Home Latest News Marekani inaongoza kwa vitambi na unene duniani

Marekani inaongoza kwa vitambi na unene duniani

1659
0
SHARE

Na Hilal K. Sued,

WATU wa nchi tajiri duniani wanazidi kuwa wanene na wenye vitambi na Marekani inaongoza katika hali hiyo, kwa mujibu wa utafiti wa taasisi moja inayoshughulikia masuala ya uchumi iliyotolewa hivi karibuni.

Inatabiriwa kwamba Wamarekani watatu kati wanne, watakuwa na vitambi ifikapo mwaka 2020 na kwamba gharama za matibabu nchini humo zitapanda kwa kiasi kikubwa.

Duniani kote tatizo hili la kiafya limesababisha ongezeko kubwa la mapato katika sekta ya kupunguza uzito (weight loss industry) na pia ubunifu wa mamilioni ya vifaa na mifumo ya mazoezi ya viungo kwa lengo la kupunguza uzito.

Unene na kitambi ni hali ya kiafya ya mtu ambapo mafuta ya ziada mwilini mwa mtu huyo huongezeka kwa kiasi kwamba kinakuwa na athari kubwa kwake – pamoja na kupungua kwa umri tarajiwa.

Ni mojawapo ya tatizo kubwa la kiafya duniani kote katika karne hii ya 21, tatizo ambalo hata hivyo linarekebishika. Ni hali ambayo katika enzi za zamani – na hata sasa hivi katika baadhi ya nchi – lilikuwa linachukuliwa kama ni alama ya utajiri.

Utafiti uliofanywa na taasisi ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi – Organization for Economic Cooperation and Development (OECD) wa nchi 33 zinazojumuisha Marekani, Ulaya Magharibi, Japan, Korea na nyinginezo zenye chumi imara – limesema katika taarifa yake kwamba tatizo la unene na vitambi litazidi kuongezeka ikiwa serikali na hususan wananchi wenyewe hawatachukua hatua za dharura na mipango madhubuti kulikabili tatizo hilo.

Taasisi hiyo yenye makao yake makuu mjini Paris inajulikana zaidi katika kutabiri viwango vya ajira na masuala mengine ya uchumi katika nchi hizo kuliko kupima vitambi vya raia wa nchi hizo.

Lakini athari kubwa za kiuchumi kutokana na ongezeko la vitambi katika nchi hizo ambayo hupunguza maisha ya watu wenye hali hiyo ya afya, pamoja na upotevu wa rasilimali-watu sasa linaanza kuwa changamoto kubwa kwa serikali husika.

Franco Sassi, mchumi mwandamizi wa masuala ya afya katika OECD ambaye alihusika katika utafiti huo anatoa sababu zile zile za msingi za ongezeko za hali hii ya kiafya.

Sassi, aliyewahi kuwa mhadhiri wa uchumi wa chuo kikuu cha London School of Economics na ambaye amehusika katika utafiti huo kwa zaidi ya miaka mitatu anasema: “Bei ya vyakula siku hizi iko chini kuliko huko nyuma, na hasa vyakula ambavyo havileti tija yoyote kwa afya. Aidha watu wanabadili namna wanavyoishi, wana muda mchache sana wa kutayarisha vyakula — hivyo wanakula nje zaidi – kwenye mahoteli na migahawa.”

Aidha, anaongeza, kuna wengi wanatambua athari za tatizo la unene na vitambi, lakini hawafanyi chochote kulirekebisha. Hii inatokana na ukweli kwamba idadi kubwa ya watu hawajui maana halisi ya kuwa na afya njema. Watu wengi, hasa vijana wamekuzwa kwa kula chipsi, mikate na vyakula vya sukari, na si mboga mboga na matunda

Hilo, pamoja na ukweli kwamba watu wengi hawafanyi sana mazoezi siku hizi kama ilivyokuwa zamani ina maana kwamba watu wenye vitambi imeongezeka na kufikia asilimia 70 nchini Marekani mwaka huu, kutoka chini ya asilimia 50 mwaka 1980, ripoti ya utafiti huo inasema.

Ripoti inasema katika kipindi cha miaka 10 ijayo asilimia 75 ya Wamarekani watakuwa na vitambi, na kulifanya taifa hilo kuwa taifa “nene” katika nchi za OECD.

Utabiri huu uko sambamba na  na ule uliofanywa na watafiti wengine nchini Marekani. Asilimia 86 ya watu wazima nchini humo watakuwa na vitambi ifikapo mwaka 2030 iwapo hali hii itaendelea, kufuatana na utafiti wa mwaka 2008 uliofanywa na mtafiti mmoja wa chuo kikuu cha John Hopkins.

Hata hivyo, utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na wanasayansi wa serikali ya Marekani unaonyesha kwamba tatizo la vitambi linapungua, na kwamba theluthi mbili tu ya Wamarekani ndiyo wenye tatizo hilo,na kwamba kiwango hicho kitabakia hivyo hivyo kwa miaka kadha ijayo.

Wakati huo huo, Sassi anasema sababu hizo hizo zinazochochea vitambi nchini Marekani ndiyo pia zinatajwa katika nchi nyingine tajiri na zile zinazoendelea.

Anaongeza: “Ongezeko la tatizo hili la kiafya katika nchi hizi linatisha.”

Kwa ujumla, umri wa mtu mnene mwenye kitambi huwa pungufu kwa miaka 8 had 10 ukilinganisha na mtu mwenye umbo la kawaida, utafiti wa OECD unaonyesha, na kuongeza kwamba pungufu hii ni sawasawa na ile ya mtu anayevuta sigara. Hii inatokana na ukweli kwamba uzito wa mtu husababisha magonjwa ya moyo, aina fulani ya kisukari, magonjwa ambayo huua mamilioni ya watu duniani kote.

Sassi anasema gharama kwa dola za Kimarekani kutokana na tatizo hili la afya, ikijumlisha na gharama kubwa za matibabu na kupotea kwa uzalishaji kazini ni sawasawa na asilimia moja ya uzalishaji mzima (GDP). Kwa nchi za OECD, kiwango hiki ni nusu asilimia. Gharama hizi zinaweza kuongezeka maradufu katika miaka ijayo.

Katika nchi nyingine za OECD viwango vya tatizo la vitambi vinatofautiana sana. Nchini Japan ni asilimia 3 hadi 4 ya watu ndiyo wana tatizo hilo, sawasawa na Korea (ya Kusini).

Hata katika nchi hizo, viwango vinaongezeka, ripoti ya OECD inasema. Nje ya OECD, viwango vya unene na vitambi pia vinapanda. Nchi hizi ni Brazil, China, India na Russia.

* Makala hii imetayarishwa kwa msaada wa vyanzo mbali mbali vya Intaneti.