Home Latest News Marekani inamtumia Rais Obama kupunguza maadui?

Marekani inamtumia Rais Obama kupunguza maadui?

1281
0
SHARE

obamaHANOI, VIETNAM

MAPEMA wiki hii Rais wa Marekani Barack Obama, amefanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini  Vietnam wakati anaanza ziara ya wiki moja barani Asia. Maofisa nchini Marekani wamesema kuwa ziara hiyo ina lengo la kuboresha ushirikiano wa ulinzi na kiuchumi kati ya mataifa hayo ambayo ni mahasimu wa zamani.

Hata hivyo wadadisi wa masula ya kisiasa wanasema kuwa Marekani inataka kuiunga mkono Vietman na mataifa ya Kusini Mashariki mwa Bara la Asia yaliyopo kwenye mzozo wa kikanda na China.

Katika kile kinachotazamwa kama njia ya kupunguza maadui kwa Marekani, kupitia ziara za Rais Obama imetangaza kuiondolea vikwazo vya mauzo ya silaha hatari Vietnam.

Rais Obama amenukuliwa kwenye ziara hiyo ya Vietnam ambalo ni taifa la kikomunisti alipokuwa akifanya mazungumzo na viongozi wa taifa hilo na kusema kuwa hatua hiyo itamaliza mgogoro wa vita baridi uliokuwepo na Vietnam na Marekani.

Kauli ya Rais Obama inaonyesha dhahiri kabisa kuwa taifa la Marekani kupitia kwa kiongozi huyo linajaribu kuimarisha uhusiano wake na mataifa yaliopo katika bahari ya Pacific, huku China ikiimarisha umiliki wa baadhi ya maeneo.

Hata hivyo Rais Obama ameeleza kuwa ziara hiyo haihusiani na sera za Marekani nchini China. “Inahusu harakati zetu za kutaka kumaliza kile kimetajwa kuwa uhasimu na kuleta ushirikiano na taifa hilo” alinukuliwa Rais Obama lipokuwa Hanoi.

Vietnam ni miongoni mwa mataifa ambayo yamezozana na China kuhusu umiliki wa maeneo yaliyomo katika bahari hiyo. Marekani inasisitiza kuwa na uhuru wa kutembea kusini mwa bahari ya China.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mwaka 2014, mgogoro kuhusu kifaa cha kuchimba mafuta karibu na kisiwa cha Paracel ulisababisha mzozo kati ya vyombo vya baharini vya China na Vietnam mbali na maandamano ya kuipinga China yaliyofanywa nchini Vietnam.

Maofisa wa Ikulu ya Marekani  walisema vikwazo hivyo vya silaha vilivyowekwa tangu mwaka 1984,vitaondolewa iwapo haki za kibinaadamu nchini Vietnam zitaimarika na kukuza uhuru wa kujieleza miongoni mwa wananchi.

Katika kile kinachoonekana kwamba Marekani inamtumia Rais Obama kurejesha ushusiano wake na maadui zake ni kutokana na kuwapo kwa mfululizo wa ziara zinazofanywa na kiongozi huyo kwenye mataifa ambayo awali hayakuwa na uhusiano mzuri na Marekani.

Itakumbukwa miezi michache iliyopita Rais Obama alizuru kwenye taifa la Cuba  ikiwa ni ziara ya kihistoria nchini humo baada ya zaidi ya 88 tangu Rais Calvin Coolidge wa Marekani azuru nchi hiyo mwaka 1928.

Katika ziara hiyo nchini Cuba, rais Obama alipata wasaa wa kufanya mazungumzo na Mkuu wa kanisa Katoliki Papa Francis ambaye aliwezesha mazungumzo ya siri kati Marekani na Cuba mwaka 2014.

Pia, Rais Obama alipata wasaa wa kukutana na kiongozi wa taifa hilo la Cuba, Raul Castro kwa lengo la kuwa na mazungumzo kuhusiana na masuala ya kibiashara, ulinzi na kidiplomasia.

Licha ya wanachama wa chama cha Republican nchini Marekani kuikosoa ziara hiyo wakisema haikufaa kufanyika wakati ambapo familia ya Castro ipo madarakani, lakini ilisaidia kuimarisha uhusiano wa mataifa hayo mawili.

Pia kwenye ziara hiyo ya Cuba Rais Obama alilitaka taifa la Cuba kutoiogopa Marekani, kwa kueleza matumani yake kwamba hali ya Cuba itaimarika, kupitia hotuba iliyorushwa moja kwa moja.

“Wakati umefika kwa Marekani na Cuba kuacha nyuma yaliyopita na kusonga mbele kama marafiki na majirani na kama familia, pamoja  kwa siku za usoni zenye ufanisi. Licha ya siasa hizi zote, watu ni wale wale na Wacuba ni Wacuba,” alinukuliwa rais Obama kwenye ziara hiyo huku akisisitiza kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara dhidi ya taifa hilo tamko lililoshangiliwa na rais wa Taifa hilo

Obama alisisitiza kuwa, kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya taifa hilo la Kikomunisti kutategemeana na uharaka wa mataifa hayo mawili kuondoa tofauti zao hasa katika suala la haki za binadamu.

Obama alielezea hatua hiyo ya kuondolewa vikwazo kwa Cuba kuwa taifa lake halikuiona nchi hiyo kama tishio na kwamba ziara yake nchini humo ililenga kuweka misingi mipya kati ya mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Hata hivyo Obama mara baada ya mazungumzo na Rais Raul Castro, alisema  kutokuwepo kwa harakati za kupigania haki za binadamu nchini Cuba ni jambo litakalo mpatia ugumu kushawishi bunge la Kongresi kuondoa vikwazo vilivyopo dhidi ya Cuba.

Kutokana na ziara hizo ni dhahiri kuwa taifa la Marekani limekuwa likimtumia kiongozi huyo katika kurejesha uhusiano wake na maadui zake wa muda mrefu kama ilivyotokea kwa Cuba ambapo mataifa haya yalikaa kwa zaidi ya miaka 40 pasi na kuwapo maelewano.

Hatua hiyo ya kutokuwapo kwa maelewano baina ya nchi hizo mbili kulisababisha taifa la Marekani kuiita Cuba kama Kitovu cha Ugaidi.

Mbali na hilo taifa la Marekani lilijaribu kumuua  kiongozi wa zamani wa taifa hilo, Fidel Castro bila mafanikio, kwa sasa mataifa haya mawili yamerejesha uhusiano wake wa zamani na vikwazo baina yao vimeondolewa.

Hali hiyo ya kumtumia Rais Obama kutaka kurejesha uhusiano ndiyo inayotumika hata kwenye taifa la Vietnam ikiwa na lengo la kurejesha uhusiano wa mataifa haya ambapo kupitia ziara hiyo tayari Marekani imetangaza kuiondolea Vietnam vikwazo vya silaha.

Swali ambalo halijapatiwa majibu hadi sasa kwenye ziara hiyo ya Rais Obama inayotarajiwa kudumu kwa muda wa siku tatu ni juu ya iwapo Marekani itaingia kwenye makubaliano ya kibiashara kama ilivyokuwa kwa Cuba.