mahindi kwani mahitaji ya nguvukazi ni ya msimu na yenye kuhitaji ujuzi wa kujirudia mwaka hadi mwaka.

Si rahisi kuwa na mkulima mpya kwenye shamba moja kila mara. Hapa sizungumzii biashara za pembejeo na huduma nyingine ambazo nazo zina ukomo kulingana na kiasi za ardhi inayofaa kwa kilimo. Hali hiini tofauti na uzalishaji wa bidhaa nyingine kiwandani ambapo unaweza kuendesha kiwanda kwa kupata mali ghafi na soko la bidhaa toka nchi nyingine. Na ukazalisha mwaka mzima usiku na mchana.

Pia ni vizuri tukumbuke kuwa hatua za mwanzo za kukuza uchumi wa nchi yetu ziliambatana na kuiunganisha sekta ya kilimo moja kwa moja na uchumi wa dunia. Hivyo tulilazimika kujenga mifumo ya kisera na kiuzalishaji kulingana na mahitaji ya uchumi wa Bara la Ulaya.

Kwa muda mrefu thamani ya mazao na ajira za sekta ya kilimo zimekuwa zikitegemea sana mipango na ufanisi wa uchumi wa nchi nyingine duniani. Tulijikuta tukilazimika kuzalisha kile walichohitaji, tena katika ubora na idadi waliyotaka. Serikali ya kikoloni iliwekeza katika ugani, upatikanaji wa mbegu, teknolojia na miundombinu kadri walivyoona inawafaa.

Na katika hili walifanikiwa kwa kiwango kikubwa. Lakini leo sio lazima kutazama mahitaji yao bali mahitaji ya ndani ya Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla. Hii ikimaanisha kuwa siyo lazima kuwekeza kwenye mazao na bidhaa zile zile za zamani, au kulitazama soko la Ulaya na Marekani kama dira ya uwekezaji nchini.

Ninachotaka kusisitiza hapa ni kuwa, kuwekeza kwa kutegemea mitaji toka nchi za nje kusitulazimishe tufuate vipaumbele vyao. Kuongeza usindikaji wa bidhaa za kilimo nchini ni lazima kuendane na uwezo wa walaji.

Kwa mfano, je Watanzania ni watumiaji wa bidhaa zilizosindikwa?  Je, soko la ndani la bidhaa kama maziwa, nyanya, maharage, matunda n.k yaliyosindikwa lipo?  Haya ni maswali muhimu ya kujiuliza hasa kwa kuwa asilimia zaidi ya 70 ya Watanzania bado inajishughulisha na kilimo na hivyo kujipatia mahitaji yao moja kwa moja toka kwa wakulima na wafugaji.

Hii ni tofauti na nchi ambayo wananchi wake wengi wanajishughulisha na kazi zisizo za kilimo kama viwanda, migodi, ujenzi na kutoa huduma mbali mbali ambao wana kipato cha kuweza kununua bidha za kilimo zilizosindikwa.

Ni vizuri basi Serikali ikatambua kuwa, ili kuwekeza kwenye viwanda vya kusindika bidhaa za kilimo, ni lazima kuendane na kupanua soko la ndani la bidhaa hizo kwa kujenga uwezo wa kifedha wa walaji.

Ni dhahiri kuwa kuongeza viwanda na kuiacha asilimia kubwa ya wafanyakazi hao kuishi vijijini, hakutapanua soko la bidhaa za viwanda hivyo. Ni lazima kuwa na mkakati wa kuongeza idadi ya miji na majiji ili kujenga tabia na fursa ya kutumia fedha (mishahara) katika matumizi zaidi ya kujipatia makazi, malazi, mavazi, matibabu, vyakula, starehe n.k. ili viwanda vipate faida.

Takwimu za mwaka 2014 zilikadiria kuwa Watanzania wapatao milioni 16 tu ndiyo wanaoishi mijini ikiwa ni pungufu ya asilimi 31 ya Watanzania wote. Hivyo ikiwa asilimia 70 ya Watanzania itazalisha malighafi kwaajili ya kuzalisha bidhaa za matumizi ya asilimia 30 tu ya watu, je soko hilo litatosha?

Ni wazi kuwa sera ya kupanua miji haiepukiki kama upanuzi wa viwanda unalenga kutegemea soko la ndani kwa zaidi ya asilimia 30. Na pia kuiacha miji ipanuke yenyewe siyo sahihi, kwani miji ni lazima ipangwe ili kuweka mifumo mbalimbali kama ya maji taka na maji safi, umeme, barabara na huduma nyingine za jamii kwa usahihi.

Kwa kifupi mambo ya msingi katika kuhakikisha sera ya viwanda inaleta manufaa nchini, ni pamoja na Serikali  kuwa na ujasiri wa kuondoa utegemezi wa taifa kwenye kilimo, kupanua soko la mitaji nchini, kujenga uwezo wa nguvukazi, kuboresha mishahara, na kuongeza idadi ya miji na huduma zake, ili kupanua soko la bidhaa za viwandani nchini.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa baruepepe; vera@muvek.co.tz au vfmkenda@gmail.com.