Home Maoni MARIDHIANO NI JUKUMU LA SERIKALI

MARIDHIANO NI JUKUMU LA SERIKALI

1578
0
SHARE

Tangu kuundwa kwa Tanzania, iliyokuwa chini ya Rais wa kwanza,  Mwalimu Julius Nyeyeye, nchi yetu imekuwa ikisifika kuwa yenye utulivu, salama na amani.

Kwamba Tanzania ina zaidi ya makabila 120, lakini yanaishi pamoja kwa amani na maelewano.

Migogoro tunayoisikia sasa baina ya makundi mbali mbali wakulima na wafugaji, wachimbaji wakubwa na wachimbaji madini wadogo, na migogoro kati ya vijiji na mamlaka za serikali, haikuwepo na kama ilikuwapo, basi ilitatuliwa kwa mazungumzo. Hiyo ndiyo Tanzanian tuliyoizoea.

Jambo la kushtusha ni mambo yanayoendelea katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na migongano kati ya makundi ya kijamii, vyama vya saisa na taasisi za serikali, hususan, Jeshi la Polisi kiasi kwamba hivi sasa imejengeka hofu kwamba polisi ambao kazi yao kuu ni Usalama wa Raia, hawatekelezi majukumu yao ipasavyo, sisi hatuliamini hilo.

Hata hivyo kumekuwapo na ongezeko la watu kuumizwa, kuharibiwa mali zao, kuuwawa katika mazingira ya kutatanisha, kimeibuka  kikundi cha ‘watu wasiojulikana’ ambao wamesababisha sintofahamu na kujenga hofu katika jamii.

Tunaunga mkono  wito uliotolewa na taasisi mbali mbali, ikiwamo Baraza la Maskofu wa Kanisa Katoliki (TEC), Kituo cha  Demokrasia Tanzania (TCD), na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kwamba ipo haja ya kuyatolea kauli ya pamoja matukio mabaya yanayoharibu sifa nzuri za nchi yetu.

Tunakubaliana na wito wa kutaka kuwapo kwa mardhiano katika nchi yetu ili kuondo hofu na woga ambavyo vinatawala hivi sasa. Ipo haja ya wadau wote wa amani kuungana katika kulifanikisha hili la kuleta maridhiano yatakayobeba sura ya utaifa.

Yaliyotokea Kibiti, Mkranga na Rufiji, mkoani Pwani si ya Tanzania hii ya Mwalimu Nyerere. Kama hiyo haitoshi kumekuwapo na mauaji ambayo yanayobebeshwa sura ya kisiasa, pamoja na dhuluma mbali mbali dhidi ya wananchi wanyonge.

Tungependa kuona mambo haya yanakwisha na kuirejesha Tanzania katika mstari wake wa kuwa kisima cha utulivu na amani. Viongozi wetu wa dini na siasa, pamoja na taasisi zake, vyombo vya Ulinzi na Usalama, na wawakilishi wa Bunge na Baraza la Wawakilishi, wakae pamoja na  kutafakari namna sahihi ya kurudi katika Tanzania ya amani na utulivu isiyo na mawaa.

Tunaamini kwa sasa Watanzania tulio wengi tuna  hofu na usalama wa maisha na mali, ukweli ni kwamba hatukuzoea matukio kama haya, ni lazima tujiulize tunakokwenda kama nchi ni wapi na ni kwa namna gani tutarejea kwenye mstari kama hakutafanyika maridhiano  hasa ya kisiasa?

Tuna imani kwamba mamlaka husika zitaitikia wito wa kuwapo kwa mkutano wa maridhiano kama taifa la Tanzania, tuangalie na kujitathimini tunataka kujenga taifa la namna gani. Hata hivyo  ni lazima kila mtu akumbuke kwamba mahali pekee pa salama kwa ajili ya ustawi wa wananchi, mahala penye usalama kwa ajili ya vijana na watoto wetu ni Tanzania.

Tuna amini kwamba Serikali yetu itabeba dhamana ya kuitisha Mkutano wa Maridhiano  utakaokuwa shirikishi kwa makundi yote, kwa kuzingatia kwamba ndiyo inayobeba uzito wa masuala yote yanayotusibu kama nchi.

Mungu Ibarika Tanzania.