Home Makala MARUFUKU YA NGUO ZA MITUMBA: ITAINUA SEKTA YA UZALISHAJI NGUO NA...

MARUFUKU YA NGUO ZA MITUMBA: ITAINUA SEKTA YA UZALISHAJI NGUO NA KUREJESHA HESHIMA

795
0
SHARE
Wananchi wakiendelea na biashara ya mitumba

NA HILAL K. SUED


MAPEMA wiki hii Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitangaza kwamba muda umewadia kuondokana na nguo za mitumba, kutokana na kuwepo nchini viwanda kadha vya nguo.

Aidha, Waziri Mkuu alisema uwepo wa viwanda hivi utasaidia wakulima wa pamba kuwa na soko la kutegemewa na hivyo akatoa wito kwao kuzalisha zao hilo kwa wingi ili sekta ya nguo ipate malighafi ya kutosha.

Alisema viwanda vya nguo vilivyopo vinaweza kuzalisha nguo za aina mbalimbali, tena kwa bei nafuu na hivyo kuondokana kabisa na uagizaji wa nguo za mitumba kutoka nchi za nje.

Hakuna haja ya kusema hapa kwamba biashara na matumizi ya nguo za mitumba haitatoweka ghafla – itachukua miaka mingi na itategemea kuwapo kwa nia ya dhati nyuma ya tangazo hili la Waziri Mkuu.

Nguo za mitumba – nguo zile zilizokwisha valiwa na watu wa nchi za nje, hususan Ulaya na Marekani na baadaye kukusanywa na kuingizwa nchini katika marobota, au ‘mitumba’ (bales) – zimekuwapo nchini tangu kabla ya uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita, ingawa awali zilikuwa zinaingizwa kwa njia za magendo kutokana na marufuku iliyokuwapo kuhusu uingizaji.

Zilikuwa zinaingia nchini kutoka Congo, Rwanda na Burundi, kwani nchi hizo zilikuwa zinaruhusu uagizaji wake. Aidha, kutokana na kwamba shehena za bidhaa hiyo kwenda nchi hizo zilikuwa zikipitia Reli ya Kati, basi ulikuwapo uwezekano mkubwa wa baadhi ya bidhaa hiyo kuingia katika soko la ndani kinyume cha sheria.

Aidha, baadhi nguo za mitumba zilikuwa zinaruhusiwa kuingia kama misaada kupitia taasisi za dini (na makundi mengine) kwa ruhusa na masharti maalumu na kusamehewa ushuru wa forodha na kodi ya mauzo (Customs Duty na Sales Tax). Sharti kubwa nguo hizo zisiuzwe, zigawiwe bure kwa watu kama misaada, ingawaje masharti yalikuwa yanakiukwa na nguo hizo kuuzwa kibiashara.

Hii ilitokana na ukweli kwamba, kwa ujumla soko la nguo hizo lilikuwa kubwa sana hapa nchini kwa sababu ya urahisi (kwa bei) kwani nguo mpya zilikuwa ghali, hasa kwa wale wa kipato cha chini.

Tangazo la Waziri Mkuu Majaliwa limekuja miaka 33 baada ya tangazo la Waziri Mkuu wa zamani, Salim Ahmed Salim, mwaka 1984, alipotoa agizo la kuhalalisha biashara ya mitumba kutokana na sababu kwamba wananchi wengi kushindwa kununua nguo mpya.

Alitoa agizo hilo akiwa katika ziara yake mikoa ya kusini, alipoona wananchi vijijini, hususan watoto wakiwa katika nguo zilizochanika na wengine bila nguo kabisa, hali aliyosema ilikuwa inasikitisha sana.

Aidha, tusisahau pia kwamba wakati huo ulikuwa na katika kipindi kigumu sana kwa Tanzania kiuchumi, ikiwamo hali ile ya ukosefu wa bidhaa muhimu.

Wengi waliuona uamuzi huo wa serikali ulikuwa wa busara na kuanzia hapo biashara ya uingizaji wa nguo za mitumba ilirasimishwa, ingawa mijadala iliendelea kuwapo kuhusu masuala ya kushuka kwa hadhi ya nchi.

Hoja ilikuwa ni kwamba, miongo miwili tu baada ya kuondokana na utawala wa wakoloni tumeshindwa hata kujivika, hadi tuagize nguo ambazo wakoloni hao hao walikwisha kuzivaa?

Hata hivyo, sasa hivi kumeanza kujitokeza mawazo mapya. Mapema mwaka jana viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waliamua kupiga marufuku uagizaji wa nguo za mitumba, katika utekelezaji utakaoanzia baada ya miaka mitatu – yaani ifikapo 2019.

Hivyo basi, agizo la Waziri Mkuu Majaliwa bila shaka linatokana na makubaliano hayo. Ilidaiwa marufuku ilikuwa ni moja ya hatua zilizopendekezwa katika azma ya kuinua viwanda vya nguo katika kanda ya Afrika Mashariki.

Serikali za Afrika Mashariki zimekuwa zikilaumu uagizaji wa nguo na viatu vilivyotumika kama moja ya sababu zinazofanya viwanda vya nguo na ngozi kusambaratika na hivyo kuwanyima wananchi wazalendo nafasi ya ajira.

Hata hivyo, wengi hawaamini iwapo mapendekezo hayo yatatekelezwa, kwani kumekuwapo na upinzani mkubwa kutoka Marekani na nchi za Ulaya ambazo husambaza nguo kuukuu takriban duniani kote, hasa katika nchi masikini.

Aidha, wataalamu wengine wanasema marufuku ya mara moja haitaweza kurejesha uwezo wa nchi hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kufufua au kuanzisha viwanda vyao vya nguo.

Inakadiriwa kwamba, biashara ya nguo za mitumba duniani imefikia Dola za Kimarekani bilioni 3.7 kwa mwaka, wakati mwaka 2014 nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pekee ziliagiza nguo za mitumba zenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 300 kutoka nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani, hivyo kuifanya bidhaa hiyo kuwa na soko kubwa na la nguvu katika eneo hili la Afrika.

Aidha, bidhaa hiyo, mbali na kuziingizia serikali za nchi hizo mabilioni kutokana na kodi mbalimbali, pia imekuwa ikitoa ajira kwa maelfu ya watu wa nchi hizo. Lakini utegemezi wa bidhaa hiyo kutoka nje umeleta athari kubwa katika kuviangamiza kabisa viwanda vya nguo vya nyumbani.

Hata hivyo, wanaounga mkono upigwaji marufuku wa nguo za mitumba wanasema kutasaidia kuimarisha chumi za nchi za Jumuiya ambazo tayari ziko katika mageuzi makubwa kuelekea chumi za viwanda na uzalishaji wa viwango vya juu.

Aidha, wengine wanasema kutarejesha hali ile ya kujivunia miongoni mwa wananchi wa jumuiya, kwani “hakuna mtu anajisikia vyema wakati amevaa nguo ambazo watu wengine wamezitupa.”