Home Makala Mapinduzi sekta ya anga

Mapinduzi sekta ya anga

891
0
SHARE

Mwandishi wetu

SEKTA ya Anga Tanzania leo inatarajiwa kuingia katika mageuzi makubwa, baada ya kuzinduliwa rasmi kwa uwanja mpya wa ndege ujulikanao kama Julius Nyerere International Airport (JNIA) Terminal III, jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi huo utafanywa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli.

Uwanja huo ambao gharama za ujenzi zinatajwa kuwa zaidi ya Sh bilioni 560, utakuwa na uwezo wa kuhudumia wasafiri milioni sita kwa mwaka, tofauti na uwanja wa sasa – JNIA Terminal II, ambao unahudumia wastani wa wasafiri milioni mbili.

Kukamilika kwa uwanja huo, kunaufanya kuwa wa pili kwa ukubwa (kwa uwezo wa kuhudumia wasafiri) eneo la Afrika Mashariki. Uwanja unaoongoza ni Jomo Kenyatta International Airport uliopo Nairobi nchini Kenya.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka jana, uwanja huo mkubwa nchini Kenya, ulihudumia wasafiri milioni 7.1 kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Uwanja wa Terminal III unatajwa kuwa wa kisasa kabisa, na wasafiri watapata huduma zenye viwango na ubora wa kimataifa kuliko wakati wowote katika historia ya usafiri wa anga nchini.

Umuhimu wa uwanja kwa uchumi

Mtaalamu wa masuala ya uchumi nchini, Profesa Samuel Wangwe, amesema kukamilika kwa jengo jipya la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) – Terminal III, kutaendana na ongezeko la matumizi na kwamba Terminal II ilikuwa imezidiwa.

Akizungumza na RAI jana, Profesa Wangwe alisema kutokana na kuzidiwa kwa Terminal II hali ilikuwa mbaya kwa wahudumu na wasafiri, pale inapotokea ndege mbili au tatu zimewasili kwa wakati mmoja.

“Hata kwa wasafiri wenyewe ilikuwa ni kero kubwa, kwa hiyo itakuwa ni ‘service’ (huduma) ambayo itakuwa imefika ‘at the right time’ (katika muda mwafaka) kwa sababu itawezesha ndege kubwa zaidi.

“Kwa wageni ‘first impression is very important’, mgeni anapofika tu anakutana na matatizo, hiyo ‘impression’ inakuwa ni mbaya kwake, kwa hiyo si vizuri afike tu anakuta ‘over-crowding’. Nafikiri kukamilika huku ni kitu kizuri,” alisema Profesa Wangwe.

Alisema kwa sasa Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta nchini Kenya ndiyo mkubwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, na kwamba umekuwa ukivutia ndege nyingi na kwamba kutokana na hali hiyo wasafiri wengi wamekuwa wakipendelea kuutumia.

“Lakini na sisi kwa sababu ni rahisi zaidi kutoka hapa kwenda Malawi, Zambia, Kongo, Rwanda, Burundi, ni ‘entry point’ ambayo inaweza ikachangia Tanzania kuwa kitovu kwenye ukanda huu kama ambavyo ule wa Kenya unapendwa kwa sababu ni mkubwa. Sasa na sisi ni vizuri tuanze kwenda na huo ushindani,” alisema.

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, alisema kufunguliwa kwa jengo hilo kutaongeza uwezo wa kupokea idadi ya ndege, na kuwezesha kupokea ndege kubwa na kuongeza uwezekano wa Serikali kupata mapato.

“Bila shaka ni mojawapo ya miundombinu ya usafiri na hiyo ni mojawapo ya miundombinu inayohitajiwa, mingine ni barabara, reli na kadhalika. Kwa hiyo kufungua uwanja huu maana yake unaongeza uwezo wa kupokea idadi ya ndege na pengine ukubwa wa ndege.

