Home Makala Kimataifa MAREKANI YAWAWEKEA VIKWAZO DK. MACHAR NA WENZAKE

MAREKANI YAWAWEKEA VIKWAZO DK. MACHAR NA WENZAKE

1340
0
SHARE

NEW YORK, MAREKANI


MAPEMA wiki hii Marekani imependekeza kuwa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Dk. Riek Machar, kiongozi wa jeshi la nchi hiyo pamoja na Waziri wa Habari wa Sudan Kusini, wawekewe vikwazo na Umoja wa Mataifa kutokana na wao kuchangia kuongezeka kwa machafuko katika nchi hiyo.

Dk. Machar, pamoja na kiongozi wa Jeshi la nchi hiyo, Paul Malong na Waziri wa Habari,  Michael Makuei, wamewekwa katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, vikwazo ambavyo sasa vitaathiri wao binafsi kwa lengo la kuhakikisha hawaendelezi misimamo yao ya kuhamasisha machafuko katika nchi hiyo. Orodha hiyo iliwasilishwa juzi na Marekani katika kikao cha Baraza hilo na ikaungwa mkono na nchi washirika katika chombo hicho muhimu cha usalama duniani.

Kutokana na mapendekezo ya vikwazo hivyo, Dk. Machar, ambaye kwa sasa anatibiwa nchini Afrika Kusini, pamoja na maafisa hao wengine wawili, watakabiliwa na kutoruhusiwa kusafiri duniani pamoja na mali zao kutaifishwa.

Katika masuala mengine ambayo yamewasilishwa katika mkutano huo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ni kuwepo kwa masharti na vikwazo kwa nchi ya Sudan Kusini, hasa katika suala la ununuzi wa silaha. Lengo halisi la vikwazo hivi ni kujaribu kupunguza kasi ya mauaji ya raia yanayotokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe iliyoanza mwaka 2013.

Katika taarifa hiyo, inaeleza kuwa kitendo cha Dr. Machar kuonekana akijihusisha moja kwa moja na kuhamasisha machafuko hayo licha ya kuwepo jitihda za kusaini makubaliano ya amani, kimeilazimu Marekani kutoa pendekezo hilo. Dk. Machar anaelezwa kukiuka masharti ya makubaliano ya amani yaliyomtaka yeye na kikundi chake kusitisha matumizi ya silaha na vita jambo ambalo hakufanya. Badala yake akaendelea na mashambulizi dhidi ya serikali ya Rais Salva Kiir. Mnamo mwezi Septemba, mambo yalipoonekana kuwa mazito, akaondoka nchini humo.

Inaelezwa pia kuwa, Makamu huyo wa Rais wa zamani, aliingia katika makubaliano na vikosi vya kijeshi vilivyo katika jimbo la Equatoria kwa lengo la kuipindua serikali ya Rais Kiir. Vikundi hivyo vilifanya uvamizi na uporaji katika vijiji, na kisha kutesa raia pamoja na wafanyakazi waliokuwa wakitoa misaada ya kijamii nchini humo.

Kwa upande mwingine, Marekani inamtuhumu Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo Malong, kwa jaribio la kutaka kumuua  Machar. Machar alirejea Juba kufuatia kulazimishwa kufanya hivyo na vyombo vya kimataifa ambavyo vilikuwa vikihitaji nchi hiyo iunde serikali ya umoja wa kitaifa.

Malong, amekuwa kiongozi wa Jeshi la nchi hiyo tangu mwaka  2014, anahusika moja kwa moja na kusudio la kutaka kumuua kiongozi wa upinzani wa nchi hiyo  Riek Machar na inafafanuliwa kuwa, hali akifahamu msimamo wa Rais Kiir, yeye aliendelea na mikakati ya kutumia zana za kijeshi, pamoja na askari wa nchi hiyo katika kufanya shambulizi lililolenga kumuua Machar kwenye makazi yake mwezi wa Julai.

Wakati Machar akirejea Juba, Malong aliamrisha jeshi kufanya uvamizi ili kummaliza Machar, huku akitoa amri pia kuwa zoezi hilo likamilike pasi kumuacha Machar hai. Taarifa hii pia imo katika ripoti iliyowasilishwa kwenye Baraza hilo.

Waziri wa Habari wa nchi hiyo naye anatuhumiwa kwa kutoa amri ya kufungwa kwa Uwanja wa Ndege wa Juba, ikiwa na lengo la kudhibiti Dk. Machar asiingie nchini humo mwezi Aprili mwaka huu.

Pia anaelezwa katika ripoti hiyo kuwa alitangaza kuwa vikosi vyote vya Umoja wa Mataifa vilivyokuwa nchini humo ni wavamizi na akaweka amri kuwadhibiti kutotoka nje ya nchi hiyo bila kibali kutoka serikalini.

Urusi mwaka jana, ilimudu kuzuia Marekani katika jitihada zake za kuwaweka katika orodha ya vikwazo maafisa wa jeshi la Sudan Kusini Malong, pamoja na Kamanda wa vikosi vya Machar, Jenerali Johnson Olony. Katika jaribio hilo la mwaka jana, pia liliungwa mkono na nchi za Angola, China na Venezuela

Kufuatia uamuzi wa sasa, Baraza hilo pia limeweka vikwazo kwa makamanda sita, watatu wakiwa wa vikosi vya serikali na wengine watatu kwa upande wa waasi.

Urusi imetoa taarifa yake kuwa haikubaliani na suala la kuweka vikwazo vya uuzaji wa silaha kwa Sudan Kusini kwa maelezo kwamba kufanya hivyo kutaongeza uadui tu kwa nchi hiyo na jumuiya ya kimataifa.

Balozi Mdogo wa Urusi, Petr Iliichev, alishindwa kufafanua kuhusu kama nchi yake itatumia kura ya turufu kupinga maamuzi hayo ya vikwazo na kafafanua kuwa Urusi inafikiria kwa umakini kabisa kuwa wazo la kuweka kikwazo cha ununuzi wa silaha lilitokana na ushauri mbaya ambao haukuangalia picha kubwa.

“Itaathiri vibaya sana na hasa kuhusu hatua chanya ambazo tumefikia na hasa kuhusu suala la kujenga umoja katika nchi hiyo. Wazo hili kwa makusudi, linaonekana jumuiya ya kimataifa imechukua upande na ni hatari kwa kufikia amani nchini humo,” alisema Iliichev.

Balozi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power, alisema miezi mingi ya mazungumzo na viongozi hao hasimu wa Sudan Kusini, imeshindwa kuleta suluhu na kutokana na hali hiyo, lililobakia ni kuwawekea vikwazo.

“Hakuna sababu nyingine nzuri kuhusu kwa nini tusiweke vikwazo kwa hawa ambao kwa makusudi kabisa, wameamua kusababisha maafa kwa jamii yao. Kufanya hivi ndio kutasaidia kuwapa funzo na huenda ndio ikawa suluhu,” alisema Balozi Power.

Sudan Kusini ni nchi changa kabisa duniani na ilianza kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe mwezi Desemba mwaka 2013, vita vilivyosababisha mauaji ya maelefu ya watu huku watu wengine zaidi ya milioni 2.5 wakijikuta wanakimbia makazi yao.

Nchi hiyo ilipata uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011 ikiungwa mkono na Marekani.

Muafaka wa amani ulisainiwa kati ya mahasimu wawili Rais Kiir na aliyekuwa Makamu wake Machar, mwezi wa nane mwaka huu, na hivyo hali ya amani ikaanza kuleta matumaini. Makubaliano hayo hayakudumu sana kufuatia machafuko mapya yaliyoibuka miezi miwili baadaye.