Home Makala Marufuku mifuko ya plastiki ilivyoibua fursa

Marufuku mifuko ya plastiki ilivyoibua fursa

1793
0
SHARE

Na Robert Hokororo

KATAZO la mifuko ya plastiki lililotangazwa na Serikali na kuanza rasmi kutekelezwa kwa mujibu wa sheria Juni mosi, mwaka huu limeibua fursa mbalimbali kwa wananchi.

Pengine kila jambo jipya au mabadiliko yoyote yanayotangazwa yanaweza kuwa changamoto katika jamii lakini kadiri wananchi wanavyoelimishwa ndivyo changamoto hizo huweza kutatuliwa.

Serikali ilikuwa na nia ya dhati kupiga marufuku uingizaji nchini, usafirishaji nje ya nchi, uzalishaji, uuzaji, usambazaji, uhifadhi na matumizi ya mifuko ya plastiki Tanzania Bara.

Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa kanuni za kupiga marufuku mifuko ya plastiki za mwaka 2019 chini ya kifungu cha 230 (2) (f)) ili kulinda afya ya binadamu, wanyama na mazingira dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya mifuko hiyo.

Kutokana na madhara hayo, wananchi wameanza kuitikia wito wa katazo hilo na kutekeleza kwa kuachana na mifuko ya plastiki na badala yake wanatumia mifuko mbadala inayotengenezwa kwa malighafi isiyokuwa ya plastiki.

Ipo mifuko mbadala ya aina mbalimbali na ambayo inazingatia utunzaji wa mazingira ikiwemo ‘non-woven’ pamoja na inayotengezwa kwa vitambaa, katani (gunia), turubai, ukili (vikapu) na karatasi.

Hivi karibuni, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan,  akifafanua kuhusu katazo hilo anawataka wananchi kutumia nafasi hii ya kipekee kwa kuzalisha mifuko mbadala iliyoruhusiwa na Serikali.

Samia anasema kunapokuwa na viwanda vya mifuko mbadala ya kubebea bidhaa kutasaidia wananchi kuacha kutumia mifuko ya plastiki iliyokatazwa kisheria.

Anaongeza kuwa kwa kutumia fursa hiyo kutasaidia kuzalisha ajira kwa wingi na hivyo kuinua uchumi kwa wananchi hususan wanawake ambao watatengeneza mifuko mbadala ikiwemo vikapu.

Katika kuhakikisha inakuwepo mifuko mbadala ya kutosha Serikali imekuwa ikichukua hatua madhubuti kuhakikisha soko la mifuko mbadala linakua kwa kasi. Itakumbukwa kwa nyakati tofauti imeweza kukutana na wadau walio tayari kuzalisha mifuko hiyo kwa wingi.

Aidha Serikali pamoja na kufanya operesheni ya kuhakikisha sheria ya katazo la mifuko linatekelezwa ipasavyo imekuwa ikifanya zoezi la ufuatiliaji na ukaguzi wa viwanda vinavyozalisha mifuko mbadala.

WAZIRI MAKAMBA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba,  amekuwa akifanya ziara katika maendeo mbalimbali nchini kukagua viwanda hivyo.

“Kabla ya Serikali kutangaza hatua ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki, ulifanyika utafiti na maandalizi ya mifuko mbadala. Uwezo wa kuzalisha upo na mifuko ya karatasi inayotumika Kenya na Rwanda inatumia malighafi inayozalishwa Mgololo-Iringa nchini Tanzania,” anasema Makamba.

Akiwa katika Kiwanda cha African Paper Bag Ltd kilichopo katika eneo la Chango’mbe, Dar es Salaam, Makamba anasema ameridhishwa na kasi ya uzalishaji wa mifuko mbadala ambapo inaelezwa kuwa kinazalisha mifuko ya karatasi laki tano kwa siku na mifuko ya ‘Non-Woven’ ipatayo laki moja kwa siku.

“Wajibu wa Serikali si kupiga marufuku na kuondoka, tunahakikisha tunaziba pengo la mifuko ya plastiki kwa kuweka mazingira wezeshi kwa uzalishaji wa mifuko mbadala yenye ubora na bei nzuri kwa watu. Lazima tuwasaidie wajasiriamali, wafanyabiashara na wenye viwanda kuzalisha mifuko ili kuziba pengo la mahitaji kwa kuwa na mifuko mbadala yenye ubora na viwango vinavyokidhi mahitaji,”  anasisitiza.

Makamba ambaye pia amekuwa akikutana na wafanyabiashara wa mifuko mbadala anafafanua kuwa kuondoka kwa mifuko ya plastiki kumeibua fursa mpya za uchumi shirikishi, ajira mpya, mapato mapya.