“Vilevile unaongeza uwezekano wa Serikali kupata mapato kwa sababu kila ndege inapotua hapo kuna mapato yanalipwa, lakini unaongeza pia uwezekano wa biashara za bidhaa na huduma kwa maana ya utalii.

“Kama una uwanja mkubwa unaoweza kupokea ndege nyingi zaidi, unaongeza biashara na vitu vingine kama hivyo. Unaongeza uwezekano wa kupata wateja, hizo ndege ambazo zilikuwa zinakuja hapa pengine zije nyingi zaidi ya zile ambazo zilikuwa hazitui hapa kwa sababu hiyo Terminal II ilikuwa ndogo, basi zinaongezeka,” alisema Profesa Ngowi.

Umadhubuti wa uwanja

Akizungumza wiki kadhaa zilizopita Dar es Salaam, msimamizi wa mradi wa ujenzi wa uwanja huo kutoka Wakala wa Taifa wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Barton Komba, alisema jengo la uwanja huo limesanifiwa kwa viwango vya kimataifa vya Daraja C vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA). Hivyo linatarajiwa kwa sasa kuwa kituo kikuu cha usafiri wa anga na kuleta tija kwa Tanzania.

Alisema asilimia 70 ya gharama ya mradi zimetumika kwenye usimikaji wa miundombinu ya mifumo maalumu ndani ya jengo (airport special systems).

“Nasema ukizungumzia uwanja wa ndege, unazungumzia usalama wa abiria na mizigo, gharama iliyotumika katika usalama wa eneo la ndani ya jengo, pamoja na kufanyia kazi eneo la uhamiaji ambalo ni zaidi ya asilimia 70 ya mradi, mitambo ndiyo imechukua sehemu kubwa ya gharama.

“Katika eneo hilo sehemu ya uhamiaji kumefungwa madawati 10 yenye sehemu za kufanyia kazi 40, zenye uwezo wa kuhudumia abiria arobaini wanaowasili au kuondoka kwa wakati mmoja,” alisema.

Komba alisema abiria ambao wanatumia hati za kusafiria za kielektroniki (E-Passport) hawatalazimika kupita kwenye huduma za uhamiaji, bali kwenye lango la kielektroniki (E-Gate), ambako watahakiki hati zao za kusafiria na alama za vidole.

Pia, kwa upande wa ukaguzi wa mizigo (Baggage Handling System HBS), umesimikwa mfumo wa kisasa wenye uwezo wa kukagua mizigo katika madaraja matano tofauti, pamoja na mashine za kukagua mizigo midogo ya mkononi.

Komba alisema kwa daraja la kwanza, mzigo utaangaliwa kwa mashine (scanner), ili kubaini taswira ya kitu kilichomo ndani na daraja la pili utachunguzwa tena kwa kutumia mashine (scanner) zenye nguvu zaidi ya kuona kwa kina.

Alisema daraja la tatu mzigo utachunguzwa kwa kutumia mashine zenye uwezo wa kuchanganua picha ya mzigo iliyoonekana kwenye daraja la pili kwa vipande mia moja tofauti (3 Dimention).

“Hatua itakayofuata ni mzigo kuingia daraja la nne, sehemu ya wataalamu wenye uwezo wa kutafsiri picha iliyoonekana katika madaraja yote yaliyotangulia,” alisema.

Mtaalamu huyo alisema endapo mzigo hautakuwa na dosari, ukifika daraja la nne utapata kibali na hivyo kuingizwa kwenye ndege na kwamba mzigo wenye dosari utaingia daraja la tano ambako hatua za kisheria zitachukuliwa na vyombo vya usalama.

Akifafanua zaidi, Komba alisema eneo la kupokea mizigo lenyewe linayo mikanda minne yenye urefu wa mita 95, ukiwemo mmoja kwa mizigo hatarishi inayotoka sehemu zisizokuwa na uhakika wa usalama kuingia kwenye nchi yetu.

