Home kitaifa Mantiki inasema JPM asiwe na mpinzani 2020

Mantiki inasema JPM asiwe na mpinzani 2020

1340
0
SHARE

Na DEOGRATIAS MUTUNGI

MANTIKI ni sayansi ya maisha ya mwanadamu wa kiwango chochote kile cha elimu na hata yule asiye na elimu. Mantiki kwa kiasi kikubwa husaidia mtu, watu au jamii kufikia maamuzi ya hoja kama ni ya kweli au la!

 Pia, hutoa hitimisho la ukweli kuhusu  dhana fulani inayojadiliwa katika jamii,  mwanamantiki hufikiri kwa kujenga hoja na kutoa suluhisho ndani yake.

 Nguli wa Sayansi na hoja za Kimantiki Aristotle (384-322 BC),  anasema katika baadhi ya maandiko yake, “watu wengi ni washabiki na wavivu wa kufikiria na kudadisi, na badala yake hushindwa kujenga hoja zenye mantiki” natumia hoja ya Aristotle katika makala haya kujenga    mantiki wakati tukielekea uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020

Ni sharti tujenge hoja za kimantiki ili kung’amua ukweli wa mambo katika medali za kisiasa, tunahitaji kutumia nadharia za kimantiki kutoa elimu na kusimamia ukweli pale inapobidi kufanya hivyo.

Mantiki yangu inaanza kwa kurejea Katiba  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ukurasa wa 30, yenye sehemu inayosomeka  “Haki ya Uhuru wa Mawazo” ibara ya 18, kifungu kidogo (a), (b), (c) na (d). Ukirejea vifungu vyote tajwa vinaeleza bayana kimantiki haki na uhuru wa mawazo alionao raia wa Tanzania katika kutoa uhuru wake kimawazo na kifikra.

Kwa dhana hiyo, kikatiba na kurejea mawazo ya Aristotle najitenga na kundi la watu wanaoshindwa kujenga hoja zenye mantiki badala yake, nasimama na hoja za kimantiki katika kuwasilisha mawazo mbadala ndani ya makala haya.

Pia, makala haya yanatumia haki ya kikatiba kuwasilisha mawazo ya kimantiki kutokana na mwenendo wa siasa zetu hasa kwa Serikali hii ya awamu ya tano.

kwa uchambuzi usioegemea upande wowote, makala haya yanamulika kwa umakini na weledi safari ya kuelekea uchaguzi mkuu ujao hapo mwakani 2020.

Ni wazi kuwa, kamaTanzania itashiriki uchaguzi mkuu mwakani, uchaguzi ujao kimantiki na kwa mchambuzi yeyote wa masuala ya siasa hapa nchini na nje ya Tanzania anajua na kuelewa fika kuwa utakuwa ni uchaguzi wa namna gani.

Aidha, ieleweke kuwa hili si jambo la kubahatisha wala kupiga ramli bali ni suala la mantiki linalotokana na uwajibikaji wa Serikali ya awamu ya tano kwa wananchi wake.

Tukizingatia hoja za kimantiki na kulinganisha uwajibikaji wa Serikali kwa sasa, inaonesha kuwa uchaguzi ujao utakuwa wa ushindi kwa asilimia zisizopungua 85 katika Serikali ya sasa kurudi madarakani na hii inatokana na uongozi bora na uwepo wa siasa za vitendo zinazoendana na mapinduzi ya kimaendeleo na kiuchumi kwa wazawa.

Inawezekana Serikali ina mapungufu yake katika kusimamia shughuli zake za kila siku ndani ya Serikali lakini, tunapopima mapungufu na mafanikio kwenye mizani, bila shaka mafanikio ni mengi zaidi kuliko mapungufu ya kisiasa ndani ya miaka hii minne.

Lazima tuseme bila kuona aibu ya aina yoyote kuwa Serikali ya awamu ya tano imefanya mambo makubwa ambayo hapo awali hakuna mtanzania aliyetegemea kuona haya tunayoendelea kuyashuhudia nchini mwetu. Ni dhahiri kuwa Serikali imejipambanua kusimamia ndoto na matamanio ya watanzania wengi na hilo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Uwajibikaji uliotukuka wa Serikali ya JPM na taasisi zake, ndio fursa adhimu inayovuta hisia na kuchochea mahaba ya watanzania  wengi kuguswa na kile kinachofanyika sasa katika nadharia ya maendeleo kwa nchi yetu.