WAZALISHAJI MIFUKO MBADALA

Anasisitiza kuwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linaandaa viwango vipya vya ubora wa mifuko hiyo mbadala vitakavyobainisha malighafi na unene wa mifuko mbadala itakayozalishwa ili kuwalinda watumiaji ikiwa ni pamoja na taarifa zitakazoainisha mfuko husika una uwezo wa kubeba kilo ngapi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Kampuni ya African Paper Bag Ltd, Hasnai Mawji, anaweka wazi kuwa kwa sasa mahitaji ya mifuko kiwandani kwake ni makubwa sana na wameongeza uzalishaji kwa kuagiza mashine mpya mbili sambamba na kuongeza idadi ya watumishi kukidhi mahitaji kwa sasa.

“Kiwanda chetu kinazalisha mifuko tani 100 kwa mwezi na tumeagiza mashine nyingine ili kuongeza uzalishaji wa kufikia tani 200 kwa mwezi na sasa tunafanya kazi masaa 24, shifti zimeongezeka kutoka shifti 1 ya awali na sasa tuna shifti 3, tumeongeza ajira kutoka watu 30 awali na sasa tuna watumishi 60 na lengo ni kufika watumishi 100,” anasisitiza Mawji.

Kiwanda kingine ambacho kimetembelewa na Makamba ni Green Earth Paper Product Ltd kilichopo katika eneo la Mbezi Makonde, Dar es Salaam chenye uwezo wa kuzalisha mifuko 22,000 kwa siku.

Robert Mosha ambaye ni mkurugenzi wa kiwanda hicho, anasema katika kipindi cha miezi mitatu kabla ya zuio walipokea oda ya Sh milioni 124 na katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya zuio la mifuko ya plastiki wamepokea mahitaji yenye thamani ya Sh milioni 124 ikiwa ni kiwango cha juu ukilinganisha na mahitaji ya awali kwa kipindi kifupi.

Wazalishaji wengine wa mifuko mbadala hivi karibuni walinukuliwa wakisema wamejipanga kukidhi mahitaji ya soko popote nchini na kwa muda muafaka ambayo pia inakwenda sambamba na ukuaji wa uchumi.

Katika kuona umuhimu wa mahitaji kwa wananchi wazalishaji hao wanasema kuwa wameanza kutoa mafunzo kwa watu mbalimbali ambayo ni fursa ya kujitengenezea kipato.

Kwamba wanawahakikishia wananchi na wadau mbalimbali wanaotaka kuwekeza kwenye fursa hii kuwa malighafi inapatikana sehemu mbalimbali nchini na wanatoa wito kwa Watanzania kuona fursa ya mifuko mbadala kuwa ni sehemu ya kujitengenezea kipato.

Aidha katika kuhamasisha uzalishaji kwa wingi wa mifuko mbadala, wanashauri Serikali na taasisi husika kutoa mafunzo na teknolojia ya kuitengeza huku wakiomba halmashauri zielekeze misaada na mikopo kwa vikundi au watu wanaoingia kwenye uchumi huu mpya wa mifuko hiyo.

NAIBU WAZIRI SIMA

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Mussa Sima, akiongoza operesheni ya kufuatilia utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki anatoa wito kwa wafanyabishara kutowakandamiza wananchi kwa bei isiyokuwa rafiki.

“Ndugu wafanyabiashara tusiwakomoe Watanzania wasije kuona sasa mifuko hii mbadala ni ghali na kuona ni bora turudi katika mifuko ya plastiki ambayo imepigwa marufuku,” anatahadharisha.

Hata hivyo anawataka wananchi hususan vikundi vya wanawake kutumia fursa hiyo kusuka vikapu ambavyo watawauzia wananchi wenye kuhitaji mbadala wa mifuko ya plastiki hivyo kujipatia kipato.

“Tukumbuke zamani tulizoea kubeba vikapu na kwenda sokoni sasa tunavyotumia vikapu hivi tutajenga utamaduni kama wa zamani na kuachana na mifuko ya plastiki ambavyo ina madhara makubwa kwa binadamu, wanyama na mazingira,” anasema.

Operesheni ya kukagua utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki linaloratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ilibaini wananchi wengi kupata uelewa wa madhara ya mifuko ya plastiki.

Wananchi mbalimbali wameitikia wito wa kuanza kutumia mifuko mbadala katika masoko na maduka ambapo wamesema wanaipongeza Serikali kwa kuliona hilo na kupiga marufuku mifuko hiyo.

Pamoja na hayo ni dhahiri kuwa katazo la mifuko ya plastiki ambalo lilitangazwa Aprili 9, mwaka huu bungeni na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mbali ya kusaidia kuondokana na madhara ya mifuko lakini pia linainua uchumi na ustawi wa Watanzania.

Mwandishi wa makala haya ni Ofisa Habari Ofisi ya Makamu wa Rais