“Miundombinu mingine iliyosimikwa kwa viwango vya kimataifa ndani ya jengo hili ni mifumo ya tahadhari ya zimamoto, utandazaji wa nyaya, ufungaji wa lifti na ngazi zinazoendeshwa kwa umeme pamoja na kazi nyingine za ndani,” alisema.

Kwa mujibu wa Komba, eneo la maegesho ya ndege na viungio vyake lina ukubwa wa mita za mraba 227,000.

Alisema uwanja huo una mwonekano wa kimataifa kutokana na usimikaji wa vivuko vya abiria 12 (Passanger Boarding Bridges) pamoja na ujenzi wa barabara za viungio kuingia na kutoka kwenye maegesho ya ndege.

Kukamilika kwa mradi huu kunatarajiwa kuwa chaguo la ndege nyingi zinazoruka kwenda nchi za Afrika na mabara ya Asia na Ulaya.

Eneo la nje ya jengo ambalo ni maegesho ya magari, ipo nafasi ya kuegesha magari 2,000 kwa abiria wanaokuja na kuondoka uwanjani.

Katika eneo hilo, imesimikwa mifumo ya kupoozea hewa na ya maji ya mvua na maji taka.

Aidha, taa nyingi zimefungwa kwenye maegesho ya magari, jenereta saba kwa dharura, kila moja ikiwa na uwezo wa 2MVA, ili kuhakikisha huduma zinapatikana wakati wote hata inapotokea hitilafu ya umeme.

Komba alisema kazi hiyo imefanywa na Kampuni ya BAM International ya Uholanzi kwa gharama ya Euro milioni 276.7, sawa na zaidi ya Sh bilioni 560 za Tanzania.

Historia ya viwanja vya ndege Tanzania

Uwanja wa kwanza wa ndege kujengwa nchini (Tanganyika wakati huo), ulijengwa na wakoloni Wajerumani mwaka 1918 eneo la Kurasini, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam na kupewa jina la Uwanja wa Ndege wa Mkeja.

Ujenzi wa uwanja wa ndege wa JNIA Terminal I ulianza kwa hatua za awali mwaka 1951, na baadaye ujenzi wa JNIA Terminal II ulianza mwaka 1982 na kukamilika mwaka 1984.  

Oktoba 2005, uwanja wa Dar es Salaam ambao ulijulikana kama Dar es Salaam International Airport (DIA), ulibadilishwa jina na kuitwa Julius Kambarage Nyerere International Airport, ambapo kwa mara nyingine Novemba, 2006 ulibadilishwa jina tena na kuitwa Julius Nyerere International Airport.

Uwanja wa Terminal I una uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 kwa mwaka, Terminal II abiria milioni 1.5, ingawaje kutokana na ongezeko la wasafiri ulilazimika kuhudumia zaidi ya wasafiri milioni 2.

Viwanja 10 vikubwa Afrika na uwezo wake kwa takwimu za mwaka 2018

Uwanja wa Kimataifa wa Oliver Tambo jijini Johannesburg, Afrika Kusini (wasafiri milioni 21.2), Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri (wasafiri milioni 17.5), Uwanja wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Abada, Ethiopia (wasafiri milioni 12.1) na Uwanja wa Ndege wa Cape Town nchini Afrika Kusini (wasafiri milioni 10.7).

Viwanja vingine ni Uwanja wa Kimataifa wa Mohammed V jijini Casablanca, Morroco (wasafiri milioni 9.7), Uwanja wa Kimataifa wa Houari Boumediene jijini Algiers nchini Algeria (wasafiri milioni 7.9), Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, Kenya (wasafiri milioni 7.1), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hurghada, jijini Hurghada nchini Misri (wasafiri milioni 6.6), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Murtala Mohammed jijini Lagos, Nigeria (wasafiri milioni 6.5) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tunis Carthage jijini Tunis, Tunisia (wasafiri milioni 6.2).