Unaweza kusema Tanzania ya sasa ni mpya kwa mantiki ya mapinduzi na mabadiliko ya kimfumo yanayofanyika na yanayoendelea kutekelezwa na Serikali ya awamu ya tano, misingi hii ya uwajibikaji ni fursa kwa watanzania wote bila kubaguana kwa rangi, makabila wala itikadi za vyama vyao.

Ni wazi kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya JPM imeweza kusimamia na kuendeleza miradi mikubwa ilianzishwa katika kipindi cha awamu ya kwanza.

Aidha, Rais Magufuli ameendelea kutekeleza na kusimamia falsafa ambazo mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa anaziishi na kuzihubiri kwa misingi ya utaifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Misimamo ya kiutendaji ya JPM yenye masilahi kwa taifa ni sehemu ya uzalendo kwetu, aidha uamuzi na utekelezaji wa sera na usimamizi wa sheria za ndani kwa misingi ya kulinda rasilimali zetu ni ushindi mwingine wa kiuchumi nchini kwetu.

Kwa maana hiyo, tunaweza kusema na kuamini kuwa huyu ni kiongozi ambaye taifa letu lilimhitaji kwa kipindi kirefu kutokana na hulka zake na misimamo yake katika kusimamia mambo ya msingi yanayogusa uhitaji wa mwananchi wa kawaida.

Kwa sasa Watanzania tukubaliane,  Rais Magufuli amefanya mambo makubwa ya kimaendeleo yanayoonekana na ambayo kwa kipindi kirefu yalikuwa ndio kilio cha wengi.

Aidha, Tanzania chini ya awamu ya tano ndani ya kipindi cha muda mfupi imeweza kufanya mabadiliko makubwa , tofauti na ilivyokuwa inafikiriwa na wengi, awamu ya tano ilijinadi kuwaletea watanzania wanyonge maendeleo na kweli imefanikisha ahadi hiyo kwa asilimia kubwa na inayokubalika na watanzania.

Tanzania ni nchi yenye mfumo wa vyama vingi kwa maana hiyo, vyama vya upinzani  nchini vimekuwa na agenda nyingi tofauti ndani ya ilani zao zinazohusu utekelezaji wa dhana ya maendeleo kwa Watanzania, kwa lugha nyepesi unaweza kusema agenda za upinzani ambazo kimantiki zilikuwa na mashiko katika maendeleo ya nchi zimetekelezwa na kufanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa  katika awamu hii ya tano.

Ingawa nia na dhumuni la chama chochote cha siasa ni kushika dola, lakini pengine tujenge hoja za kimantiki kuwa inapoonekana kuna kiongozi wa kisiasa wa chama kingine anatimiza na kutekeleza kwa wajibu mkubwa maendeleo na matakwa ya kero na vilio vya vyama vingine hatuna budi kumuunga mkono kiongozi mwenye dira endelevu ya kuiletea nchi maendeleo.

Hili ni swali ambalo wazalendo wa kweli tunahitaji kujiuliza na kupata majibu mbadala ambayo hayana chembechembe za kiitikadi wala ukada isipokuwa uzalendo wa kweli katika kulijenga taifa letu.

Tukijenga hoja ya kimantiki na kurejea   maendeleo yaliyofanyika sasa chini ya JPM ndani ya kipindi hiki cha miaka minne, tunaweza kusema kimantiki kuwa, Rais Magufuli asiwe na mpinzani ndani ya chama chake au hata nje ya chama chake katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020 ili aweze kutimiza ahadi zake ambazo kwa kipimo cha sasa zimefanikiwa kwa asilimia kubwa na zinaridhisha kwa kumgusa kila mzalendo wa nchi hii.

Mantiki ya makala haya ni kufafanua na kuelezea umma shughuli za kimaendeleo ambazo awamu ya tano kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kuwafanyia watanzania katika upande wa maendeleo ya dhana ya vitu, nidhamu, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, uwajibikaji kwa viongozi wa umma na mapinduzi ya falsafa na mifumo ya utawala kwa ujumla.

Hoja ya kimantiki tunayo hitimisha nayo katika makala haya ni je? Kama JPM amefanikisha kuleta mabadiliko haya ndani ya kipindi cha miaka minne kwa ufanisi wa hali ya juu, iweje sasa awe na mpinzani katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu ujao wa 2020.

Kwa mantiki hiyo ni rai ya makala haya kuwaambia Watanzania kutafakari na kuchukua maamuzi yenye busara wakati wa kupiga kura kutokana na mazingira ya kimaendeleo na uchumi yalivyo kwa sasa hapa nchini.